Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 9:3-13

2 Samweli 9:3-13 SRUV

Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu yeyote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi mfalme Daudi akatuma watu, na kumwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumishi wako! Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, babu yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima. Akasujudu, akasema, Mimi mtumishi wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi? Ndipo mfalme akamwita Siba, mtumishi wa Sauli, akamwambia, Mali yote yaliyokuwa ya Sauli na ya nyumba yake nimempa mjukuu wa bwana wako. Nawe utamlimia nchi hiyo, wewe, na wanao, na watumishi wako; nawe utamletea mjukuu wa bwana wako matunda yake, apate chakula ale; lakini Mefiboshethi, mjukuu wa bwana wako, atakula chakula mezani pangu siku zote. Basi huyo Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumishi ishirini. Ndipo Siba akamwambia mfalme, Mimi, mtumishi wako, nitatenda hayo yote kama bwana wangu, mfalme, alivyoniamuru. Na kuhusu Mefiboshethi, mfalme alisema, Atakula mezani pangu, kama mmojawapo wa wana wa mfalme. Huyo Mefiboshethi alikuwa na mwana mdogo, jina lake akiitwa Mika. Na watu wote waliokaa nyumbani mwa Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi. Basi Mefiboshethi akakaa Yerusalemu; maana alikuwa akila chakula siku zote mezani pa mfalme; naye alikuwa na kilema cha miguu yote miwili.