2 Samueli 24:18-25
2 Samueli 24:18-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku hiyohiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, “Panda juu, ukamjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu, katika kiwanja cha kupuria nafaka cha Arauna, Myebusi.” Basi, Daudi akapanda juu kufuatana na neno la Gadi kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru. Arauna alipoangalia upande wa chini alimwona mfalme akimkaribia pamoja na watumishi wake, naye akatoka, akaenda na kumsujudia mfalme, akainama mpaka chini ardhini. Kisha Arauna akamwuliza mfalme, “Kwa nini bwana wangu mfalme amenijia mimi mtumishi wake?” Daudi akamjibu, “Nimekuja kununua uwanja wako wa kupuria nafaka ili nimjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu ili tauni iliyowakumba watu ikome.” Naye Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme, chukua chochote unachoona kinafaa na utolee sadaka. Mimi nawatoa fahali hawa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na vifaa hivi vya kupuria na nira za ng'ombe kuwa kuni. Hivi vyote, ee mfalme, nakupa. Natumaini Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atapokea sadaka yako kwa wema.” Lakini mfalme akamwambia Arauna, “La! Wewe hutanipa chochote. Mimi nitavinunua kwako kwa thamani yake. Sitamtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa ambazo hazijanigharimu kitu.” Hivyo, mfalme Daudi alinunua uwanja wa kupuria na fahali kwa fedha shekeli hamsini. Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu mahali hapo na kumtolea sadaka za kuteketezwa na za amani. Basi, Mwenyezi-Mungu akayakubali maombi kwa ajili ya nchi, na ile tauni iliyowakumba Waisraeli ikakoma.
2 Samueli 24:18-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie BWANA madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea kama alivyoagizwa na Gadi, kama BWANA alivyoamuru. Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifudifudi hadi chini. Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumishi wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Nimekuja kununua kwako kiwanja hiki cha kupuria, ili nimjengee BWANA madhabahu, ili tauni ipate kuzuiliwa kwa watu. Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, natoa ng'ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng'ombe, viko kwa kuni, vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na akukubali. Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo; lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake; wala sitamtolea BWANA, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa isiyonigharimu chochote. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng'ombe kwa shekeli hamsini za fedha. Naye Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi BWANA aliiridhia nchi, na tauni ikazuiliwa katika Israeli.
2 Samueli 24:18-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie BWANA madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, kama BWANA alivyoamuru. Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifulifuli hata nchi. Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumwa wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Makusudi ninunue kwako kiwanja hiki, ili nimjengee BWANA madhabahu, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa katika watu. Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, ng’ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng’ombe, viko kwa kuni, vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na akukubali. Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo; lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake; wala sitamtolea BWANA, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa nisizozigharimia. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng’ombe kwa shekeli hamsini za fedha. Naye Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi BWANA aliiridhia nchi, na tauni ikazuiliwa katika Israeli.
2 Samueli 24:18-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Panda ukamjengee BWANA madhabahu kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi.” Kwa hiyo Daudi akakwea kama vile BWANA alivyokuwa ameamuru kwa kinywa cha Gadi. Arauna alipotazama na kumwona mfalme na watu wake wakija kumwelekea, alitoka nje na kusujudu mbele ya mfalme kifudifudi, akiuinamisha uso wake ardhini. Arauna akasema, “Mbona bwana wangu mfalme amekuja kwa mtumishi wake?” Daudi akajibu, “Kununua sakafu yako ya kupuria, ili niweze kumjengea BWANA madhabahu, ili tauni iliyo katika watu iondolewe.” Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme na achukue chochote kinachompendeza na akitoe sadaka. Hapa kuna maksai kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia kuna miti ya kupuria na nira za ngʼombe kwa ajili ya kuni. Ee mfalme, Arauna anatoa vyote hivi kwa mfalme.” Pia Arauna akamwambia mfalme, “BWANA Mungu wako na akukubali.” Lakini mfalme akamjibu Arauna, “La hasha, nasisitiza kuvilipia. Sitatoa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA Mungu wangu isiyonigharimu chochote.” Kwa hiyo Daudi akanunua ile sakafu ya kupuria nafaka na maksai, akazilipia shekeli hamsini za fedha. Kisha Daudi akamjengea BWANA madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha BWANA akajibu kwa ajili ya nchi, nayo tauni ikakoma katika Israeli.