2 Samweli 24:18-25
2 Samweli 24:18-25 SRUV
Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie BWANA madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea kama alivyoagizwa na Gadi, kama BWANA alivyoamuru. Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifudifudi hadi chini. Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumishi wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Nimekuja kununua kwako kiwanja hiki cha kupuria, ili nimjengee BWANA madhabahu, ili tauni ipate kuzuiliwa kwa watu. Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, natoa ng'ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng'ombe, viko kwa kuni, vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na akukubali. Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo; lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake; wala sitamtolea BWANA, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa isiyonigharimu chochote. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng'ombe kwa shekeli hamsini za fedha. Naye Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi BWANA aliiridhia nchi, na tauni ikazuiliwa katika Israeli.