2 Samueli 23:1-7
2 Samueli 23:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Yafuatayo ni maneno ya mwisho ya Daudi. Ni ujumbe wa Daudi mwana wa Yese; ujumbe wa mtu ambaye Mungu alimfanya awe mkuu. Mungu wa Yakobo alimteua Daudi kuwa mfalme na maneno yake Waisraeli walifurahi kuyaimba. “Roho ya Mwenyezi-Mungu imesema kwa njia yangu, aliyaweka maneno yake kinywani mwangu. Mungu wa Israeli amesema, Mwamba wa Israeli ameniambia, ‘Mtu anapowatawala watu kwa haki, atawalaye kwa kumcha Mungu, yeye ni kama mwanga wa asubuhi, jua linapochomoza asubuhi isiyo na mawingu; naam, kama mvua inayootesha majani ardhini’. Hivyo ndivyo Mungu alivyoujalia ukoo wangu. Maana amefanya nami agano la kudumu milele; agano kamili na thabiti. Naye atanifanikisha katika matakwa yangu yote. Lakini wasiomcha Mungu wote ni kama miiba inayotupwa tu, maana haiwezi kuchukuliwa kwa mkono; kuishika, lazima kutumia chuma au mpini wa mkuki. Watu hao wataangamizwa kabisa kwa moto.”
2 Samueli 23:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi haya ndiyo maneno ya mwisho ya Daudi. Daudi, mwana wa Yese, anena, Anena huyo mtu aliyeinuliwa juu, Yeye, masihi wake Mungu wa Yakobo, Mtungaji wa nyimbo za Israeli mwenye kupendeza; Roho ya BWANA ilinena ndani yangu, Na neno lake likawa ulimini mwangu. Mungu wa Israeli alisema, Mwamba wa Israeli aliniambia, Atawalaye wanadamu kwa haki, Akitawala katika kicho cha Mungu, Atakuwa kama nuru ya asubuhi jua lichapo, Asubuhi isiyo na mawingu. Likichipuza mimea ardhini, Kwa mwangaza baada ya mvua; Je! Sivyo ilivyo nyumba yangu mbele za BWANA? Kwa kuwa amefanya nami agano la milele; Ina taratibu katika yote, ni thabiti, Maana ni wokovu wangu wote, na shauku langu lote. Lakini hatawachipuza watu wasiofaa; Watakuwa wote kama miiba ya nyikani ya kutupwa, Maana haichukuliki kwa mkono, Mtu atakayeigusa hiyo, Na awe na chuma na mpini wa mkuki, Nao watateketezwa papo hapo kwa moto.
2 Samueli 23:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi haya ndiyo maneno ya mwisho ya Daudi. Daudi, mwana wa Yese, anena, Anena huyo mtu aliyeinuliwa juu, Yeye, masihi wake Mungu wa Yakobo, Mtungaji wa nyimbo za Israeli mwenye kupendeza; Roho ya BWANA ilinena ndani yangu, Na neno lake likawa ulimini mwangu. Mungu wa Israeli alisema, Mwamba wa Israeli aliniambia, Atawalaye wanadamu kwa haki, Akitawala katika kicho cha Mungu, Atakuwa kama nuru ya asubuhi jua lichapo, Asubuhi isiyo na mawingu. Lachipuza majani mabichi juu ya nchi, Kwa mwangaza baada ya mvua; Je! Sivyo ilivyo nyumba yangu mbele za BWANA? Kwa kuwa amefanya nami agano la milele; Ina taratibu katika yote, ni thabiti, Maana ni wokovu wangu wote, na shauku langu lote. Lakini hatawachipuza watu wa ubatili; Watakuwa wote kama miiba ya nyikani ya kutupwa, Ambayo haivuniki kwa mkono, Mtu atakayeigusa hiyo, Na awe na chuma na mpini wa mkuki, Nao watateketezwa papo hapo kwa moto.
2 Samueli 23:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Haya ni maneno ya mwisho ya Daudi: “Neno la Daudi mwana wa Yese, neno la mtu aliyeinuliwa na Aliye Juu Sana, mtu aliyepakwa mafuta na Mungu wa Yakobo, mwimbaji wa nyimbo wa Israeli: “Roho wa BWANA alinena kupitia kwangu, neno lake lilikuwa ulimini mwangu. Mungu wa Israeli alinena, mwamba wa Israeli akaniambia: ‘Mtu anatawala watu kwa haki, wakati anapotawala akiwa na hofu ya Mungu, yeye ni kama mwanga wa asubuhi jua lichomozapo asubuhi isiyo na mawingu, kama mwanga baada ya mvua uchipuzao majani kutoka ardhini.’ “Je, si hivyo ilivyo nyumba yangu mbele za Mungu? Je, hajafanya Agano la milele nami, lililopangwa na kuimarishwa kila sehemu? Je, hatanifanya niufurahie wokovu wangu na kunijalia matakwa yangu yote? Lakini watu waovu wote watatupwa kando kama miiba, ambayo haikusanywi kwa mkono. Yeyote agusaye miiba hutumia chombo cha chuma au mpini wa mkuki, nayo huchomwa pale ilipo.”