2 Samueli 2:12-32
2 Samueli 2:12-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Abneri mwana wa Neri, pamoja na maofisa wa Ishboshethi, mwana wa Shauli, waliondoka Mahanaimu na kwenda Gibeoni. Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wengine wa Daudi, nao walitoka na kukutana na Abneri na watu aliokuwa nao kwenye bwawa lililoko huko Gibeoni. Kikosi kimoja upande mmoja wa bwawa na kingine upande mwingine. Abneri akamwambia Yoabu, “Waruhusu vijana wapambane mbele yetu!” Yoabu akamjibu, “Sawa.” Ndipo vijana ishirini na wanne wakatolewa: Upande wa kabila la Benyamini na Ishboshethi mwana wa Shauli, vijana kumi na wawili; na upande wa Daudi vijana kumi na wawili. Kila mmoja alimkamata adui yake kichwani, akamchoma mpinzani wake upanga, hivyo wote wawili wakaanguka chini, wamekufa. Hivyo, mahali hapo pakaitwa Helkath-hazurimu. Mahali hapo pako huko Gibeoni. Vita vya siku hiyo vilikuwa vikali. Abneri na watu wa Israeli walipigwa vibaya na watu wa Daudi. Wana watatu wa Seruya: Yoabu, Abishai na Asaheli walikuwapo hapo. Asaheli alikuwa na mbio kama paa. Asaheli alimfuatia Abneri moja kwa moja bila kugeuka kulia wala kushoto. Abneri alipoangalia nyuma na kumwona Asaheli, alimwambia, “Je, ni wewe Asaheli?” Yeye akamjibu, “Naam, ni mimi.” Abneri akamwambia, “Geukia kulia au kushoto, umkamate kijana mmoja na kuchukua nyara zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfuatia. Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, “Acha kunifuatia. Kwa nini nikuue? Nitawezaje kuonana na kaka yako Yoabu?” Lakini Asaheli alikataa. Hivyo Abneri akampiga mkuki tumboni kinyumenyume, na mkuki huo ukatokeza mgongoni kwa Asaheli. Asaheli akaanguka chini, na kufa papo hapo. Watu wote waliofika mahali alipofia Asaheli, walisimama kimya. Lakini Yoabu na Abishai walimfuatia Abneri. Jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye mlima wa Ama, ulioko mashariki ya Gia, katika barabara iendayo jangwa la Gibeoni. Watu wa kabila la Benyamini wakajikusanya pamoja wakawa nyuma ya Abneri, hivyo wakaunda kikosi chao; nao wakasimama juu ya mlima. Kisha Abneri akamwita Yoabu, “Je, tutapigana siku zote? Je, huoni kwamba mwisho utakuwa mchungu? Je, utaendelea kwa muda gani bila kuwashawishi watu wako waache kuwaandama ndugu zao?” Yoabu akamwambia, “Naapa kwa Mungu aliye hai, kwamba kama hungesema jambo hilo, hakika watu wangu wangeendelea kuwaandama ndugu zao hadi kesho asubuhi.” Hivyo, Yoabu akapiga tarumbeta na watu wakaacha kuwafuatia watu wa Israeli, wala hawakupigana zaidi. Abneri na watu wake walipita bonde la Araba usiku kucha. Wakavuka mto Yordani, wakatembea mchana kutwa hadi Mahanaimu. Yoabu aliporudi kutoka kumfuatia Abneri, aliwakusanya watu wake wote, akagundua kuwa watumishi kumi na tisa wa Daudi walikosekana, licha ya Asaheli. Lakini watumishi wa Daudi walikuwa wamewaua watu 360 kutoka kabila la Benyamini pamoja na watu wa Abneri. Yoabu na watu wake waliuchukua mwili wa Asaheli, wakauzika kwenye kaburi la baba yake, lililoko huko Bethlehemu. Yoabu na watu wake walitembea usiku kucha, na kulipokucha wakafika mjini Hebroni.
2 Samueli 2:12-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Abneri, mwana wa Neri, na watumishi wa Ishboshethi, mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni. Huyo Yoabu naye, mwana wa Seruya, na watumishi wa Daudi, wakatoka, wakakutana nao karibu na ziwa la Gibeoni; wakaketi, hawa upande huu wa ziwa, na hawa upande huu wa ziwa. Abneri akamwambia Yoabu, Tafadhali vijana hawa na waondoke na kucheza mbele yetu. Yoabu akasema, Haya! Na waondoke. Basi wakaondoka, wakaenda upande wa pili kwa hesabu yao watu kumi na wawili wa Benyamini, na wa Ishboshethi, mwana wa Sauli na watu kumi na wawili wa watumishi wa Daudi. Wakakamatana, kila mtu akimshika mwenziwe kichwa chake, na kutia upanga wake katika ubavu wa mwenzake; wakaanguka pamoja; hata mahali pale pakaitwa Helkath-hasurimu, napo ni katika Gibeoni. Vita vile vilikuwa vikali sana siku ile; naye Abneri akashindwa, na watu wa Israeli, mbele ya watumishi wa Daudi. Na wana watatu wa Seruya walikuwako huko, Yoabu, na Abishai, na Asaheli; na Asaheli alikuwa mwepesi wa miguu kama kulungu. Naye Asaheli akamfuatia Abneri; na katika kwenda kwake hakugeuka kwenda mkono wa kulia wala mkono wa kushoto katika kumfuatia Abneri. Basi Abneri akatazama nyuma yake, akasema, Ni wewe, Asaheli? Akajibu, Ni mimi. Basi Abneri akamwambia, Geuka mkono wa kulia au mkono wa kushoto, ukamshike mmoja wa vijana, ukazitwae silaha zake. Lakini Asaheli hakukubali kugeuka na kuacha kumfuata. Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, Geuka, acha kunifuatia mimi; kwa nini nikupige hadi chini? Hapo ningewezaje kuinua uso wangu mbele ya Yoabu, ndugu yako? Lakini akakataa kugeuka; kwa hiyo Abneri akampiga tumboni kwa ncha ya nyuma ya mkuki wake, ule mkuki ukamtoka kwa nyuma; naye akaanguka hapo, akafa papo hapo; ikawa, watu wote waliofika hapo, alipoanguka Asaheli na kufa, wakasimama. Ila Yoabu na Abishai wakamfuatia Abneri; na jua likachwa hapo walipoufikia mlima wa Ama, uelekeao Gia, katika njia ya nyika ya Gibeoni. Nao wana wa Benyamini wakakusanyika pamoja nyuma ya Abneri, wakawa kikosi kimoja, wakasimama juu ya mlima. Ndipo huyo Abneri akamwita Yoabu, akasema, Je! Upanga uwale watu sikuzote? Je! Hujui ya kwamba utakuwa uchungu mwisho wake? Basi itakuwa hata lini usijewaamuru watu warudi na kuacha kuwafuatia ndugu zao? Naye Yoabu akasema, Aishivyo Mungu, usingalinena, basi asubuhi wangalikwenda zao, wasiwafuatie kila mtu ndugu yake. Basi Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wote wakasimama, wasiwafuatie Israeli tena, wala hawakupigana tena. Wakaenda Abneri na watu wake usiku ule wote kati ya ile Araba; wakavuka Yordani, wakapita kati ya Bithroni yote, wakaja Mahanaimu. Akarudi Yoabu naye kutoka kumfuatia Abneri; na alipokwisha kuwakusanya watu wote pamoja, wa hao watumishi wa Daudi walipungukiwa na watu kumi na tisa pamoja na Asaheli. Ila watumishi wa Daudi walikuwa wamewapiga watu wa Benyamini, na watu wa Abneri, hata wakafa watu mia tatu na sitini. Nao wakamchukua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake, lililokuwako Bethlehemu. Yoabu na watu wake wakaenda usiku kucha, wakapambazukiwa huko Hebroni.
2 Samueli 2:12-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Abneri, mwana wa Neri, na watumishi wa Ishboshethi, mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni. Huyo Yoabu naye, mwana wa Seruya, na watumishi wa Daudi, wakatoka, wakakutana nao karibu na ziwa la Gibeoni; wakaketi, hawa upande huu wa ziwa, na hawa upande huu wa ziwa. Abneri akamwambia Yoabu, Tafadhali vijana hawa na waondoke na kucheza mbele yetu. Yoabu akasema, Haya! Na waondoke. Basi wakaondoka, wakaenda upande wa pili kwa hesabu yao watu kumi na wawili wa Benyamini, na wa Ishboshethi, mwana wa Sauli na watu kumi na wawili wa watumishi wa Daudi. Wakakamatana, kila mtu akimshika mwenziwe kichwa chake, na kutia upanga wake katika ubavu wa mwenzake; wakaanguka pamoja; hata mahali pale pakaitwa Helkath-hasurimu, napo ni katika Gibeoni. Vita vile vilikuwa vikali sana siku ile; naye Abneri akashindwa, na watu wa Israeli, mbele ya watumishi wa Daudi. Na wana watatu wa Seruya walikuwako huko, Yoabu, na Abishai, na Asaheli; na Asaheli alikuwa mwepesi wa miguu kama kulungu. Naye Asaheli akamfuatia Abneri; na katika kwenda kwake hakugeuka kwenda mkono wa kuume wala mkono wa kushoto katika kumfuatia Abneri. Basi Abneri akatazama nyuma yake, akasema, Ni wewe, Asaheli? Akajibu, Ni mimi. Basi Abneri akamwambia, Geuka mkono wa kuume au mkono wa kushoto, ukamshike mmoja wa vijana, ukazitwae silaha zake. Lakini Asaheli hakukubali kugeuka na kuacha kumfuata. Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, Geuka, acha kunifuatia mimi; kwa nini nikupige hata chini? Hapo ningewezaje kuinua uso wangu mbele ya Yoabu, ndugu yako? Lakini akakataa kugeuka; kwa hiyo Abneri akampiga tumboni kwa ncha ya nyuma ya mkuki wake, ule mkuki ukamtoka kwa nyuma; naye akaanguka hapo, akafa papo hapo; ikawa, watu wote waliofika hapo, alipoanguka Asaheli na kufa, wakasimama. Ila Yoabu na Abishai wakamfuatia Abneri; na jua likachwa hapo walipoufikilia mlima wa Ama, uelekeao Gia, katika njia ya nyika ya Gibeoni. Nao wana wa Benyamini wakakusanyika pamoja nyuma ya Abneri, wakawa kikosi kimoja, wakasimama juu ya mlima. Ndipo huyo Abneri akamwita Yoabu, akasema, Je! Upanga uwale watu sikuzote? Je! Hujui ya kwamba utakuwa uchungu mwisho wake? Basi itakuwa hata lini usijewaamuru watu warudi na kuacha kuwafuatia ndugu zao? Naye Yoabu akasema, Aishivyo Mungu, usingalinena, basi asubuhi wangalikwenda zao, wasiwafuatie kila mtu ndugu yake. Basi Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wote wakasimama, wasiwafuatie Israeli tena, wala hawakupigana tena. Wakaenda Abneri na watu wake usiku ule wote kati ya ile Araba; wakavuka Yordani, wakapita kati ya Bithroni yote, wakaja Mahanaimu. Akarudi Yoabu naye kutoka kumfuatia Abneri; na alipokwisha kuwakusanya watu wote pamoja, wa hao watumishi wa Daudi walipungukiwa na watu kumi na kenda pamoja na Asaheli. Ila watumishi wa Daudi walikuwa wamewapiga watu wa Benyamini, na watu wa Abneri, hata wakafa watu mia tatu na sitini. Nao wakamwinua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake, lililokuwako Bethlehemu. Yoabu na watu wake wakaenda usiku kucha, wakapambazukiwa huko Hebroni.
2 Samueli 2:12-32 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Abneri mwana wa Neri, pamoja na watumishi wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni. Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wa Daudi wakatoka na kukutana nao kwenye bwawa la Gibeoni. Kikundi kimoja kiliketi upande mmoja wa bwawa, na kikundi kingine upande wa pili. Ndipo Abneri akamwambia Yoabu, “Tuwaweke baadhi ya vijana wasimame, wapigane ana kwa ana mbele yetu.” Yoabu akasema, “Sawa, na wafanye hivyo.” Kwa hiyo vijana wakasimama, wakahesabiwa: watumishi wa Benyamini na wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli kumi na wawili, na upande wa Daudi kumi na wawili. Kisha kila mwanaume akamkamata mpinzani wake kichwani na kumchoma kwa upanga, nao wakaanguka chini pamoja. Kwa hiyo mahali pale katika Gibeoni pakaitwa Helkath-Hasurimu. Siku hiyo vita vilikuwa vikali sana, naye Abneri na Waisraeli wakashindwa na watumishi wa Daudi. Wana watatu wa Seruya walikuwa huko: Yoabu, Abishai na Asaheli. Basi huyo Asaheli alikuwa na mbio kama paa. Asaheli akamfukuza Abneri, pasipo kugeuka kulia wala kushoto wakati alimfuata. Abneri akaangalia nyuma na kumuuliza, “Ni wewe, Asaheli?” Akamjibu, “Ndiyo.” Ndipo Abneri akamwambia, “Geuka upande wa kulia au kushoto. Mchukue mmoja wa vijana, umvue silaha zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfukuza. Abneri akamwonya tena Asaheli akimwambia, “Acha kunifukuza! Kwa nini nikuue? Je, nitawezaje kumtazama ndugu yako Yoabu usoni?” Lakini Asaheli alikataa kuacha kumfuatia, kwa hiyo Abneri akamchoma Asaheli tumboni kwa ncha butu ya mkuki wake, mkuki ukamtoboa ukatokea mgongoni mwake. Akaanguka na kufa papo hapo. Ikawa kila mtu alisimama alipofika mahali pale Asaheli alipoanguka na kufa. Lakini Yoabu na Abishai walimfuata Abneri, na jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye kilima cha Ama, karibu na Gia kwenye njia ya kuelekea kwenye nyika ya Gibeoni. Ndipo Wabenyamini wakakusanyika tena nyuma ya Abneri. Wakaunda kikosi na kujiimarisha juu ya kilima. Abneri akamwita Yoabu, akamwambia, “Je, ni lazima upanga uendelee kuangamiza milele? Hutambui kwamba jambo hili litaishia katika uchungu? Utaacha kuwaagiza watu wako waache kuwafuatilia ndugu zao hata lini?” Yoabu akajibu, “Hakika kama aishivyo Mungu, kama hukusema, hawa watu wangeendelea kuwafuatia ndugu zao hadi asubuhi.” Basi Yoabu akapiga tarumbeta, nao watu wote wakasimama, hawakuwafuata Waisraeli tena, wala hawakuwapiga tena. Usiku ule wote Abneri na watu wake wakatembea kupitia Araba. Wakavuka Mto Yordani, wakaendelea wakipitia nchi yote ya Bithroni wakafika Mahanaimu. Basi Yoabu akarudi kutoka kumfuatia Abneri, na kuwakusanya watu wake wote. Pamoja na Asaheli, watumishi kumi na tisa wa Daudi walikuwa wamepotea. Lakini watumishi wa Daudi walikuwa wamewaua Wabenyamini mia tatu na sitini waliokuwa pamoja na Abneri. Wakamchukua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake huko Bethlehemu. Kisha Yoabu na vijana wake wakatembea usiku kucha na kufika huko Hebroni wakati wa mapambazuko.