2 Samueli 12:1-10
2 Samueli 12:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi Mwenyezi-Mungu akamtuma nabii Nathani kwa Daudi. Nathani alimwendea Daudi, akamwambia, “Kulikuwa na wanaume wawili katika mji mmoja; mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo wengi na ng'ombe wengi. Lakini yule maskini alikuwa na mwanakondoo mdogo mmoja jike, ambaye alikuwa amemnunua. Alimtunza, naye akakua nyumbani mwake pamoja na watoto wake. Alimlisha mwanakondoo huyo chakula kilekile kama chake na kunywea kikombe chake naye pia alikuwa akimpakata kifuani. Mwanakondoo huyo alikuwa kama binti kwa yule mtu maskini. Siku moja, yule tajiri alifikiwa na mgeni. Basi, tajiri huyo hakutaka kuchukua mmoja wa kondoo wake mwenyewe au ng'ombe wake, amchinjie mgeni wake, ila alikwenda na kumnyanganya yule maskini mwanakondoo wake, akamchinjia mgeni wake.” Daudi aliposikia hayo, akawaka hasira dhidi ya yule tajiri. Akamwambia nabii Nathani, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai kwamba mtu aliyefanya jambo hilo anastahili kufa! Ni lazima amlipe yule maskini mwanakondoo huyo, tena mara nne, kwani ametenda jambo baya na hakuwa na huruma!” Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Mimi nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli na kukuokoa mikononi mwa Shauli. Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake zake wawe wako, tena nikakupa watu wa Israeli na wa Yuda uwatawale. Na kama haya yangekuwa kidogo mno kwako ningekuongezea mara mbili zaidi ya hayo. Kwa nini basi, umedharau neno langu mimi Mwenyezi-Mungu ukafanya uovu huu mbele yangu? Umemuua Uria Mhiti, kwa upanga, ukamchukua mke wake kuwa mkeo. Umewatumia Waamoni kumwua Uria vitani! Kwa hiyo basi, kwa kuwa umenidharau na umemchukua mke wa Uria Mhiti, kuwa mkeo, mauaji hayataondoka katika jamaa yako’.
2 Samueli 12:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana-kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Kisha msafiri mmoja akamfikia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng'ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikia, bali alimnyang'anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo BWANA, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma. Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nilikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa kutoka kwa mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo mengine mengi. Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa Waamoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako.
2 Samueli 12:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng’ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang’anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo BWANA, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma. Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha. Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako.
2 Samueli 12:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA akamtuma Nathani kwa Daudi. Alipofika kwake akamwambia, “Katika mji mmoja kulikuwepo na watu wawili, mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini. Yule mtu tajiri alikuwa na idadi kubwa sana ya kondoo na ngʼombe, lakini yule maskini hakuwa na chochote ila kondoo jike mdogo aliyekuwa amemnunua. Akamtunza kondoo huyo, akakulia kwake pamoja na watoto wake. Kondoo huyo alishiriki chakula cha bwana wake na kunywea kikombe chake hata pia huyo kondoo alilala mikononi mwa bwana wake. Kwake alikuwa kama binti yake. “Siku moja yule tajiri akafikiwa na mgeni, lakini huyo tajiri akaacha kuchukua mmoja wa kondoo au ngʼombe wake mwenyewe amwandalie mgeni. Badala yake akachukua yule kondoo jike mdogo aliyekuwa mali ya yule maskini na kumwandalia yule mgeni wake.” Daudi akawakwa na hasira dhidi ya mtu huyo tajiri na kumwambia Nathani, “Hakika kama BWANA aishivyo, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa! Lazima alipe mara nne zaidi, kwa ajili ya kondoo huyo, kwa sababu amefanya jambo kama hilo na hakuwa na huruma.” Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli: ‘Nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, nilikuokoa kutokana na mkono wa Sauli. Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake za bwana wako mikononi mwako. Nikakupa nyumba ya Israeli na Yuda. Kama haya yote yalikuwa madogo sana, ningekupa hata zaidi. Kwa nini ulilidharau neno la BWANA kwa kufanya lililo ovu machoni pake? Ulimuua Uria, Mhiti kwa upanga na kumchukua mke wake awe mkeo. Ulimuua kwa upanga wa Waamoni. Basi kwa hiyo, upanga hautaondoka nyumbani mwako kamwe kwa sababu ulinidharau mimi na kumchukua mke wa Uria, Mhiti kuwa mkeo.’