Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 12:1-10

2 Samweli 12:1-10 SRUV

Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana-kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Kisha msafiri mmoja akamfikia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng'ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikia, bali alimnyang'anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo BWANA, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma. Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nilikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa kutoka kwa mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo mengine mengi. Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa Waamoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako.