2 Wafalme 24:8-20
2 Wafalme 24:8-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miezi mitatu. Mama yake alikuwa Nehushta binti Elnathani, mkazi wa Yerusalemu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama aliyoyafanya baba yake. Wakati huo jeshi la Nebukadneza mfalme wa Babuloni, lilishambulia mji wa Yerusalemu na kuuzingira. Wakati majeshi yalipokuwa yanauzingira mji, Nebukadneza mwenyewe alikuja Yerusalemu, na Yehoyakini mfalme wa Yuda alijisalimisha kwa mfalme wa Babuloni, yeye mwenyewe pamoja na mama yake, watumishi wake, maofisa na maakida wake. Mfalme wa Babuloni alimchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. Vilevile, pia kama Mwenyezi-Mungu alivyosema, Nebukadneza alichukua mali yote iliyokuwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na ndani ya ikulu. Alikatakata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Solomoni mfalme wa Israeli alitengeneza. Vyombo hivyo vilikuwa ndani ya hekalu la Mwenyezi-Mungu. Alichukua watu wote wa Yerusalemu: Wakuu wote, watu wote waliokuwa mashujaa, mateka 10,000, na mafundi wote na wahunzi. Hakuna aliyebaki isipokuwa waliokuwa maskini kabisa nchini. Alimchukua Yehoyakini mpaka Babuloni pamoja na mama yake mfalme, wake za mfalme, maofisa wake na wakuu wa nchi; wote hao aliwatoa Yerusalemu, akawapeleka Babuloni. Nebukadneza alichukua watu mashujaa wa Yuda jumla yao watu 7,000 pamoja na mafundi hodari na wahunzi 1,000; wote hawa wakiwa watu wenye nguvu na wa kuweza kupigana vitani. Nebukadneza akamtawaza Matania, mjomba wake Yehoyakini, kuwa mfalme badala yake, akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala; alitawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, mkazi wa mji wa Libna. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile alivyofanya mfalme Yehoyakimu. Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia sana watu wa Yerusalemu na Yuda, hata akawafukuza mbali naye. Sedekia alimwasi mfalme wa Babuloni.
2 Wafalme 24:8-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake. Wakati ule watumishi wa Nebukadneza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa. Na Nebukadneza, mfalme wa Babeli, akaufikia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru. Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maofisa wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. Akatoa huko hazina zote za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikatakata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivitengeneza katika hekalu la BWANA, kama BWANA alivyosema. Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge wa watu wa nchi. Akamchukua Yekonia mpaka Babeli; na mama yake mfalme, na wake zake mfalme, na maofisa wake, na wakuu wa nchi, aliwachukua mateka toka Yerusalemu mpaka Babeli. Na mashujaa wote, watu elfu saba, na mafundi na wafua chuma elfu moja, wote pia wenye nguvu, tayari kwa vita, hao wote mfalme wa Babeli aliwachukua mateka mpaka Babeli. Mfalme wa Babeli akamtawaza Matania, ndugu ya baba yake, awe mfalme badala yake, akalibadili jina lake, akamwita Sedekia. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali, binti Yeremia wa Libna. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Yehoyakimu. Maana kwa sababu ya hasira ya BWANA mambo hayo yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata alipokuwa amewaondosha wasiwe mbele ya uso wake; naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.
2 Wafalme 24:8-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake. Wakati ule watumishi wa Nebukadreza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa. Na Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaufikilia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru. Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maakida wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. Akatoa huko hazina zote za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikata-kata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivifanya katika hekalu la BWANA, kama BWANA alivyosema. Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge wa watu wa nchi. Akamchukua Yekonia mpaka Babeli; na mama yake mfalme, na wake zake mfalme, na maakida wake, na wakuu wa nchi, aliwachukua mateka toka Yerusalemu mpaka Babeli. Na mashujaa wote, watu elfu saba, na mafundi na wafua chuma elfu moja, wote pia wenye nguvu, tayari kwa vita, hao wote mfalme wa Babeli aliwachukua mateka mpaka Babeli. Mfalme wa Babeli akamtawaza Matania, ndugu ya baba yake, awe mfalme badala yake, akalibadili jina lake, akamwita Sedekia. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali, binti Yeremia wa Libna. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Yehoyakimu. Maana kwa sababu ya hasira ya BWANA mambo hayo yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata alipokuwa amewaondosha wasiwe mbele ya uso wake; naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.
2 Wafalme 24:8-20 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu. Mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani kutoka Yerusalemu. Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya. Wakati huo, maafisa wa Nebukadneza mfalme wa Babeli walikuja kushambulia Yerusalemu, nao wakauzingira kwa jeshi. Nebukadneza mwenyewe akaupandia mji wakati maafisa wake walipokuwa wameuzingira. Yehoyakini mfalme wa Yuda, mama yake, wahudumu wake, wakuu na maafisa wake wote wakajisalimisha kwa Nebukadneza. Katika mwaka wa nane wa utawala wa mfalme wa Babeli, akamchukua Yehoyakini kuwa mfungwa. Kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema, Nebukadneza akaondoa hazina yote kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu na kutoka jumba la mfalme, akavichukua vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani mfalme wa Israeli alikuwa amevitengeneza kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu. Akawachukua watu wa Yerusalemu wote kwenda uhamishoni: yaani maafisa wote na wapiganaji, watu wenye ustadi wa ufundi na wahunzi, jumla yao watu elfu kumi. Watu maskini sana tu ndio walibaki katika nchi. Nebukadneza akamchukua mateka Yehoyakini hadi Babeli. Pia akawachukua utumwani kutoka Yerusalemu hadi Babeli mama yake mfalme, wake zake, maafisa wake, na viongozi wote wa nchi. Mfalme wa Babeli pia akawahamishia Babeli wapiganaji elfu saba wenye nguvu na tayari kwa vita, na mafundi na wahunzi elfu moja. Akamfanya Matania, ndugu wa baba yake Yehoyakini, kuwa mfalme mahali pake, na akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na moja. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, kutoka Libna. Alifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kama alivyofanya Yehoyakimu. Haya yote yalitendeka Yerusalemu na Yuda kwa sababu ya hasira ya Mwenyezi Mungu, naye mwishoni akawaondoa mbele zake. Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli.