2 Wafalme 24:8-20
2 Wafalme 24:8-20 SRUV
Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake. Wakati ule watumishi wa Nebukadneza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa. Na Nebukadneza, mfalme wa Babeli, akaufikia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru. Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maofisa wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. Akatoa huko hazina zote za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikatakata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivitengeneza katika hekalu la BWANA, kama BWANA alivyosema. Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge wa watu wa nchi. Akamchukua Yekonia mpaka Babeli; na mama yake mfalme, na wake zake mfalme, na maofisa wake, na wakuu wa nchi, aliwachukua mateka toka Yerusalemu mpaka Babeli. Na mashujaa wote, watu elfu saba, na mafundi na wafua chuma elfu moja, wote pia wenye nguvu, tayari kwa vita, hao wote mfalme wa Babeli aliwachukua mateka mpaka Babeli. Mfalme wa Babeli akamtawaza Matania, ndugu ya baba yake, awe mfalme badala yake, akalibadili jina lake, akamwita Sedekia. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali, binti Yeremia wa Libna. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Yehoyakimu. Maana kwa sababu ya hasira ya BWANA mambo hayo yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata alipokuwa amewaondosha wasiwe mbele ya uso wake; naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.