Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 22:3-20

2 Wafalme 22:3-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, mfalme alimtuma katibu Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu akisema, “Nenda kwa kuhani mkuu Hilkia umwambie ahesabu zile fedha zilizoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambazo mabawabu walizikusanya kutoka kwa watu. Kiasi cha fedha hizo zipewe wasimamizi wa marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kulipa mishahara ya mafundi wanaofanya marekebisho, yaani maseremala, wajenzi na waashi. Kiasi kingine kitumike kununua mbao na mawe yaliyochongwa kwa ajili ya kurekebisha nyumba. Watu wanaosimamia ujenzi wasidaiwe kutoa hesabu ya matumizi ya fedha watakazokabidhiwa, kwa sababu wanazitumia kwa uaminifu.” Kisha kuhani mkuu Hilkia alimwambia katibu Shafani, “Nimekipata Kitabu cha Sheria katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Halafu Hilkia akampatia Shafani kitabu, naye akakisoma. Katibu Shafani, alimwendea mfalme na kutoa habari, akisema, “Watumishi wako wametoa fedha zilizopatikana katika nyumba halafu wamezikabidhi kwa mafundi wanaosimamia marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Kisha katibu Shafani, akamwambia mfalme, “Kuhani Hilkia amenipa kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme. Mfalme aliposikia maneno ya Kitabu cha Sheria, alirarua mavazi yake. Mara aliamuru kuhani Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani na Akbori mwana wa Mikaya pamoja na katibu Shafani na Asaya mtumishi wa mfalme, akisema, “Nendeni mkatafute shauri kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwa niaba yangu na watu wa Yuda wote kuhusu maneno ya kitabu hiki kilichopatikana kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imewaka juu yetu, maana babu zetu hawakutii maneno ya kitabu hiki, na kutimiza yote yaliyoandikwa kutuhusu.” Kwa hiyo kuhani Hilkia, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya, wote walikwenda kwa mama mmoja nabii jina lake Hulda aliyekuwa mke wa Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya hekalu. Wakati huo Hulda alikuwa anaishi katika mtaa wa pili wa Yerusalemu, nao wakazungumza naye. Basi akawaambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Mwambie huyo aliyewatuma kwangu, Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Nitaleta uovu juu ya mahali hapa na juu ya wakazi wake kama ilivyo katika kitabu kilichosomwa na mfalme wa Yuda. Kwa sababu wameniacha na kufukizia ubani miungu mingine na hivyo kunikasirisha kwa kazi zote za mikono yao, ghadhabu yangu dhidi ya Yerusalemu itawaka na haitaweza kutulizwa. Lakini kuhusu mfalme wa Yuda aliyewatuma kutafuta shauri la Mwenyezi-Mungu, mwambie kwamba, hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, juu ya maneno uliyoyasikia, Kwa kuwa umetubu na kunyenyekea mbele yangu, hata umerarua mavazi yako na kulia mbele yangu, hapo uliposikia niliyosema dhidi ya mahali hapa na dhidi ya wakazi wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nami pia nimekusikia. Kwa hiyo tazama, nitakukusanya pamoja na babu zako nawe utawekwa kaburini kwa amani, macho yako hayataona uovu nitakaouleta juu ya mahali hapa.’” Basi wajumbe wakamletea mfalme Yosia habari hizi.

2 Wafalme 22:3-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa, katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia, mfalme akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, mwandishi, nyumbani kwa Bwana, akisema, Nenda kwa Hilkia, kuhani mkuu, ili aihesabu fedha yote inayoletwa nyumbani mwa BWANA, ambayo mabawabu wameipokea kwa watu; tena waitie ile fedha katika mikono ya wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA; wakapewe wafanya kazi waliomo ndani ya nyumba ya BWANA, ili wapate kupatengeneza mahali palipobomoka ndani ya nyumba; wapewe maseremala, na wajenzi, na waashi; ili kununua miti na mawe yaliyochongwa wapate kuitengeneza nyumba. Lakini hawakuulizwa habari za ile fedha waliyokabidhiwa; maana walitenda kazi kwa uaminifu. Naye Hilkia, kuhani mkuu, akamwambia Shafani, mwandishi, Nimekiona kitabu cha Torati katika nyumba ya BWANA. Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma. Shafani mwandishi akamwendea mfalme, akamletea mfalme habari tena, akasema, Watumishi wako wamezitoa zile fedha zilizoonekana ndani ya nyumba, nao wamewakabidhi wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA. Kisha Shafani mwandishi akamwambia mfalme, akasema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akakisoma mbele ya mfalme. Ikawa, mfalme alipokwisha kuyasikia maneno ya kitabu hicho cha torati, alirarua nguo zake. Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Akbori, mwana wa Mikaya, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme akasema, Nendeni, mkamwulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, kuhusu maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya BWANA ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa. Basi Hilkia kuhani, na Ahikamu, na Akbori, na Shafani, na Asaya, wakamwendea Hulda, nabii wa kike, mkewe Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya mfalme; (naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili;) wakasema naye. Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu yule aliyewatuma ninyi kwangu, BWANA asema hivi, Tazama, mimi nitaleta uovu juu ya mahali hapa, na juu yao wakaao hapa, naam, maneno yote ya kitabu alichokisoma mfalme wa Yuda; kwa sababu wameniacha mimi, wameifukizia uvumba miungu mingine, ili wapate kunikasirisha kwa kazi yote ya mikono yao; kwa hiyo hasira yangu itawaka juu ya mahali hapa, isizimike. Lakini yule mfalme wa Yuda, aliyewatuma ninyi kumwuliza BWANA, mtamwambia hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa habari ya maneno yale uliyoyasikia, kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe ukajinyenyekeza mbele za BWANA, hapo ulipoyasikia maneno niliyoyanena juu ya mahali hapa, na juu ya wenyeji wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nawe ulizirarua nguo zako, ukalia mbele zangu; basi, mimi nami nimekusikia wewe, asema BWANA. Kwa hiyo tazama, nitakukusanya pamoja na baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani; wala macho yako hayatauona uovu huo wote nitakaouleta juu ya mahali hapa. Basi wakamletea mfalme habari tena.

2 Wafalme 22:3-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa, katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia, mfalme akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, mwandishi, nyumbani kwa Bwana, akisema, Enenda kwa Hilkia, kuhani mkuu, ili aihesabu fedha yote inayoletwa nyumbani mwa BWANA, ambayo mabawabu wameipokea kwa watu; tena waitie ile fedha katika mikono ya wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA; wakapewe wafanya kazi waliomo ndani ya nyumba ya BWANA, ili wapate kupatengeneza mahali palipobomoka ndani ya nyumba; wapewe maseremala, na wajenzi, na waashi; ili kununua miti na mawe yaliyochongwa wapate kuitengeneza nyumba. Lakini hawakuulizwa habari za ile fedha waliyokabidhiwa; maana walitenda kazi kwa uaminifu. Naye Hilkia, kuhani mkuu, akamwambia Shafani, mwandishi, Nimekiona kitabu cha torati katika nyumba ya BWANA. Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma. Shafani mwandishi akamwendea mfalme, akamletea mfalme habari tena, akasema, Watumishi wako wamezitoa zile fedha zilizoonekana ndani ya nyumba, nao wamewakabidhi wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA. Kisha Shafani mwandishi akamwambia mfalme, akasema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akakisoma mbele ya mfalme. Ikawa, mfalme alipokwisha kuyasikia maneno ya kitabu hicho cha torati, alirarua nguo zake. Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Akbori, mwana wa Mikaya, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme akasema, Enendeni, mkamwulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, katika habari za maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya BWANA ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa. Basi Hilkia kuhani, na Ahikamu, na Akbori, na Shafani, na Asaya, wakamwendea Hulda, nabii mke, mkewe Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya mfalme; (naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili;) wakasema naye. Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu yule aliyewatuma ninyi kwangu, BWANA asema hivi, Tazama, mimi nitaleta uovu juu ya mahali hapa, na juu yao wakaao hapa, naam, maneno yote ya kitabu alichokisoma mfalme wa Yuda; kwa sababu wameniacha mimi, wameifukizia uvumba miungu mingine, ili wapate kunikasirisha kwa kazi yote ya mikono yao; kwa hiyo hasira yangu itawaka juu ya mahali hapa, isizimike. Lakini yule mfalme wa Yuda, aliyewatuma ninyi kumwuliza BWANA, mtamwambia hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa habari ya maneno yale uliyoyasikia, kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe ukajinyenyekesha mbele za BWANA, hapo ulipoyasikia maneno niliyoyanena juu ya mahali hapa, na juu ya wenyeji wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nawe ulizirarua nguo zako, ukalia mbele zangu; basi, mimi nami nimekusikia wewe, asema BWANA. Kwa hiyo tazama, nitakukusanya pamoja na baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani; wala macho yako hayatauona uovu huo wote nitakaouleta juu ya mahali hapa. Basi wakamletea mfalme habari tena.

2 Wafalme 22:3-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, Mfalme Yosia akamtuma mwandishi Shafani mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, kwenda katika Hekalu la BWANA. Akasema: “Panda uende kwa Hilkia, kuhani mkuu, umwambie ahesabu zile fedha ambazo zimeletwa katika Hekalu la BWANA, ambazo mabawabu wamekusanya kutoka kwa watu. Waambie waikabidhi kwa watu walioteuliwa kusimamia kazi ya Hekalu. Waamuru watu hawa wawalipe wafanyakazi ambao wanakarabati Hekalu la BWANA: wale maseremala, wajenzi na waashi. Waambie pia wanunue mbao na mawe yaliyochongwa ili kukarabati Hekalu. Lakini hawahitajiki kutoa hesabu ya fedha walizokabidhiwa, kwa sababu wanafanya kwa uaminifu.” Hilkia kuhani mkuu akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Sheria ndani ya Hekalu la BWANA.” Akampa Shafani, ambaye alikisoma. Kisha Shafani mwandishi akamwendea mfalme na kumpa taarifa akisema: “Maafisa wako wametoa ile fedha ambayo ilikuwa ndani ya Hekalu la BWANA na imekabidhiwa mikononi mwa wasimamizi wa marekebisho ya Hekalu.” Ndipo Shafani mwandishi akampasha mfalme habari kwamba: “Hilkia kuhani amenipa kitabu hiki.” Naye Shafani akakisoma kile kitabu mbele ya mfalme. Mfalme aliposikia maneno ya kile Kitabu cha Sheria, akararua mavazi yake. Akatoa maagizo haya kwa Hilkia kuhani, Ahikamu mwana wa Shafani, Akbori mwana wa Mikaya, Shafani mwandishi, na Asaya mtumishi wa mfalme: “Nendeni mkamuulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu na Yuda wote kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya BWANA ni kubwa inayowaka dhidi yetu kwa sababu baba zetu hawakuyatii maneno ya kitabu hiki. Hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa humo kutuhusu sisi.” Hilkia kuhani, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya wakaenda kuongea na nabii mke Hulda, ambaye alikuwa mke wa Shalumu mwana wa Tikwa, mwana wa Harhasi mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu katika Mtaa wa Pili. Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, kulingana na kila kitu kilichoandikwa katika kitabu hicho mfalme wa Yuda alichosoma. Kwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine, na kunighadhibisha kwa sanamu zote zilizotengenezwa kwa mikono yao, hasira yangu itawaka dhidi ya mahali hapa, wala haitatulizwa.’ Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza BWANA, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia: Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za BWANA uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake, kwamba wangelaaniwa na kuachwa ukiwa, basi kwa sababu uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema BWANA. Kwa hiyo nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa.’ ” Basi wakapeleka jibu lake kwa mfalme.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha