Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 18:13-27

2 Wafalme 18:13-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Mnamo mwaka wa kumi na nne wa utawala wa mfalme Hezekia, mfalme Senakeribu wa Ashuru aliishambulia miji yote yenye ngome ya Yuda na kuiteka. Hezekia akatuma ujumbe kwa Senakeribu huko Lakishi na kumwambia, “Nimefanya makosa. Tafadhali, komesha mashambulio yako kwangu; nami nitalipa chochote utakacho.” Mfalme wa Ashuru akaagiza Hezekia amletee tani kumi za fedha na tani moja ya dhahabu. Hezekia akampelekea fedha yote iliyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina za nyumba ya mfalme; kadhalika, alingoa dhahabu kutoka katika milango ya hekalu la Mwenyezi-Mungu na ile dhahabu ambayo yeye mwenyewe aliiweka kwenye mihimili ya mlango; yote akampelekea Senakeribu. Kisha mfalme wa Ashuru alimtuma jemadari mkuu, amiri mkuu, mkuu wa matowashi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi kwenda kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Walisafiri na kufika Yerusalemu. Nao walipowasili waliingia na kusimama karibu na mfereji wa bwawa lililoko upande wa juu katika barabara kuu inayoelekea Uwanda wa Dobi. Walipomwita mfalme Hezekia walilakiwa na Eliakimu mwana wa Hilkia, ambaye alikuwa msimamizi wa ikulu; Shebna, aliyekuwa katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wa kumbukumbu za mfalme. Ndipo jemadari mkuu alipowaambia, “Mwambieni Hezekia, hivi ndivyo anavyosema mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni ujasiri wa namna gani huu unaouwekea matumaini? Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi? Angalia, sasa, unategemea Misri, utete uliovunjika ambao utamchoma mkono yeyote atakayeutegemea. Hivyo ndivyo Farao mfalme wa Misri alivyo kwa wote wale wanaomtegemea.” “Lakini hata kama mkiniambia: ‘Tunamtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu’, Jueni kwamba ni Mungu huyohuyo ambaye Hezekia alipaharibu mahali pake pa juu na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu waabudu tu mbele ya madhabahu iliyoko Yerusalemu. Basi, fanyeni mkataba na bwana wangu mfalme wa Ashuru, nami nitawapa farasi 2,000 kama mtaweza kupata wapandafarasi. Mwawezaje kumrudisha nyuma ofisa mmoja kati ya watumishi wa bwana wangu walio na cheo cha chini kabisa, wakati mnategemea Misri iwaletee magari na wapandafarasi?” Zaidi ya hayo, je, mnafikiri nimekuja bila amri ya Mwenyezi-Mungu ili kuishambulia na kuiangamiza nchi hii? Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeniambia, “Ishambulie nchi hii na kuiangamiza!” Basi, Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia huyo jemadari mkuu, “Tafadhali, sema nasi kwa lugha ya Kiaramu, maana tunaielewa; usiseme nasi kwa lugha ya Kiebrania; kwa kuwa watu walioko ukutani wanasikiliza.” Yule jemadari mkuu akawaambia, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu wanaokaa ukutani ambao wamehukumiwa pamoja nanyi kula mavi yao wenyewe na kunywa mikojo yao wenyewe?”

2 Wafalme 18:13-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa. Basi Hezekia, mfalme wa Yuda, akapeleka wajumbe waende Lakishi kwa mfalme wa Ashuru, kusema, Nimekosa; uniache ukarudi kwako; chochote utakachoweka juu yangu, nitakichukua. Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia, mfalme wa Yuda, talanta za fedha mia tatu, na talanta za dhahabu thelathini. Hezekia akampa fedha yote iliyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme. Wakati huo Hezekia aliiondoa dhahabu iliyokuwa juu ya milango ya hekalu la BWANA, na juu ya nguzo, ambazo Hezekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amezitia dhahabu, akampa mfalme wa Ashuru. Mfalme wa Ashuru akawatuma jemadari wake, na mkuu wa matowashi, na kamanda wake, toka Lakishi, kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu, pamoja na jeshi kubwa. Nao wakakwea wakafika Yerusalemu. Na walipokwisha kufika, wakaja wakasimama karibu na mfereji wa birika la juu, lililo katika njia kuu ya kuuendea Uwanda wa Dobi. Na walipokwisha kumwita mfalme, wakatokewa na Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe. Yule amiri akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kusema, Mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia? Wewe wasema, lakini ni maneno yasiyo na maana, kwamba, Lipo shauri na zipo nguvu kwa vita hivi. Basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi? Sasa tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliopondeka, yaani, Misri, ambayo mtu akiitegemea, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio. Lakini mkiniambia, Tunamtumaini BWANA, Mungu wetu; je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii hapa Yerusalemu? Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao. Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa ofisa mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi? Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la BWANA? BWANA ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule kamanda, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa hao watu walio ukutani. Lakini yule kamanda akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma kwa bwana wako, na kwako wewe, niseme maneno haya? Je! Hakunituma kwa watu hawa walio ukutani, ili wale mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi?

2 Wafalme 18:13-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa. Basi Hezekia, mfalme wa Yuda, akapeleka wajumbe waende Lakishi kwa mfalme wa Ashuru, kusema, Nimekosa; uniache ukarudi kwako; cho chote utakachoweka juu yangu, nitakichukua. Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia, mfalme wa Yuda, talanta za fedha mia tatu, na talanta za dhahabu thelathini. Hezekia akampa fedha yote iliyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme. Wakati huo Hezekia aliiondoa dhahabu iliyokuwa juu ya milango ya hekalu la BWANA, na juu ya nguzo, ambazo Hezekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amezitia dhahabu, akampa mfalme wa Ashuru. Mfalme wa Ashuru akawatuma jemadari wake, na mkuu wa matowashi, na amiri wake, toka Lakishi, kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu, pamoja na jeshi kubwa. Nao wakakwea wakafika Yerusalemu. Na walipokwisha kufika, wakaja wakasimama karibu na mfereji wa birika la juu, lililo katika njia kuu ya kuuendea uwanda wa dobi. Na walipokwisha kumwita mfalme, wakatokewa na Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe. Yule amiri akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kusema, Mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia? Wewe wasema, lakini ni maneno yasiyo na maana, kwamba, Lipo shauri na zipo nguvu kwa vita hivi. Basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi? Sasa tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliopondeka, yaani, Misri, ambayo mtu akiitegemea, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio. Lakini mkiniambia, Tunamtumaini BWANA, Mungu wetu; je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii hapa Yerusalemu? Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao. Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa akida mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi? Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la BWANA? BWANA ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule amiri, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa hao watu walio ukutani. Lakini yule amiri akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma kwa bwana wako, na kwako wewe, niseme maneno haya? Je! Hakunituma kwa watu hawa walio ukutani, ili wale mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi?

2 Wafalme 18:13-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka. Basi Hezekia mfalme wa Yuda akamtumia ujumbe mfalme wa Ashuru huko Lakishi akisema: “Nimefanya makosa. Ondoka katika nchi yangu, nami nitakulipa chochote unachokitaka kwangu.” Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia mfalme wa Yuda talanta mia tatu za fedha, na talanta thelathini za dhahabu. Basi Hezekia akampa fedha yote iliyopatikana ndani ya Hekalu la BWANA na katika hazina ya jumba la mfalme. Wakati huu Hezekia mfalme wa Yuda akabandua dhahabu yote iliyokuwa imefunika milango na miimo ya Hekalu la BWANA, akampa mfalme wa Ashuru. Mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wake mkuu, na afisa wake mkuu, na jemadari wa jeshi, pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Wakaja Yerusalemu na kusimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi. Wakaagiza mfalme aitwe. Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la mfalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakawaendea. Yule jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia: “ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako? Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi? Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea. Nawe ukiniambia, “Tunamtumainia BWANA Mungu wetu”: je, siyo yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya katika Yerusalemu”? “ ‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao! Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi? Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza mahali hapa pasipo neno kutoka kwa BWANA? BWANA mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ” Ndipo Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania, watu walio juu ya ukuta wakiwa wanasikia.” Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioketi ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mkojo wao wenyewe?”