2 Mambo ya Nyakati 34:1-7
2 Mambo ya Nyakati 34:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; alitawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu. Alifuata njia zake Daudi babu yake, na kushika amri za Mwenyezi-Mungu kwa dhati. Katika mwaka wa nne wa utawala wake, mfalme Yosia, akiwa bado kijana, alianza kumwabudu Mungu wa Daudi, baba yake. Baadaye alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili alianza kuisafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuharibu mahali pa kuabudia miungu mingine, sanamu za Ashera, na sanamu nyinginezo za kuchonga na za kusubu. Watu wake walizibomoa madhabahu za ibada za Mabaali mbele yake na alizikatakata madhabahu za kufukizia ubani zilizoinuliwa juu ya madhabahu hizo; pia alizipondaponda sanamu za Ashera na nyinginezo za kuchonga na za kusubu; alizifanya kuwa mavumbi, nayo mavumbi akayamwaga juu ya makaburi ya wale ambao hapo awali walizitolea sadaka. Aidha, aliiteketeza mifupa ya makuhani wa miungu hiyo kwenye madhabahu zao, hivyo akatakasa Yuda na Yerusalemu. Alifanya vivyo hivyo katika miji ya Manase, Efraimu, Simeoni mpaka Naftali na kwenye magofu yaliyokuwa kandokando ya miji hiyo. Alizibomoa madhabahu na kupondaponda Maashera na sanamu za kuchongwa zikawa mavumbi. Kadhalika alizikatakata madhabahu za kufukizia ubani katika nchi yote ya Israeli. Hatimaye alirudi Yerusalemu.
2 Mambo ya Nyakati 34:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaziendea njia za Daudi babaye, asigeuke kwa kulia wala kwa kushoto. Kwa kuwa katika mwaka wa nane wa kutawala kwake, naye akiwa bado mchanga, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi babaye; hata katika mwaka wa kumi na mbili akaanza kusafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuondoa mahali pa juu, na kwa kuondoa Maashera, na sanamu za kuchonga, na za kusubu. Wakazibomoa madhabahu za mabaali machoni pake; na sanamu za jua, zilizoinuliwa juu yake, akazikatakata; Maashera, sanamu za kuchonga, na za kusubu, akazivunjavunja, akaziponda kuwa mavumbi, akayamimina juu ya makaburi ya hao waliozichinjia dhabihu. Akaiteketeza mifupa ya makuhani madhabahuni mwao, akasafisha Yuda na Yerusalemu. Na katika miji ya Manase, Efraimu, na Simeoni, mpaka Naftali, akafanya vile vile; na katika maganjo yake pande zote. Akazibomoa madhabahu, akazipondaponda Maashera na sanamu kuwa mavumbi, akazikatakata sanamu zote za jua katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu.
2 Mambo ya Nyakati 34:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaziendea njia za Daudi babaye, asigeuke kwa kuume wala kwa kushoto. Kwa kuwa katika mwaka wa nane wa kutawala kwake, naye akali mchanga, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi babaye; hata katika mwaka wa kumi na mbili akaanza kusafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuondoa mahali pa juu, na kwa kuondoa maashera, na sanamu za kuchora, nazo za kusubu. Wakazibomoa madhabahu za mabaali machoni pake; na sanamu za jua, zilizoinuliwa juu yake, akazikata-kata; na maashera, na sanamu za kuchonga, nazo za kusubu, akazivunja-vunja, akaziponda kuwa mavumbi, akayamimina juu ya makaburi ya hao waliozichinjia dhabihu. Akaiteketeza mifupa ya makuhani madhabahuni mwao, akasafisha Yuda na Yerusalemu. Na katika miji ya Manase, na Efraimu, na Simeoni, mpaka Naftali, akafanya vile vile; na katika maganjo yake pande zote. Akazibomoa madhabahu, akaponda-ponda maashera na sanamu kuwa mavumbi, akazikata-kata sanamu zote za jua katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu.
2 Mambo ya Nyakati 34:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yosia alikuwa na miaka minane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka thelathini na mmoja. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA na kuenenda katika njia za Daudi baba yake, hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto. Katika mwaka wa nane wa utawala wake, alipokuwa angali bado mdogo, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi baba yake. Katika mwaka wake wa kumi na mbili alianza kusafisha mahali pa juu pa kuabudia miungu pa Yuda na Yerusalemu, akiondoa nguzo za Ashera, sanamu za kuchonga na vinyago vya kusubu. Mbele ya macho yake, wakazibomoa madhabahu za Mabaali, wakazivunja madhabahu za kufukizia uvumba zilizokuwa zimesimama juu yake, wakazivunja nguzo za Ashera, sanamu na vinyago. Hivi alivivunja vipande vipande na kuvisambaza juu ya makaburi ya waliokuwa wamevitolea kafara. Akachoma mifupa ya makuhani wao juu ya madhabahu zao na kwa njia hiyo akaitakasa Yuda na Yerusalemu. Katika miji ya Manase, Efraimu na Simeoni, hadi Naftali na kwenye magofu yanayoizunguka, akavunja madhabahu na nguzo za Ashera na kuzipondaponda hizo sanamu hadi zikawa unga na kukata vipande vipande madhabahu zote za kufukizia uvumba katika Israeli yote. Kisha akarudi Yerusalemu.