2 Mambo ya Nyakati 34:1-7
2 Mambo ya Nyakati 34:1-7 SRUV
Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaziendea njia za Daudi babaye, asigeuke kwa kulia wala kwa kushoto. Kwa kuwa katika mwaka wa nane wa kutawala kwake, naye akiwa bado mchanga, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi babaye; hata katika mwaka wa kumi na mbili akaanza kusafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuondoa mahali pa juu, na kwa kuondoa Maashera, na sanamu za kuchonga, na za kusubu. Wakazibomoa madhabahu za mabaali machoni pake; na sanamu za jua, zilizoinuliwa juu yake, akazikatakata; Maashera, sanamu za kuchonga, na za kusubu, akazivunjavunja, akaziponda kuwa mavumbi, akayamimina juu ya makaburi ya hao waliozichinjia dhabihu. Akaiteketeza mifupa ya makuhani madhabahuni mwao, akasafisha Yuda na Yerusalemu. Na katika miji ya Manase, Efraimu, na Simeoni, mpaka Naftali, akafanya vile vile; na katika maganjo yake pande zote. Akazibomoa madhabahu, akazipondaponda Maashera na sanamu kuwa mavumbi, akazikatakata sanamu zote za jua katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu.