Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 19:4-11

2 Mambo ya Nyakati 19:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Yehoshafati alikaa Yerusalemu, lakini hata hivyo, mara kwa mara aliwatembelea watu wa Beer-sheba kusini, mpaka milima ya Efraimu, upande wa kaskazini. Alifanya hivyo ili kuwavutia watu wamrudie Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. Aliteua waamuzi katika miji yote ya Yuda yenye ngome, akawaambia, “Muwe waangalifu sana wakati mnapoamua, kwa maana hukumu mtoayo hamwitoi kwa amri ya binadamu, bali kwa amri itokayo kwa Mwenyezi-Mungu, naye yu pamoja nanyi mnapotoa uamuzi. Basi, sasa mwogopeni Mwenyezi-Mungu, muwe waangalifu katika kila jambo mtakalotenda kwa sababu Mwenyezi-Mungu wetu hatavumilia upotoshaji wa haki, wala upendeleo wala ulaji rushwa.” Mjini Yerusalemu, Yehoshafati aliteua Walawi kadhaa, waamuzi na baadhi ya wakuu wa jamaa za Waisraeli wawe waamuzi wa magomvi yahusuyo uvunjaji wa sheria za Mwenyezi-Mungu, au ugomvi baina ya wakazi wa mji. Akawaamuru akisema; “Tekelezeni wajibu wenu mkimwogopa Mwenyezi-Mungu, kwa uaminifu na kwa moyo wote. Kila mara ndugu zenu kutoka katika mji wowote ule wanapowaletea shtaka lolote kuhusu uuaji, uvunjaji wa sheria, amri, kanuni au maagizo, washaurini vema ili wasije wakamkosea Mwenyezi-Mungu. Msipofanya hivyo, nyinyi pamoja na ndugu zenu mtapatwa na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Lakini mkiutekeleza wajibu wenu, hamtakuwa na hatia. Amaria, kuhani mkuu, ndiye atakayesimamia mambo yote yanayomhusu Mwenyezi-Mungu, naye Zebadia mwana wa Ishmaeli, gavana wa Yuda atasimamia mambo yote ya utawala, na Walawi watakuwa maofisa. Jipeni moyo muyatekeleze masharti haya, naye Mwenyezi-Mungu awe pamoja nao walio wema.”

2 Mambo ya Nyakati 19:4-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Yehoshafati aliishi huko Yerusalemu, naye akatoka akaenda tena miongoni mwa watu, kuanzia Beer-Sheba hadi nchi ya vilima ya Efraimu na kuwageuza wakamrudia BWANA, Mungu wa baba zao. Akawaweka waamuzi katika nchi, kwenye miji yote ya Yuda yenye maboma. Akawaambia, “Angalieni kwa makini yale mtendayo, kwa kuwa hamkuhukumu kwa ajili ya mwanadamu bali kwa ajili ya BWANA ambaye yu pamoja nanyi kila mtoapo hukumu. Basi sasa hofu ya BWANA na iwe juu yenu. Hukumuni kwa uangalifu, kwa kuwa kwa BWANA Mungu wetu hakuna jambo lisilo la haki, upendeleo, wala rushwa.” Pia huko Yerusalemu, Yehoshafati akaweka baadhi ya Walawi, makuhani na viongozi wa jamaa za Waisraeli ili kutoa hukumu kwa ajili ya BWANA na kuamua magomvi. Nao waliishi huko Yerusalemu. Akawapa maagizo haya: “Ni lazima mtumike kwa uaminifu na kwa moyo wote katika kicho cha BWANA. Katika kila shauri lifikalo mbele yenu kutoka kwa ndugu zenu wale waishio katika miji, ikiwa ni la umwagaji wa damu au mambo mengine yahusuyo sheria, amri, hukumu au maagizo, inawapasa ninyi kuwaonya kwamba wasiingie katika hatia dhidi ya BWANA, la sivyo ghadhabu yake itakuja juu yenu na ndugu zenu. Tendeni hivyo, nanyi hamtatenda dhambi. “Amaria kuhani mkuu atakuwa juu yenu katika jambo lolote linalomhusu BWANA naye Zebadia mwana wa Ishmaeli, kiongozi wa kabila la Yuda, atakuwa juu yenu kwa jambo lolote linalomhusu mfalme, nao Walawi watatumika kama maafisa mbele yenu. Tendeni kwa ujasiri, naye BWANA atakuwa pamoja na wale watendao vyema.”