2 Mambo ya Nyakati 15:1-7
2 Mambo ya Nyakati 15:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo roho ya Mungu ikamjia Azaria mwana wa Odedi; naye akatoka ili amlaki Asa, akamwambia, Nisikieni, Ee Asa, na Yuda wote na Benyamini; BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi. Basi tangu siku nyingi Israeli wamekuwa hawana Mungu wa kweli, wala hawana kuhani afundishaye, wala hawana torati; lakini walipomgeukia BWANA, Mungu wa Israeli, katika msiba wao, na kumtafuta, akaonekana kwao. Hata na zamani zile hakukuwa na amani kwake atokaye, wala kwake aingiaye, ila fadhaa kubwa juu yao wote wakaao katika nchi. Wakavunjika-vunjika, taifa juu ya taifa, na mji juu ya mji; kwani Mungu aliwafadhaisha kwa shida zote. Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na ijara.
2 Mambo ya Nyakati 15:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Roho wa BWANA akamjia Azaria mwana wa Odedi. Akatoka ili kumlaki Asa na kumwambia, “Nisikilizeni, Asa na Yuda wote na Benyamini. BWANA yu pamoja nanyi mkiwa pamoja naye. Kama mkimtafuta, ataonekana kwenu, lakini kama mkimwacha yeye, naye atawaacha ninyi. Kwa muda mrefu Israeli walikuwa hawana Mungu wa kweli, walikuwa hawana kuhani wa kuwafundisha na wala hawakuwa na sheria. Lakini katika taabu yao walimrudia BWANA, Mungu wa Israeli na kumtafuta, naye akaonekana kwao. Katika siku hizo hapakuwa na amani kwa yeyote aliyesafiri, kutoka wala kuingia, kwa kuwa wakazi wote wa nchi walikuwa katika machafuko makubwa. Taifa moja lilipigana na taifa lingine na mji mmoja ukapigana na mji mwingine, kwa sababu Mungu alikuwa anawahangaisha kwa taabu za kila aina. Lakini kwa habari yenu ninyi, kuweni hodari wala msikate tamaa, kwa kuwa mtapata thawabu kwa kazi yenu.”
2 Mambo ya Nyakati 15:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Roho ya Mungu ilimjia Azaria mwana wa Odedi, naye akatoka kwenda kumlaki mfalme Asa, akamwambia, “Nisikilize, ee mfalme Asa na watu wote wa Yuda na Benyamini! Mwenyezi-Mungu yu pamoja nanyi, ikiwa mtakuwa pamoja naye. Mkimtafuta, mtampata, lakini mkimwacha naye atawaacha. Kwa muda mrefu sasa, Waisraeli wameishi bila Mungu wa kweli, wala makuhani wa kuwafundisha, na bila sheria. Lakini walipopatwa na shida, walimgeukia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, wakamtafuta, wakampata. Zamani hizo, hakuna mtu aliyeweza kuingia wala kutoka kwa usalama kwa sababu hapakuwa na amani; ghasia nyingi mno ziliwasumbua wananchi wa kila nchi. Kulijaa mafarakano mengi, taifa moja lilipigana na taifa lingine na mji mmoja ulipigana na mji mwingine, kwa sababu Mungu aliwafadhaisha kwa taabu za kila aina. Lakini nyinyi jipeni moyo, wala msilegee kwa maana mtapata tuzo kwa kazi mfanyayo.”
2 Mambo ya Nyakati 15:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Roho ya Mungu ikamjia Azaria mwana wa Odedi; naye akatoka ili amlaki Asa, akamwambia, Nisikieni, Ee Asa, na Yuda wote na Benyamini; BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi. Basi kwa siku nyingi Israeli wamekuwa hawana Mungu wa kweli, wala hawana kuhani afundishaye, wala hawana torati; lakini walipomgeukia BWANA, Mungu wa Israeli, katika msiba wao, na kumtafuta, akaonekana kwao. Hata na zamani zile hakukuwa na amani kwake atokaye, wala kwake aingiaye, ila fadhaa kubwa juu yao wote wakaao katika nchi. Walivunjikavunjika, taifa juu ya taifa, na mji juu ya mji; kwa sababu Mungu aliwafadhaisha kwa shida zote. Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na thawabu.