2 Mambo ya Nyakati 1:6-12
2 Mambo ya Nyakati 1:6-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za BWANA, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu yake. Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake. Basi sasa, Ee BWANA Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi. Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi? Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha za wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao; basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.
2 Mambo ya Nyakati 1:6-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Solomoni akapanda huko yalikokuwa madhabahu ya shaba mbele za BWANA katika Hema la Kukutania, na kutoa dhabihu 1,000 za sadaka za kuteketezwa juu yake. Usiku ule Mungu akamtokea Solomoni na kumwambia, “Omba lolote utakalo nikupe.” Solomoni akamjibu Mungu, “Umemwonyesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, nawe umeniweka niwe mfalme mahali pake. Sasa, BWANA Mungu, ahadi yako kwa baba yangu Daudi na ithibitike, kwa kuwa umenifanya mimi mfalme juu ya watu ambao ni wengi kama mavumbi ya nchi. Nakuomba unipe mimi hekima na maarifa, ili niweze kuongoza watu hawa, kwa kuwa ni nani awezaye kutawala hawa watu wako walio wengi hivi?” Mungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili ndilo shauku ya moyo wako na hukuomba mali, utajiri au heshima, wala kifo kwa ajili ya adui zako, nawe kwa kuwa hukuomba maisha marefu, bali umeomba hekima na maarifa ili kuongoza watu wangu ambao nimekufanya uwe mfalme juu yao, kwa hiyo utapewa hekima na maarifa. Tena nitakupa pia mali, utajiri na heshima, ambavyo hakuna mfalme yeyote aliyekuwepo kabla yako amewahi kuwa navyo, na hakuna yeyote baada yako atakayekuwa navyo.”
2 Mambo ya Nyakati 1:6-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Solomoni alipanda mbele ya madhabahu ya shaba iliyokuwa kwenye hema la mkutano. Hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akatoa tambiko 1,000 za kuteketezwa juu ya madhabahu hayo. Usiku huo, Mungu alimtokea Solomoni, akamwambia, “Omba chochote, nami nitakupa.” Solomoni akamwambia Mungu, “Ulimwonesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, na umenijalia kuwa mfalme mahali pake. Sasa, ee Mungu, Mwenyezi-Mungu, itimize ahadi uliyompa baba yangu Daudi. Umenitawaza niwe mfalme juu ya watu hawa walio wengi kama mavumbi. Kwa hiyo, nakuomba unipe hekima na maarifa ili niweze kuwatawala watu wako vizuri. La sivyo, nitawezaje kuwatawala hawa watu wako walio wengi hivi?” Mungu akamjibu Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili uliloomba limo moyoni mwako, na wala hukuomba mali, wala utajiri, wala heshima wala hukuomba wanaokuchukia waangamizwe, wala maisha marefu, lakini umeomba hekima na maarifa ili uwatawale vizuri watu wangu ambao nimekupa uwe mfalme wao, ninakupa hekima na maarifa. Pia, nitakupa utajiri, mali na heshima zaidi ya mfalme mwingine yeyote aliyekuwako kabla yako na mfalme mwingine yeyote atakayetawala baada yako.”
2 Mambo ya Nyakati 1:6-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za BWANA, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu yake. Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake. Basi sasa, Ee BWANA Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi. Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwatawala watu wako hawa walio wengi? Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha ya wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwatawala watu wangu, niliokutawaza juu yao; basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.