2 Mambo ya Nyakati 1:1-6
2 Mambo ya Nyakati 1:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Sulemani, mwana wa Daudi, alithibitishwa katika ufalme wake, naye BWANA, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, akamtukuza mno. Sulemani akasema na Israeli wote, na maakida wa maelfu, na wa mamia, na waamuzi, na kila shehe wa Israeli wote, wakuu wa nyumba za mababa. Basi Sulemani akaenda mahali pa juu pa Gibeoni, na kusanyiko lote naye; kwani ndipo ilipokuwako hema ya kukutania ya Mungu, aliyoifanya Musa mtumishi wa BWANA jangwani. Lakini sanduku la Mungu, Daudi alikuwa amelipandisha kutoka Kiriath-yearimu mpaka mahali Daudi alipolitengenezea; maana amelitandia hema katika Yerusalemu. Tena madhabahu ya shaba, aliyoifanyiza Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwako huko mbele ya maskani ya BWANA; Sulemani na kusanyiko wakaiendea. Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za BWANA, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu yake.
2 Mambo ya Nyakati 1:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Solomoni, mwanawe mfalme Daudi, alijiimarisha katika utawala wake, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wake alikuwa pamoja naye, akambariki na kumfanya awe mkuu sana. Mfalme Solomoni aliwaita makamanda wote wa vikosi vya maelfu na vya mamia, waamuzi, na viongozi wote wa koo za Israeli. Kisha akaandamana nao hadi mahali pa ibada huko Gibeoni. Walikwenda huko kwa sababu hapo ndipo mahali lilipokuwa hema la mkutano la Mungu alilolitengeneza Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, nyikani. (Lakini, sanduku la Mungu lilikuwa Yerusalemu katika hema ambalo mfalme Daudi alilipigilia alipolileta kutoka Kiriath-yearimu). Tena, madhabahu ya shaba iliyotengenezwa na Bezaleli, mwana wa Uri na mjukuu wa Huri, pia ilikuwa huko Gibeoni mbele ya hema takatifu la Mwenyezi-Mungu. Hapo mfalme Solomoni na watu wote wakamwomba Mwenyezi-Mungu. Solomoni alipanda mbele ya madhabahu ya shaba iliyokuwa kwenye hema la mkutano. Hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akatoa tambiko 1,000 za kuteketezwa juu ya madhabahu hayo.
2 Mambo ya Nyakati 1:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Sulemani, mwana wa Daudi, alijiimarisha katika ufalme wake, naye BWANA, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, akamtukuza mno. Sulemani akawaita Israeli wote, na makamanda wa maelfu, na wa mamia, na waamuzi, na kila kiongozi wa Israeli, na wakuu wa familia. Basi Sulemani akaenda mahali pa juu pa Gibeoni, na kusanyiko lote naye; kwani ndipo lilipokuwako hema la kukutania la Mungu, alilolifanya Musa mtumishi wa BWANA jangwani. Lakini sanduku la Mungu, Daudi alikuwa amelipandisha kutoka Kiriath-yearimu mpaka mahali Daudi alipolitengenezea; maana amelitandia hema katika Yerusalemu. Tena madhabahu ya shaba, aliyoifanya Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwako huko mbele ya maskani ya BWANA; Sulemani na kusanyiko wakaiendea. Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za BWANA, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu yake.
2 Mambo ya Nyakati 1:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Solomoni mwana wa Daudi alijiimarisha kwenye milango yote! Katika ufalme wake, kwa kuwa BWANA Mungu wake alikuwa pamoja naye, naye akamfanya mkuu mno. Ndipo Solomoni akasema na Israeli wote, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, waamuzi na viongozi wote katika Israeli, pamoja na wakuu wa jamaa. Naye Solomoni na kusanyiko lote wakakwea mpaka mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni, kwa kuwa huko ndiko Hema la Kukutania la Mungu lilipokuwa, ambalo Mose mtumishi wa BWANA alikuwa amelitengeneza huko jangwani. Basi Daudi alikuwa amelipandisha Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu mpaka mahali alipokuwa amepatengeneza kwa ajili yake, kwa sababu alikuwa amesimamisha hema kwa ajili ya hilo Sanduku huko Yerusalemu. Lakini yale madhabahu ya shaba ambayo Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, alikuwa ametengeneza yalikuwa huko Gibeoni mbele ya Maskani ya BWANA Mungu, hivyo Solomoni na kusanyiko lote walimtafuta Mungu huko. Solomoni akapanda huko yalikokuwa madhabahu ya shaba mbele za BWANA katika Hema la Kukutania, na kutoa dhabihu 1,000 za sadaka za kuteketezwa juu yake.