1 Samueli 4:10-18
1 Samueli 4:10-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu elfu thelathini walioenda vitani kwa miguu. Hilo sanduku la Mungu likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa. Basi, mtu mmoja wa Benyamini akapiga mbio kutoka mle vitani akafika Shilo siku ile ile, hali nguo zake zimeraruliwa, na mavumbi kichwani mwake. Alipofika, tazama, Eli alikuwa ameketi kitini pake kando ya njia, akingojea; maana moyo wake ulitetemeka kwa ajili ya sanduku la Mungu. Na yule mtu alipoingia mjini, akatoa habari, mji wote ukalia. Naye Eli aliposikia kelele za kile kilio, akasema, Maana yake nini kelele za kishindo hiki? Yule mtu akafanya haraka, akaenda, akamwambia Eli. Basi Eli umri wake umepata miaka tisini na minane; na macho yake yamepofuka hata asiweze kuona. Yule mtu akamwambia Eli, Mimi ndimi niliyetoka jeshini, nami leo hivi nimekimbia toka jeshini. Naye akasema, Yalikwendaje, mwanangu? Yeye aliyeleta habari akajibu, akasema, Israeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, tena watu wengi sana wameuawa, hata na wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa pia, na sanduku la Mungu limetwaliwa. Ikawa alipolitaja sanduku la Mungu, Eli akaanguka kitini pake kwa nyuma, kando ya mlango, shingo yake ikavunjika, akafa; maana alikuwa mzee, tena mzito. Naye alikuwa amewaamua Waisraeli miaka arubaini.
1 Samueli 4:10-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu. Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa. Basi, mtu mmoja wa Benyamini akapiga mbio kutoka mle jeshini akafika Shilo siku ile ile, hali nguo zake zimeraruliwa, na mavumbi kichwani mwake. Alipofika, tazama, Eli alikuwa ameketi kitini pake kando ya njia, akingojea; maana moyo wake ulitetemeka kwa ajili ya sanduku la Mungu. Na yule mtu alipoingia mjini, akatoa habari, mji wote ukalia. Naye Eli aliposikia kelele za kile kilio, akasema, Maana yake nini kelele za kishindo hiki? Yule mtu akafanya haraka, akaenda, akamwambia Eli. Basi Eli umri wake umepata miaka tisini na minane; na macho yake yamepofuka hata asiweze kuona. Yule mtu akamwambia Eli, Mimi ndimi niliyetoka jeshini, nami leo hivi nimekimbia toka jeshini. Naye akasema, Yalikwendaje, mwanangu? Yeye aliyeleta habari akajibu, akasema, Israeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, tena watu wengi sana wameuawa, hata na wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa pia, na sanduku la Mungu limetwaliwa. Ikawa alipolitaja sanduku la Mungu, Eli akaanguka kitini pake kwa nyuma, kando ya mlango, shingo yake ikavunjika, akafa; maana alikuwa mzee, tena mzito. Naye alikuwa amewaamua Israeli miaka arobaini.
1 Samueli 4:10-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Wafilisti walipiga vita, na Waisraeli walishindwa na kukimbia kila mtu nyumbani kwake. Siku hiyo kulikuwa na mauaji makubwa kwani askari wa miguu 30,000 wa Israeli waliuawa. Sanduku la agano la Mungu lilitekwa, na wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa. Siku hiyohiyo, mtu mmoja wa kabila la Benyamini alikimbia kutoka mstari wa mbele wa mapigano mpaka Shilo huku mavazi yake yakiwa yamechanika na akiwa na mavumbi kichwani. Eli, akiwa na wasiwasi moyoni kuhusu sanduku la Mungu, alikuwa ameketi kwenye kiti chake, kando ya barabara akiangalia. Yule mtu alipowasili mjini na kueleza habari hizo, mji mzima ulilia kwa sauti. Eli aliposikia sauti ya kilio, akauliza, “Kelele hizo ni za nini?” Yule mtu akaenda haraka kwa Eli ili kumpa habari hizo. Wakati huo, Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane na macho yake yalikuwa yamepofuka. Yule mtu akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi; nimekimbia kutoka vitani leo.” Eli akamwuliza, “Mwanangu, mambo yalikuwaje huko?” Yule aliyeleta habari akasema, “Waisraeli wamewakimbia Wafilisti. Kumekuwa na mauaji makubwa miongoni mwa Waisraeli. Zaidi ya yote, wanao wote wawili, Hofni na Finehasi, wameuawa, na sanduku la agano la Mungu limetekwa.” Huyo mtu alipotaja tu sanduku la Mungu, Eli alianguka chali kutoka kwenye kiti chake kando ya lango. Eli alipoanguka hivyo, shingo yake ilivunjika kwani alikuwa mzee na mnene, naye akafariki. Eli alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka arubaini.
1 Samueli 4:10-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia hemani mwake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari 30,000 waendao kwa miguu. Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa. Siku ile ile mtu mmoja wa kabila la Benyamini akakimbia kutoka kwenye uwanja wa vita na kwenda Shilo, nguo zake zikiwa zimeraruka na akiwa na mavumbi kichwani mwake. Alipofika, Eli alikuwa ameketi juu ya kiti chake kando ya barabara akiangalia, kwa sababu moyo wake ulikuwa na hofu kwa ajili ya Sanduku la Mungu. Mtu yule alipoingia mjini na kueleza kilichokuwa kimetokea, mji wote ukalia. Eli akasikia kelele za kilio, naye akauliza, “Ni nini maana ya makelele haya?” Yule mtu akafanya haraka kwenda kwa Eli, wakati huu Eli alikuwa na miaka tisini na minane nayo macho yake yalikuwa yamepofuka na hakuweza kuona. Akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi, nimekimbia kutoka huko leo hii.” Eli akamuuliza, “Je, mwanangu, ni nini kimetokea huko?” Yule mtu aliyeleta habari akajibu, “Israeli amekimbia mbele ya Wafilisti, nalo jeshi limepata hasara kubwa. Pia wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa, na Sanduku la Mungu limetekwa.” Mara alipotaja Sanduku la Mungu, Eli alianguka kutoka kwenye kiti chake kwa nyuma kando ya lango. Shingo yake ikavunjika naye akafa, kwa kuwa alikuwa mzee tena mzito. Alikuwa amewaongoza Israeli kwa miaka arobaini.