1 Samueli 4:10-18
1 Samueli 4:10-18 BHN
Wafilisti walipiga vita, na Waisraeli walishindwa na kukimbia kila mtu nyumbani kwake. Siku hiyo kulikuwa na mauaji makubwa kwani askari wa miguu 30,000 wa Israeli waliuawa. Sanduku la agano la Mungu lilitekwa, na wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa. Siku hiyohiyo, mtu mmoja wa kabila la Benyamini alikimbia kutoka mstari wa mbele wa mapigano mpaka Shilo huku mavazi yake yakiwa yamechanika na akiwa na mavumbi kichwani. Eli, akiwa na wasiwasi moyoni kuhusu sanduku la Mungu, alikuwa ameketi kwenye kiti chake, kando ya barabara akiangalia. Yule mtu alipowasili mjini na kueleza habari hizo, mji mzima ulilia kwa sauti. Eli aliposikia sauti ya kilio, akauliza, “Kelele hizo ni za nini?” Yule mtu akaenda haraka kwa Eli ili kumpa habari hizo. Wakati huo, Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane na macho yake yalikuwa yamepofuka. Yule mtu akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi; nimekimbia kutoka vitani leo.” Eli akamwuliza, “Mwanangu, mambo yalikuwaje huko?” Yule aliyeleta habari akasema, “Waisraeli wamewakimbia Wafilisti. Kumekuwa na mauaji makubwa miongoni mwa Waisraeli. Zaidi ya yote, wanao wote wawili, Hofni na Finehasi, wameuawa, na sanduku la agano la Mungu limetekwa.” Huyo mtu alipotaja tu sanduku la Mungu, Eli alianguka chali kutoka kwenye kiti chake kando ya lango. Eli alipoanguka hivyo, shingo yake ilivunjika kwani alikuwa mzee na mnene, naye akafariki. Eli alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka arubaini.