1 Samueli 3:1-21
1 Samueli 3:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, kijana Samueli alipokuwa anamtumikia Mwenyezi-Mungu chini ya uangalizi wa Eli, ujumbe kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ulikuwa haba sana; hata na maono kutoka kwake yalipatikana mara chache. Siku moja usiku, Eli ambaye macho yake yalikuwa yamefifia, alikuwa amelala katika chumba chake. Samueli naye alikuwa amelala ndani ya hekalu la Mwenyezi-Mungu karibu na sanduku la agano la Mungu. Taa ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa bado inawaka kwani kulikuwa hakujapambazuka. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwita Samueli! Naye Samueli, akaitika, “Naam!” Kisha Samueli akamwendea Eli kwa haraka, akamwambia, “Nimekuja kwani umeniita.” Lakini Eli akamwambia, “Mimi sijakuita. Nenda ukalale.” Samueli akarudi na kulala. Mwenyezi-Mungu akamwita tena, “Samueli!” Samueli akaamka, akamwendea Eli na kumwambia, “Nimekuja, kwani umeniita.” Lakini Eli akamwambia, “Sikukuita mwanangu, kalale tena.” Samueli alikuwa hamjui Mwenyezi-Mungu bado, wala ujumbe wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa bado haujafunuliwa kwake. Mwenyezi-Mungu akamwita Samueli kwa mara ya tatu. Samueli akaamka, akamwendea Eli na kumwambia, “Nimekuja, kwani umeniita.” Ndipo Eli alipotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyemwita Samueli. Kwa hiyo Eli akamwambia Samueli, “Nenda ukalale, na akikuita, mwambie hivi: ‘Sema, ee Mwenyezi-Mungu, kwani mimi mtumishi wako nasikiliza.’” Hivyo Samueli akarudi na kulala mahali pake. Baadaye Mwenyezi-Mungu akaja na kusimama hapo, akamwita Samueli kama hapo awali, “Samueli! Samueli!” Samueli akasema, “Sema, kwani mimi mtumishi wako nasikiliza.” Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Tazama, nataka kutenda jambo fulani katika Israeli ambalo kila atakayesikia, atashtuka kulisikia. Siku hiyo, nitatimiza yale yote niliyosema tangu mwanzo hadi mwisho dhidi ya Eli kuhusu jamaa yake. Nimekwisha mwambia kuwa nitaiadhibu jamaa yake milele, kwa uovu anaoujua kwa sababu watoto wake wa kiume wamenikufuru mimi na hakuwazuia. Kwa hiyo naapa kuhusu jamaa ya Eli kwamba uovu wao hautaondolewa kamwe kwa tambiko wala kwa sadaka.” Samueli akalala pale hadi asubuhi, kisha akaamka na kufungua milango ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Lakini Samueli aliogopa kumwambia Eli maono hayo. Hata hivyo, Eli alimwita Samueli, akamwambia, “Mwanangu Samueli.” Samueli akaitika, “Naam!” Eli akamwuliza, “Je, Mwenyezi-Mungu alikuambia nini? Usinifiche alichokuambia. Ikiwa utanificha alichokuambia, Mungu atakuadhibu vikali.” Basi, Samueli akamweleza Eli yote aliyoambiwa, bila kumficha chochote. Ndipo Eli akasema, “Yeye ni Mwenyezi-Mungu; na afanye anachoona ni chema kwake.” Samueli aliendelea kukua na Mwenyezi-Mungu akawa pamoja naye, na yale yote aliyosema hakuna hata moja ambalo halikutimia. Watu wote kote nchini Israeli toka Dani, upande wa kaskazini, hadi Beer-sheba, upande wa kusini, wakajua kuwa Samueli alikuwa nabii mwaminifu wa Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu alizidi kujionesha huko Shilo, ambako alimtokea Samueli na kuongea naye. Naye Samueli aliposema kitu, Waisraeli wote walimsikiliza.
1 Samueli 3:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, mtoto Samweli akamtumikia BWANA mbele ya Eli. Na neno la BWANA lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri. Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona), na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la BWANA, palipokuwa na sanduku la Mungu; basi, wakati huo BWANA akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa. Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena. BWANA akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. Basi Samweli alikuwa hamjui BWANA bado, na neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. BWANA akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa BWANA ndiye aliyemwita yule mtoto. Kwa hiyo Eli akamwambia Samweli, Nenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake. BWANA akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. BWANA akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha. Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli kuhusu nyumba yake, tangu mwanzo hadi mwisho. Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia. Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele. Naye Samweli akalala hadi asubuhi, akaifungua milango ya nyumba ya BWANA. Samweli akaogopa kumjulisha Eli maono hayo. Basi Eli akamwita Samweli, akasema, Samweli, mwanangu. Naye akajibu, Mimi hapa. Akamwuliza, Ni neno gani alilosema nawe? Nakusihi, usinifiche; Mungu akufanyie vivyo hivyo, na kuzidi, ukinificha lolote katika hayo yote BWANA aliyosema nawe. Basi Samweli akamwambia kila neno, asimfiche lolote. Naye akasema, Ndiye BWANA; na afanye alionalo kuwa ni jema. Samweli akakua, naye BWANA alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lolote lianguke chini. Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa BWANA. Naye BWANA akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa BWANA akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la BWANA. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote.
1 Samueli 3:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, mtoto Samweli akamtumikia BWANA mbele ya Eli. Na neno la BWANA lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri. Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona), na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la BWANA, palipokuwa na sanduku la Mungu; basi, wakati huo BWANA akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa. Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena. BWANA akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. Basi Samweli alikuwa hamjui BWANA bado, na neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. BWANA akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa BWANA ndiye aliyemwita yule mtoto. Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake. BWANA akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. BWANA akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha. Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho. Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia. Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele. Naye Samweli akalala hata asubuhi, akaifungua milango ya nyumba ya BWANA. Samweli akaogopa kumjulisha Eli maono hayo. Basi Eli akamwita Samweli, akasema, Samweli, mwanangu. Naye akajibu, Mimi hapa. Akamwuliza, Ni neno gani alilosema nawe? Nakusihi, usinifiche; Mungu akufanyie vivyo hivyo, na kuzidi, ukinificha lo lote katika hayo yote BWANA aliyosema nawe. Basi Samweli akamwambia kila neno, asimfiche lo lote. Naye akasema, Ndiye BWANA; na afanye alionalo kuwa ni jema. Samweli akakua, naye BWANA alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini. Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa BWANA. Naye BWANA akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa BWANA akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la BWANA. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote.
1 Samueli 3:1-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kijana Samweli alihudumu mbele za BWANA chini ya Eli. Katika siku zile neno la Mungu lilikuwa adimu, hapakuwepo na maono mengi. Usiku mmoja Eli, ambaye macho yake yalikuwa yamefifia sana kiasi kwamba aliona kwa shida sana, alikuwa amelala mahali pake pa kawaida. Taa ya Mungu bado ilikuwa haijazimika, na Samweli alikuwa amelala Hekaluni mwa BWANA, ambapo Sanduku la Mungu lilikuwako. Kisha BWANA akamwita Samweli. Samweli akajibu, “Mimi hapa.” Naye akakimbia kwa Eli na kumwambia, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” Lakini Eli akasema, “Sikukuita; rudi ukalale.” Hivyo akaenda kulala. BWANA akaita tena, “Samweli!” Naye Samweli akaamka, kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” Eli akasema, “Mwanangu, sikukuita, rudi ukalale.” Wakati huu Samweli alikuwa bado hajamjua BWANA. Neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. BWANA akamwita Samweli mara ya tatu, naye Samweli akaamka kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” Ndipo Eli akatambua kuwa BWANA alikuwa akimwita kijana. Hivyo Eli akamwambia Samweli, “Nenda ukalale, na kama akikuita, sema, ‘Nena BWANA, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akaenda na kulala mahali pake. BWANA akaja akasimama hapo, akiita kama mara zile nyingine, “Samweli! Samweli!” Kisha Samweli akasema, “Nena BWANA, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.” Naye BWANA akamwambia Samweli: “Tazama, nipo karibu kufanya kitu katika Israeli ambacho kitafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia yawashe. Wakati huo nitatimiza dhidi ya Eli kila kitu nilichonena dhidi ya jamaa yake, kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Kwa kuwa nilimwambia kwamba ningehukumu jamaa yake milele kwa sababu ya dhambi aliyoijua, wanawe kumkufuru Mungu, naye akashindwa kuwazuia. Kwa hiyo, nikaapa kuhusu nyumba ya Eli, ‘Hatia ya nyumba ya Eli kamwe haitaweza kufidiwa kwa dhabihu au sadaka.’ ” Samweli akalala mpaka asubuhi, kisha akafungua milango ya nyumba ya BWANA. Aliogopa kumwambia Eli yale maono, lakini Eli akamwita na kumwambia, “Samweli mwanangu.” Samweli akamjibu, “Mimi hapa.” Eli akamuuliza, “Ni nini alichokuambia? Usinifiche. BWANA na ashughulike nawe, tena kwa ukali, kama utanificha chochote alichokuambia.” Kwa hiyo Samweli akamwambia kila kitu, bila kumficha chochote. Ndipo Eli akasema, “Yeye ni BWANA; na afanye lile lililo jema machoni pake!” BWANA alikuwa pamoja na Samweli alipokuwa akikua, na hakuacha hata moja ya maneno yake lianguke chini. Nao Israeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba wakatambua kuwa Samweli amethibitishwa kuwa nabii wa BWANA. BWANA akaendelea kutokea huko Shilo, na huko kujidhihirisha kwa Samweli kwa njia ya neno lake.