Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 3:1-21

1 Samweli 3:1-21 NEN

Kijana Samweli alihudumu mbele za BWANA chini ya Eli. Katika siku zile neno la Mungu lilikuwa adimu, hapakuwepo na maono mengi. Usiku mmoja Eli, ambaye macho yake yalikuwa yamefifia sana kiasi kwamba aliona kwa shida sana, alikuwa amelala mahali pake pa kawaida. Taa ya Mungu bado ilikuwa haijazimika, na Samweli alikuwa amelala Hekaluni mwa BWANA, ambapo Sanduku la Mungu lilikuwako. Kisha BWANA akamwita Samweli. Samweli akajibu, “Mimi hapa.” Naye akakimbia kwa Eli na kumwambia, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” Lakini Eli akasema, “Sikukuita; rudi ukalale.” Hivyo akaenda kulala. BWANA akaita tena, “Samweli!” Naye Samweli akaamka, kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” Eli akasema, “Mwanangu, sikukuita, rudi ukalale.” Wakati huu Samweli alikuwa bado hajamjua BWANA. Neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. BWANA akamwita Samweli mara ya tatu, naye Samweli akaamka kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” Ndipo Eli akatambua kuwa BWANA alikuwa akimwita kijana. Hivyo Eli akamwambia Samweli, “Nenda ukalale, na kama akikuita, sema, ‘Nena BWANA, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akaenda na kulala mahali pake. BWANA akaja akasimama hapo, akiita kama mara zile nyingine, “Samweli! Samweli!” Kisha Samweli akasema, “Nena BWANA, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.” Naye BWANA akamwambia Samweli: “Tazama, nipo karibu kufanya kitu katika Israeli ambacho kitafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia yawashe. Wakati huo nitatimiza dhidi ya Eli kila kitu nilichonena dhidi ya jamaa yake, kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Kwa kuwa nilimwambia kwamba ningehukumu jamaa yake milele kwa sababu ya dhambi aliyoijua, wanawe kumkufuru Mungu, naye akashindwa kuwazuia. Kwa hiyo, nikaapa kuhusu nyumba ya Eli, ‘Hatia ya nyumba ya Eli kamwe haitaweza kufidiwa kwa dhabihu au sadaka.’ ” Samweli akalala mpaka asubuhi, kisha akafungua milango ya nyumba ya BWANA. Aliogopa kumwambia Eli yale maono, lakini Eli akamwita na kumwambia, “Samweli mwanangu.” Samweli akamjibu, “Mimi hapa.” Eli akamuuliza, “Ni nini alichokuambia? Usinifiche. BWANA na ashughulike nawe, tena kwa ukali, kama utanificha chochote alichokuambia.” Kwa hiyo Samweli akamwambia kila kitu, bila kumficha chochote. Ndipo Eli akasema, “Yeye ni BWANA; na afanye lile lililo jema machoni pake!” BWANA alikuwa pamoja na Samweli alipokuwa akikua, na hakuacha hata moja ya maneno yake lianguke chini. Nao Israeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba wakatambua kuwa Samweli amethibitishwa kuwa nabii wa BWANA. BWANA akaendelea kutokea huko Shilo, na huko kujidhihirisha kwa Samweli kwa njia ya neno lake.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Samweli 3:1-21