Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 28:1-14

1 Samueli 28:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya muda fulani, Wafilisti walikusanya majeshi yao tayari kwenda kupigana na Waisraeli. Akishi akamwambia Daudi, “Uelewe vizuri kwamba wewe na watu wako mnapaswa kwenda pamoja nami kupigana vita.” Daudi akamjibu Akishi, “Naam! Utaona kitu ambacho mtumishi wako anaweza kufanya.” Akishi akamwambia, “Nami nitakufanya kuwa mlinzi wangu binafsi wa maisha.” Wakati huu, Samueli alikuwa amekwisha fariki, na Waisraeli wote walikuwa wamekwisha mwombolezea na kumzika katika mji wake Rama. Shauli alikuwa amewafukuza kutoka nchini watabiri na wachawi. Wafilisti walikusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu; na Shauli aliwakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao kwenye mlima Gilboa. Shauli alipoona jeshi la Wafilisti alianza kuogopa, akaanza kutetemeka kwa hofu aliyokuwa nayo moyoni mwake. Hata alipomwomba Mwenyezi-Mungu shauri, Mwenyezi-Mungu hakumjibu kwa ndoto, kwa mawe ya kauli, wala kwa njia ya manabii. Ndipo Shauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke ambaye anaweza kutabiri ili nimwendee na kumtaka shauri.” Watumishi wake wakamjibu, “Yuko mtabiri mmoja huko Endori.” Basi, Shauli akajigeuza na kuvaa mavazi mengine, akaenda huko pamoja na watu wake wawili. Walifika kwa huyo mwanamke usiku, akamwambia, “Nitabirie kwa pepo, umlete duniani yeyote nitakayekutajia.” Yule mwanamke akamwambia, “Wewe unajua kwa hakika kuwa mfalme Shauli amewaangamiza kabisa watabiri na wachawi wote katika nchi ya Israeli. Sasa kwa nini unaniwekea mtego wa kuninasa na kuniua?” Shauli akamwapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akisema, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba hakuna adhabu yoyote itakayokupata kutokana na jambo hili.” Yule mwanamke akamwuliza, “Je, nikuletee nani kutoka huko?” Shauli akajibu, “Niletee Samueli.” Yule mwanamke alipomwona Samueli alilia kwa sauti kuu, akamwambia Shauli, “Kwa nini umenidanganya? Wewe ni Shauli!” Mfalme Shauli akamwambia, “Usiogope! Unaona nini?” Yule mwanamke akamjibu, “Naona mungu akitokea ardhini.” Shauli akamwambia mwanamke, “Ni mfano wa nani?” Yule mwanamke akamwambia, “Mwanamume mzee anapanda juu, naye amejizungushia joho.” Hapo, Shauli akatambua kwamba huyo ni Samueli. Shauli akainama hadi chini, na kusujudu.

1 Samueli 28:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa siku zile hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao waende vitani, ili kupigana na Israeli. Naye Akishi akamwambia Daudi, Jua hakika ya kuwa wewe utatoka pamoja nami jeshini, wewe na watu wako. Naye Daudi akamwambia Akishi, Vema, sasa utajua atakayoyatenda mtumishi wako. Naye Akishi akamwambia Daudi, Haya basi! Mimi nitakufanya wewe kuwa mlinzi wangu binafsi daima. Basi Samweli alikuwa amefariki dunia, nao Waisraeli wote walikuwa wamemwomboleza, na kumzika huko Rama, ndani ya mji wake mwenyewe. Tena Sauli alikuwa amewaondolea mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi. Nao Wafilisti wakakusanyika, wakaenda kufanya kambi huko Shunemu; naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote, nao wakapiga hema katika Gilboa. Basi alipowaona hao majeshi ya Wafilisti, huyo Sauli akaogopa, na moyo wake ukatetemeka sana. Lakini Sauli alipouliza kwa BWANA, BWANA hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii. Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori. Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye pamoja na watu wawili wakamfikia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukaniletee yeye nitakayemtaja kwako. Yule mwanamke akamwambia, Angalia, unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili kuniua? Naye Sauli akamwapia kwa BWANA, akasema, Aishivyo BWANA, haitakupata adhabu yoyote kwa jambo hili. Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekuletea? Naye akasema, Niletee Samweli. Hata yule mwanamke alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli, akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli. Mfalme akamwambia Usiogope; unaona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu akitoka katika nchi. Naye akamwuliza, Ni mfano wa nini? Akajibu, Ni mzee anazuka; naye amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe, akainama uso wake mpaka chini, akasujudia.

1 Samueli 28:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa siku zile hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao waende vitani, ili kupigana na Israeli. Naye Akishi akamwambia Daudi, Jua hakika ya kuwa wewe utatoka pamoja nami jeshini, wewe na watu wako. Naye Daudi akamwambia Akishi, Vema, sasa utajua atakayoyatenda mtumishi wako. Naye Akishi akamwambia Daudi, Haya basi! Mimi nitakufanya wewe kuwa mlinda kichwa changu daima. Basi Samweli alikuwa amefariki dunia, nao Israeli wote walikuwa wamemwomboleza, na kumzika huko Rama, ndani ya mji wake mwenyewe. Tena Sauli alikuwa amewaondolea mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi. Nao Wafilisti wakakusanyika, wakaenda kufanya kambi huko Shunemu; naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote, nao wakapiga hema katika Gilboa. Basi alipowaona hao majeshi ya Wafilisti, huyo Sauli akaogopa, na moyo wake ukatetemeka sana. Lakini Sauli alipouliza kwa BWANA, BWANA hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii. Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori. Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye na watu wawili pamoja naye, wakamfikilia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukanipandishie yeye nitakayemtaja kwako. Yule mwanamke akamwambia, Angalia, unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili kuniua? Naye Sauli akamwapia kwa BWANA, akasema, Aishivyo BWANA, haitakupata adhabu yo yote kwa jambo hili. Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekupandishia? Naye akasema, Nipandishie Samweli. Hata yule mwanamke alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli, akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli. Mfalme akamwambia Usiogope; waona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu anatoka katika nchi. Naye akamwuliza, Ni mfano wa nini? Akajibu, Ni mzee anazuka; naye amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe, akainama uso wake mpaka nchi, akasujudia.

1 Samueli 28:1-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Siku zile Wafilisti wakakusanya majeshi yao ili kupigana vita dhidi ya Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Lazima ujue kuwa wewe pamoja na watu wako mtafuatana nami kwenda vitani.” Daudi akasema, “Ndipo wewe mwenyewe utakapojionea jambo ambalo mtumishi wako anaweza kufanya.” Akishi akamjibu Daudi, “Vyema sana, mimi nitakufanya uwe mlinzi wangu daima.” Wakati huo Samweli alikuwa amekufa, nao Waisraeli wote walikuwa wamemwombolezea na kumzika kwenye mji wake mwenyewe huko Rama. Sauli alikuwa amewafukuza waaguzi na wachawi. Wafilisti wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu, naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao huko Gilboa. Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa; moyo wake ukajawa na hofu kuu. Ndipo Sauli akauliza ushauri kwa Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kupitia manabii. Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwaguzi ili nimwendee, nipate kuuliza kwake.” Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.” Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie kwa uaguzi, unipandishie yule nitakayekutajia.” Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya Mfalme Sauli. Amewakatilia mbali waaguzi, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?” Sauli akamwapia huyo mwanamke kwa Jina la Mwenyezi Mungu, akasema, “Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.” Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani?” Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.” Yule mwanamke alipomwona Samweli, alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamuuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.” Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini?” Yule mwanamke akasema, “Naona mungu unapanda kutoka ardhini.” Sauli akamuuliza, “Ni mfano wa nini?” Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.” Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu, uso wake ukagusa chini.