Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 22:1-12

1 Wafalme 22:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Kwa muda wa miaka mitatu hivi, kulikuwa na amani kati ya Israeli na Aramu. Lakini mnamo mwaka wa tatu, Yehoshafati, mfalme wa Yuda, alifika kumtembelea Ahabu, mfalme wa Israeli. Ahabu akawaambia watumishi wake, “Je, hamjui kwamba Ramoth-gileadi ni mali yetu? Mbona basi tunajikalia tu bila kuunyakua kutoka kwa mfalme wa Aramu?” Kisha akamwambia Yehoshafati, “Je, utaandamana nami kupigana huko Ramoth-gileadi?” Naye Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Naam; mimi na wewe ni kitu kimoja, na pia watu wangu ni watu wako, farasi wangu ni farasi wako.” Kisha Yehoshafati aliendelea kumwambia mfalme wa Israeli: “Lakini, kwanza mwulize Mwenyezi-Mungu ushauri.” Basi, Ahabu akaitisha kikao cha manabii wapatao 400, akawauliza, “Je, niende nikaushambulie mji wa Ramoth-gileadi au nisiende?” Wao wakamjibu: “Nenda! Mwenyezi-Mungu atakupatia ushindi.” Lakini, Yehoshafati akasema, “Je, hapa hakuna nabii mwingine wa Mwenyezi-Mungu ambaye twaweza kumwuliza shauri?” Naye mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Yupo, bado mmoja, Mikaya mwana wa Imla. Yeye twaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu. Lakini namchukia sana kwa sababu yeye, kamwe hatabiri jambo jema juu yangu, ila mabaya tu.” Yehoshafati akamwambia, “Si vizuri mfalme kusema hivyo.” Basi, Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwita mtumishi mmoja, akamwamuru, “Haraka! Nenda ukamlete Mikaya mwana wa Imla.” Wakati huo, mfalme wa Israeli pamoja na Yehoshafati mfalme wa Yuda, walikuwa wameketi katika viti vyao vya enzi wakikaa kwenye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la kuingilia mjini Samaria nao walikuwa wamevalia mavazi yao ya kifalme; wakati huo manabii wote wakawa wanatabiri mbele yao. Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Waaramu na kuwaangamiza.’” Hata wale manabii wengine wote wakatabiri vivyo hivyo, wakasema, “Nenda uushambulie Ramoth-gileadi, utashinda! Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.”

1 Wafalme 22:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wakakaa miaka mitatu pasipo vita kati ya Shamu na Israeli. Ikawa, mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme Wa Yuda akamshukia mfalme wa Israeli. Mfalme wa Israeli akawaambia watumishi wake, Je! Hamjui ya kuwa Ramoth-Gileadi ni yetu? Nasi tumenyamaza tusiitwae mkononi mwa mfalme wa Shamu? Akamwambia Yehoshafati, Je! Utakwenda nami tupigane na Ramoth-gileadi? Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Mimi ni kama wewe, na watu wangu ni kama watu wako na farasi wangu ni kama farasi wako. Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la BWANA. Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya pamoja manabii, kama watu mia nne. Akawaambia Je! Niende juu ya Ramoth-Gileadi kuupiga vita, au ninyamaze? Wakasema Kwea; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii mwingine wa BWANA, ili tumwulize yeye? Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza BWANA kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi. Ndipo mfalme wa Israeli akamwita ofisa, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla. Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao. Na Sedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike. Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme.

1 Wafalme 22:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wakakaa miaka mitatu pasipo vita kati ya Shamu na Israeli. Ikawa, mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme Wa Yuda akamshukia mfalme wa Israeli. Mfalme wa Israeli akawaambia watumishi wake, Je! Hamjui ya kuwa Ramoth-Gileadi ni yetu? Nasi tumenyamaza tusiitwae mkononi mwa mfalme wa Shamu? Akamwambia Yehoshafati, Je! Utakwenda nami tupigane na Ramoth-gileadi? Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Mimi ni kama wewe, na watu wangu ni kama watu wako na farasi zangu ni kama farasi zako. Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la BWANA. Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya pamoja manabii, kama watu mia nne. Akawaambia Je! Niende juu ya Ramoth-Gileadi kuupiga vita, au ninyamaze? Wakasema Kwea; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii wa BWANA tena, ili tumwulize yeye? Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza BWANA kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi. Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla. Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao. Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike. Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme.

1 Wafalme 22:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kwa miaka mitatu hapakuwa na vita kati ya Aramu na Israeli. Lakini katika mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme wa Yuda akashuka kwenda kumwona mfalme wa Israeli. Mfalme wa Israeli alikuwa amewaambia maafisa wake, “Je, hamjui Ramoth-Gileadi ni mali yetu na bado hatufanyi chochote kuirudisha kwetu kutoka kwa mfalme wa Aramu?” Kwa hiyo akamuuliza Yehoshafati, “Je, utakwenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?” Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.” Lakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta shauri la BWANA.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, niende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?” Wakajibu, “Naam, nenda, kwa kuwa Bwana ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.” Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa BWANA hapa ambaye tunaweza kumuuliza?” Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia yeye twaweza kumuuliza shauri la BWANA, lakini namchukia kwa sababu huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu mimi, lakini kila mara hunitabiria mabaya tu. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.” Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.” Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, pamoja na manabii wote wakiwa wakitabiri mbele yao. Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma, akatangaza, “Hivi ndivyo BWANA asemavyo, ‘Kwa hizi pembe utawapiga na kuwarudisha Waaramu nyuma mpaka wameangamizwa.’ ” Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa BWANA ataitia mkononi mwa mfalme.”