Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 22:1-12

1 Wafalme 22:1-12 NEN

Kwa miaka mitatu hapakuwa na vita kati ya Aramu na Israeli. Lakini katika mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme wa Yuda akashuka kwenda kumwona mfalme wa Israeli. Mfalme wa Israeli alikuwa amewaambia maafisa wake, “Je, hamjui Ramoth-Gileadi ni mali yetu na bado hatufanyi chochote kuirudisha kwetu kutoka kwa mfalme wa Aramu?” Kwa hiyo akamuuliza Yehoshafati, “Je, utakwenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?” Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.” Lakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta shauri la BWANA.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, niende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?” Wakajibu, “Naam, nenda, kwa kuwa Bwana ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.” Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa BWANA hapa ambaye tunaweza kumuuliza?” Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia yeye twaweza kumuuliza shauri la BWANA, lakini namchukia kwa sababu huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu mimi, lakini kila mara hunitabiria mabaya tu. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.” Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.” Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, pamoja na manabii wote wakiwa wakitabiri mbele yao. Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma, akatangaza, “Hivi ndivyo BWANA asemavyo, ‘Kwa hizi pembe utawapiga na kuwarudisha Waaramu nyuma mpaka wameangamizwa.’ ” Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa BWANA ataitia mkononi mwa mfalme.”