Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 17:8-24

1 Wafalme 17:8-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Hapo, neno la Mwenyezi-Mungu, lilimjia Elia: “Ondoka uende mjini Sarefathi, karibu na Sidoni, ukae huko. Nimemwamuru mwanamke mmoja mjane akupatie chakula huko.” Basi, Elia akaondoka, akaenda Sarefathi. Alipofika penye lango la mji, alimkuta mwanamke mmoja mjane anaokota kuni. Elia akamwita mwanamke huyo na kumwambia “Niletee maji ninywe.” Yule mwanamke alipokuwa anaondoka, Elia akamwita tena na kumwambia, “Niletee na kipande cha mkate pia.” Huyo mwanamke akamwambia, “Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wako aliye hai, sina mkate hata kidogo. Nilicho nacho ni konzi ya unga katika chungu na mafuta kidogo katika chupa. Nimefika hapa kuokota kuni, kisha niende nyumbani kupika chakula hicho, mwanangu na mimi tule, kisha tufe.” Elia akamwambia, “Usiogope. Nenda ukafanye kama ulivyosema. Lakini nitengenezee mimi kwanza na kuniletea andazi dogo, kisha jitengenezee wewe na mwanao chakula. Maana, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Unga ulioko chunguni mwako hautapungua wala mafuta yaliomo ndani ya chupa hayataisha, mpaka hapo mimi Mwenyezi-Mungu nitakaponyesha mvua nchini.’” Basi, huyo mwanamke mjane akaenda akafanya kama alivyoambiwa na Elia hata mama huyo, jamaa yake na Elia wakapata chakula kwa siku nyingi. Unga chunguni haukupunguka, wala mafuta katika chupa hayakwisha sawa kabisa na neno la Mwenyezi-Mungu alilomwambia Elia aseme. Baada ya hayo, mwana wa mwanamke huyo mwenye nyumba akaugua, na hali yake ikazidi kuwa mbaya, hata mwishowe akafariki. Huyo mwanamke akamwambia Elia, “Ewe mtu wa Mungu, una kisa gani nami? Kumbe ulikuja kwangu kuzifichua dhambi zangu na kusababisha kifo cha mwanangu?” Elia akamwambia, “Nipe mwanao.” Basi, Elia akamtwaa mtoto kifuani pa mama yake, akamchukua juu chumbani mwake, akamlaza juu ya kitanda chake. Kisha akamsihi Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, je, hata mwanamke huyu mjane ambaye ninakaa kwake, naye ananitunza, unamletea balaa kwa kumwua mwanawe?” Kisha Elia akajinyosha juu ya mtoto huyo mara tatu na kumwomba Mwenyezi-Mungu, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mrudishie mtoto huyu roho yake!” Mwenyezi-Mungu akasikiliza ombi la Elia; mtoto akaanza kupumua tena. Elia akamrudisha mtoto chini kwa mama yake, akamwambia, “Tazama! Mwanao yu hai.” Huyo mwanamke mjane akamwambia Elia, “Sasa najua kwa hakika kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na maneno aliyokupa Mwenyezi-Mungu uyaseme ni ya kweli.”

1 Wafalme 17:8-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Neno la BWANA likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama BWANA, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie mwenyewe na mwanangu, tule kisha tufe. Eliya akamwambia, Usiogope; nenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujitengenezee na mwanao. Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa kinywa cha Eliya. Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. Akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumwua mwanawe? Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. BWANA akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka. Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka ghorofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai. Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la BWANA kinywani mwako ni kweli.

1 Wafalme 17:8-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha neno la BWANA likamjia, kusema, “Ondoka, uende Sarepta ya Sidoni na ukae huko. Nimemwagiza mjane katika sehemu ile akupatie chakula.” Hivyo akaenda Sarepta. Alipofika kwenye lango la mji, mjane alikuwa huko akiokota kuni. Akamwita na kumwambia, “Naomba uniletee maji kidogo kwenye gudulia ili niweze kunywa.” Alipokuwa anakwenda kumletea, akamwita akasema, “Tafadhali niletee pia kipande cha mkate.” Akamjibu, “Hakika kama BWANA Mungu wako aishivyo, sina mkate wowote, isipokuwa konzi ya unga kwenye gudulia na mafuta kidogo kwenye chupa. Ninakusanya kuni chache nipeleke nyumbani na nikapike chakula kwa ajili yangu na mwanangu, ili kwamba tule, kiishe, tukafe.” Eliya akamwambia, “Usiogope. Nenda nyumbani ukafanye kama ulivyosema. Lakini kwanza unitengenezee mimi mkate mdogo kutoka vile ulivyo navyo kisha uniletee na ndipo utayarishe chochote kwa ajili yako na mwanao. Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli: ‘Lile gudulia la unga halitakwisha wala ile chupa ya mafuta haitakauka hadi siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi.’ ” Akaondoka na kufanya kama Eliya alivyomwambia. Kwa hiyo kukawa na chakula kila siku kwa ajili ya Eliya, yule mwanamke na jamaa yake. Kwa kuwa lile gudulia la unga halikwisha na ile chupa ya mafuta haikukauka, sawasawa na lile neno la BWANA alilosema Eliya. Baada ya muda, mwana wa yule mwanamke mwenye nyumba akaugua. Hali yake ikaendelea kuwa mbaya sana, na hatimaye akaacha kupumua. Akamwambia Eliya, “Una nini dhidi yangu, ewe mtu wa Mungu? Umekuja ili kukumbushia dhambi yangu na kusababisha kifo cha mwanangu?” Eliya akamjibu, “Nipe mwanao.” Eliya akampokea kutoka kifuani mwake, akambeba mpaka chumba cha juu alipokuwa anaishi, akamlaza kitandani mwake. Kisha akamlilia BWANA, akasema “Ee BWANA Mungu wangu, je, pia umeleta msiba juu ya mjane huyu ninayeishi pamoja naye, kwa kusababisha mwanawe kufa?” Kisha akajinyoosha juu ya kijana mara tatu na kumlilia BWANA, akisema, “Ee BWANA Mungu wangu, nakuomba roho ya huyu kijana imrudie!” BWANA akasikia kilio cha Eliya, na roho ya kijana ikamrudia, naye akafufuka. Eliya akamtwaa kijana na kumbeba kutoka chumbani mwake akamshusha kumpeleka kwenye nyumba. Akampa mama yake na kusema, “Tazama, mwanao yu hai!” Ndipo yule mwanamke akamwambia Eliya, “Sasa ninajua kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na kwamba neno la BWANA kutoka kinywani mwako ni kweli.”

1 Wafalme 17:8-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Neno la BWANA likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama BWANA, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa kinywa cha Eliya. Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. Akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. BWANA akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka. Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka orofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai. Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la BWANA kinywani mwako ni kweli.