1 Wafalme 17:17-24
1 Wafalme 17:17-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya hayo, mwana wa mwanamke huyo mwenye nyumba akaugua, na hali yake ikazidi kuwa mbaya, hata mwishowe akafariki. Huyo mwanamke akamwambia Elia, “Ewe mtu wa Mungu, una kisa gani nami? Kumbe ulikuja kwangu kuzifichua dhambi zangu na kusababisha kifo cha mwanangu?” Elia akamwambia, “Nipe mwanao.” Basi, Elia akamtwaa mtoto kifuani pa mama yake, akamchukua juu chumbani mwake, akamlaza juu ya kitanda chake. Kisha akamsihi Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, je, hata mwanamke huyu mjane ambaye ninakaa kwake, naye ananitunza, unamletea balaa kwa kumwua mwanawe?” Kisha Elia akajinyosha juu ya mtoto huyo mara tatu na kumwomba Mwenyezi-Mungu, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mrudishie mtoto huyu roho yake!” Mwenyezi-Mungu akasikiliza ombi la Elia; mtoto akaanza kupumua tena. Elia akamrudisha mtoto chini kwa mama yake, akamwambia, “Tazama! Mwanao yu hai.” Huyo mwanamke mjane akamwambia Elia, “Sasa najua kwa hakika kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na maneno aliyokupa Mwenyezi-Mungu uyaseme ni ya kweli.”
1 Wafalme 17:17-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. Akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumwua mwanawe? Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. BWANA akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka. Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka ghorofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai. Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la BWANA kinywani mwako ni kweli.
1 Wafalme 17:17-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. Akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. BWANA akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka. Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka orofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai. Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la BWANA kinywani mwako ni kweli.
1 Wafalme 17:17-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya muda, mwana wa yule mwanamke mwenye nyumba akaugua. Hali yake ikaendelea kuwa mbaya sana, na hatimaye akaacha kupumua. Akamwambia Eliya, “Una nini dhidi yangu, ewe mtu wa Mungu? Umekuja ili kukumbushia dhambi yangu na kusababisha kifo cha mwanangu?” Eliya akamjibu, “Nipe mwanao.” Eliya akampokea kutoka kifuani mwake, akambeba mpaka chumba cha juu alipokuwa anaishi, akamlaza kitandani mwake. Kisha akamlilia BWANA, akasema “Ee BWANA Mungu wangu, je, pia umeleta msiba juu ya mjane huyu ninayeishi pamoja naye, kwa kusababisha mwanawe kufa?” Kisha akajinyoosha juu ya kijana mara tatu na kumlilia BWANA, akisema, “Ee BWANA Mungu wangu, nakuomba roho ya huyu kijana imrudie!” BWANA akasikia kilio cha Eliya, na roho ya kijana ikamrudia, naye akafufuka. Eliya akamtwaa kijana na kumbeba kutoka chumbani mwake akamshusha kumpeleka kwenye nyumba. Akampa mama yake na kusema, “Tazama, mwanao yu hai!” Ndipo yule mwanamke akamwambia Eliya, “Sasa ninajua kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na kwamba neno la BWANA kutoka kinywani mwako ni kweli.”