1 Wafalme 14:1-31
1 Wafalme 14:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, Abiya mwana wa mfalme Yeroboamu, akawa mgonjwa. Yeroboamu akamwambia mkewe, “Jisingizie kuwa mwingine, uende mjini Shilo anakokaa nabii Ahiya aliyesema kwamba mimi nitakuwa mfalme wa Israeli. Mpelekee mikate kumi, maandazi kadha, na asali chupa moja. Yeye atakuambia yatakayompata mtoto wetu.” Basi, mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda Shilo nyumbani kwa Ahiya. Wakati huo, Ahiya alikuwa hawezi tena kuona sawasawa kwa sababu ya uzee. Mwenyezi-Mungu alikuwa amekwisha mwambia Ahiya kwamba mke wa Yeroboamu alikuwa njiani, anakuja kumwuliza yatakayompata mwanawe mgonjwa, na jinsi atakavyomjibu. Mkewe Yeroboamu alipofika, alijisingizia kuwa mtu mwingine. Lakini Ahiya alipomsikia anaingia mlangoni, alisema, “Karibu ndani mke wa Yeroboamu. Lakini mbona unajisingizia kuwa mtu mwingine? Ninao ujumbe usio mzuri kwako! Nenda ukamwambie Yeroboamu kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Nilikuteua miongoni mwa watu, nikakufanya kuwa kiongozi wa watu wangu, Israeli; nikaurarua ufalme utoke kwa wazawa wa Daudi, nikakupa wewe. Lakini wewe ni kinyume kabisa cha mtumishi wangu Daudi ambaye alizishika amri zangu, akafuata matakwa yangu kwa moyo wake wote na kutenda tu yaliyo sawa mbele ya macho yangu. Wewe umetenda uovu mbaya zaidi kuliko waliotenda wale waliokutangulia; wewe umenikasirisha kwa kujitengenezea miungu mingine na sanamu za kufua, kisha umeniacha. Haya basi, sasa nitailetea balaa jamaa hii yake, Yeroboamu, nitawaua wanaume wote wa jamaa zake katika Israeli, awe mtumwa au huru. Jamaa wake wote nitawateketeza kama mtu ateketezavyo mavi, mpaka yatoweke. Yeyote aliye wa jamaa ya Yeroboamu atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.’” Ahiya akamwambia mkewe Yeroboamu, “Haya inuka, uende zako nyumbani. Mara tu utakapoingia mjini, mwanao atakufa. Watu wote wa Israeli watafanya matanga na kumzika. Walakini, ni huyo tu wa jamaa ya Yeroboamu atakayezikwa, kwani ni yeye tu wa jamaa ya Yeroboamu aliyepata kumpendeza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Tena leo hii, Mwenyezi-Mungu ataweka mfalme mwingine katika Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Naam, tangu sasa, Mwenyezi-Mungu atawapiga watu wa Israeli, nao watatikisika kama unyasi unavyotikiswa mtoni. Atawangoa kutoka nchi hii nzuri aliyowapa babu zao, na kuwatawanya mbali, ngambo ya mto Eufrate, kwa sababu wamemkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa kujitengenezea sanamu za Ashera, mungu wa kike. Mwenyezi-Mungu ataitupa Israeli kwa sababu ya dhambi alizotenda Yeroboamu, na kuwafanya watu wa Israeli pia watende dhambi.” Hapo, mkewe Yeroboamu akaondoka, akashika safari mpaka Tirza. Mara tu alipofika mlangoni, mtoto akafa. Watu wote wa Israeli wakamzika na kufanya matanga kama alivyosema Mwenyezi-Mungu, kwa njia ya nabii Ahiya, mtumishi wake. Matendo mengine ya mfalme Yeroboamu, jinsi alivyopigana vita na alivyotawala, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Yeroboamu alitawala kwa muda wa miaka ishirini na miwili, halafu akafariki, na Nadabu, mwanawe, akatawala mahali pake. Rehoboamu, mwanawe Solomoni, alikuwa na umri wa miaka arubaini na mmoja alipoanza kutawala Yuda. Naye alitawala kwa muda wa miaka kumi na saba katika Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi-Mungu aliuchagua miongoni mwa miji ya makabila yote ya Israeli aabudiwe humo. Mama yake Rehoboamu alikuwa Naama kutoka Amoni. Watu wa Yuda walitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha kwa dhambi zao walizotenda, nyingi kuliko za babu zao. Walijitengenezea pia mahali pa ibada, minara ya kutambikia, na sanamu za Ashera, juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Tena, kukawa na ibada za ukahaba nchini; watu walitenda matendo ya kuchukiza ya mataifa ambayo Mungu aliyafukuza Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini Kanaani. Katika mwaka wa tano wa utawala wa Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri, aliushambulia mji wa Yerusalemu, akaichukua hazina yote ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya ikulu; alichukua kila kitu; pia alichukua ngao zote za dhahabu alizozitengeneza Solomoni. Badala ya ngao hizo, mfalme Rehoboamu alitengeneza ngao za shaba na kuziweka chini ya ulinzi wa wangojamlango wa ikulu. Kila wakati mfalme alipokwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walinzi walizibeba ngao hizo, na baadaye wakazirudisha katika chumba cha ulinzi. Matendo mengine ya mfalme Rehoboamu, na yote aliyoyafanya, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Daima kulikuwako vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. Hatimaye, Rehoboamu alifariki na kuzikwa kwenye makaburi ya wazee wake, katika mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama kutoka Amoni, na Abiyamu mwanawe akatawala mahali pake.
1 Wafalme 14:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku zile akaugua Abiya, mwana wa Yeroboamu. Yeroboamu akamwambia mkewe, Ondoka, tafadhali, ujibadilishe, wasikujue kuwa mkewe Yeroboamu; ukaende Shilo; tazama, yuko huko Ahiya nabii, aliyeninena mimi ya kwamba nitakuwa mfalme juu ya watu hawa. Twaa mkononi mikate kumi, na kaki, na mtungi wa asali, ukamwendee; naye atakuambia kijana atakuwaje. Akafanya hivi mkewe Yeroboamu, akaondoka, akaenda Shilo, akaja nyumbani kwa Ahiya. Basi Ahiya hakuweza kuona; kwa kuwa macho yake yamepofuka kwa sababu ya uzee wake. BWANA akamwambia Ahiya, Angalia, mkewe Yeroboamu anakuja akuulize mambo ya mwanawe; kwa maana ni mgonjwa; umwambie hivi na hivi; kwani itakuwa akiingia atajifanya kuwa mwanamke mwingine. Ikawa, Ahiya alipoisikia sauti ya miguu yake, akiingia mlangoni, alisema, Karibu, mkewe Yeroboamu; mbona wajifanya kuwa mwingine maana nimetumwa kwako wewe, mwenye maneno mazito. Nenda, umwambie Yeroboamu, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa nilikutukuza miongoni mwa watu, nikakufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli, nikaurarulia mbali ufalme utoke nyumba yake Daudi, na kukupa wewe; lakini wewe hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, aliyezishika amri zangu, na kunifuata kwa moyo wake wote, asifanye lolote ila yaliyo mema machoni pangu; lakini umekosa kuliko wote waliokutangulia, umekwenda kujifanyia miungu mingine, na sanamu zilizoyeyuka, unikasirishe, na kunitupa nyuma yako; tazama, kwa hiyo mimi nitaleta mabaya juu ya nyumba yake Yeroboamu, nami nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli, nami kuondoa nitawaondoa waliobaki wa nyumba yake Yeroboamu, kama mtu aondoavyo mavi, hata itakapokwisha pia. Yeye afaye wa Yeroboamu mjini mbwa watamla; afaye mashambani ndege wa angani watamla; kwa kuwa BWANA amelinena hilo. Basi ondoka, urudi nyumbani kwako; na miguu yako itakapoingia mjini huyo kijana atakufa. Na Israeli wote watamlilia, na kumzika, kwa maana ndiye peke yake wa Yeroboamu atakayeingia kaburini; kwa sababu limeonekana ndani yake jambo lililo jema kwa BWANA, Mungu wa Israeli, nyumbani mwa Yeroboamu. Tena Bwana atajiinulia mfalme wa Israeli atakayeiharibu nyumba ya Yeroboamu siku ile; na nini tena hata sasa? Kwa kuwa BWANA atawapiga Israeli kama manyasi yatikiswavyo majini; naye atawang'oa Israeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, naye atawatawanya ng'ambo ya Mto; kwa sababu wamejitengenezea Maashera yao, wakimkasirisha BWANA. Naye atawatoa Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu, aliyoyakosa, ambayo kwa hayo amewakosesha Israeli. Basi mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda zake, akafika Tirza; naye alipofika kizingitini kwa nyumba, huyo kijana akafa. Israeli wote wakamzika, wakamlilia; sawasawa na neno la BWANA, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Ahiya nabii. Na mambo yake Yeroboamu yaliyosalia, ya kupigana na ya kutawala, tazama, yameandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli. Na siku alizotawala Yeroboamu zilikuwa miaka ishirini na miwili; akalala na babaze, naye Nadabu mwanawe akatawala mahali pake. Naye Rehoboamu mwana wa Sulemani akatawala katika Yuda. Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arubaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua BWANA miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Basi Yuda wakafanya maovu machoni pa BWANA; wakamtia wivu, kwa makosa yao waliyoyakosa, kuliko yote waliyoyafanya baba zao. Maana hao pia wakajijengea mahali pa juu, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Na mahanithi walikuwako katika nchi, wakafanya sawasawa na machukizo yote ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Ikawa, mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu; akazichukua hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao zote za dhahabu alizozifanya Sulemani. Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme. Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa BWANA, hao walinzi walizichukua; wakazirudisha tena katika chumba cha walinzi. Na mambo yake Rehoboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote. Rehoboamu akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Na mwanawe, Abiya, alitawala mahali pake.
1 Wafalme 14:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku zile akaugua Abiya, mwana wa Yeroboamu. Yeroboamu akamwambia mkewe, Ondoka, tafadhali, ujibadilishe, wasikujue kuwa mkewe Yeroboamu; ukaende Shilo; tazama, yuko huko Ahiya nabii, aliyeninena mimi ya kwamba nitakuwa mfalme juu ya watu hawa. Twaa mkononi mikate kumi, na kaki, na mtungi wa asali, ukamwendee; naye atakuambia kijana atakuwaje. Akafanya hivi mkewe Yeroboamu, akaondoka, akaenda Shilo, akaja nyumbani kwa Ahiya. Basi Ahiya hakuweza kuona; kwa kuwa macho yake yamepofuka kwa sababu ya uzee wake. BWANA akamwambia Ahiya, Angalia, mkewe Yeroboamu anakuja akuulize mambo ya mwanawe; kwa maana hawezi; hivi na hivi umwambie; kwani itakuwa akiingia atajifanya kuwa mwanamke mwingine. Ikawa, Ahiya alipoisikia sauti ya miguu yake, akiingia mlangoni, alisema, Karibu, mkewe Yeroboamu; mbona wajifanya kuwa mwingine maana nimetumwa kwako wewe, mwenye maneno mazito. Nenda, umwambie Yeroboamu, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa nilikutukuza miongoni mwa watu, nikakufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli, nikaurarulia mbali ufalme utoke nyumba yake Daudi, na kukupa wewe; walakini wewe hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, aliyezishika amri zangu, na kunifuata kwa moyo wake wote, asifanye lo lote ila yaliyo mema machoni pangu; lakini umekosa kuliko wote waliokutangulia, umekwenda kujifanyia miungu mingine, na sanamu zilizoyeyuka, unikasirishe, na kunitupa nyuma yako; tazama, kwa hiyo mimi nitaleta mabaya juu ya nyumba yake Yeroboamu, nami nitamkatia Yeroboamu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli, nami kuondoa nitawaondoa waliobaki wa nyumba yake Yeroboamu, kama mtu aondoavyo mavi, hata itakapokwisha pia. Yeye afaye wa Yeroboamu mjini mbwa watamla; afaye mashambani ndege wa angani watamla; kwa kuwa BWANA amelinena hilo. Basi ondoka, urudi nyumbani kwako; na miguu yako itakapoingia mjini huyo kijana atakufa. Na Israeli wote watamlilia, na kumzika, kwa maana ndiye peke yake wa Yeroboamu atakayeingia kaburini; kwa sababu limeonekana ndani yake jambo lililo jema kwa BWANA, Mungu wa Israeli, nyumbani mwa Yeroboamu. Tena Bwana atajiinulia mfalme wa Israeli atakayeiharibu nyumba ya Yeroboamu siku ile; na nini tena hata sasa? Kwa kuwa BWANA atawapiga Israeli kama manyasi yatikiswavyo majini; naye atawang’oa Israeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, naye atawatawanya ng’ambo ya Mto; kwa sababu wamejifanyia maashera yao, wakimkasirisha BWANA. Naye atawatoa Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu, aliyoyakosa, ambayo kwa hayo amewakosesha Israeli. Basi mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda zake, akafika Tirza; naye alipofika kizingitini kwa nyumba, huyo kijana akafa. Israeli wote wakamzika, wakamlilia; sawasawa na neno la BWANA, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Ahiya nabii. Na mambo yake Yeroboamu yaliyosalia, ya kupigana na ya kutawala, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli. Na siku alizotawala Yeroboamu zilikuwa miaka ishirini na miwili; akalala na babaze, naye Nadabu mwanawe akatawala mahali pake. Naye Rehoboamu mwana wa Sulemani akatawala katika Yuda. Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arobaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua BWANA miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Basi Yuda wakafanya maovu machoni pa BWANA; wakamtia wivu, kwa makosa yao waliyoyakosa, kuliko yote waliyoyafanya baba zao. Maana hao pia wakajijengea mahali pa juu, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Na mahanithi walikuwako katika nchi, wakafanya sawasawa na machukizo yote ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Ikawa, mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu; akazichukua hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao zote za dhahabu alizozifanya Sulemani. Mfalme Rehoboamu akafanya ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme. Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa BWANA, hao walinzi walizichukua; wakazirudisha tena katika chumba cha walinzi. Na mambo yake Rehoboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote. Rehoboamu akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Na mwanawe, Abiya, alitawala mahali pake.
1 Wafalme 14:1-31 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati ule Abiya mwana wa Yeroboamu akaugua, naye Yeroboamu akamwambia mke wake, “Nenda ukajibadilishe, ili watu wasijue kwamba wewe ni mke wa Yeroboamu. Kisha uende Shilo. Nabii Ahiya yuko huko, yule aliyeniambia kuwa nitakuwa mfalme juu ya watu hawa. Chukua mikate kumi, maandazi kadhaa na gudulia la asali na umwendee. Atakuambia kitakachotokea kwa kijana.” Basi mke wa Yeroboamu akafanya kama alivyosema mumewe, akaenda kwenye nyumba ya Ahiya huko Shilo. Wakati huu Ahiya alikuwa kipofu naye alishindwa kuona kwa sababu ya umri wake. Lakini BWANA alikuwa amemwambia Ahiya, “Mke wa Yeroboamu anakuja kukuuliza kuhusu mwanawe, kwa kuwa ni mgonjwa, nawe utamjibu hivi na hivi. Atakapowasili, atajifanya kuwa ni mtu mwingine.” Hivyo Ahiya aliposikia kishindo cha hatua zake mlangoni, akasema, “Karibu ndani, mke wa Yeroboamu. Kwa nini kujibadilisha? Nimetumwa kwako nikiwa na habari mbaya. Nenda, ukamwambie Yeroboamu kwamba hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli: ‘Nilikuinua miongoni mwa watu na kukufanya kiongozi juu ya watu wangu Israeli. Nikararua ufalme kutoka kwa nyumba ya Daudi na kukupa wewe, lakini hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye aliyashika maagizo yangu na kunifuata kwa moyo wake wote, akifanya tu lile lililokuwa sawa machoni pangu. Umefanya maovu mengi kuliko wote waliokutangulia. Umejitengenezea miungu mingine, sanamu za chuma, umenighadhibisha na kunitupa nyuma yako. “ ‘Kwa sababu ya hili, nitaleta maafa juu ya nyumba ya Yeroboamu. Nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, mtumwa au mtu huru. Nitachoma nyumba ya Yeroboamu mpaka iteketee yote kama mtu achomaye kinyesi. Mbwa watawala wale walio wa nyumba ya Yeroboamu watakaofia ndani ya mji na ndege wa angani watajilisha kwa wale watakaofia mashambani. BWANA amesema!’ “Kukuhusu wewe, rudi nyumbani. Wakati utakapotia mguu katika mji wako, kijana atakufa. Israeli yote itamwombolezea na kumzika. Kwa sababu ni yeye pekee wa nyumba ya Yeroboamu atakayezikwa, kwa sababu ni yeye peke yake ndani ya nyumba ya Yeroboamu ambaye BWANA, Mungu wa Israeli, ameona kitu chema kwake. “BWANA atajiinulia mwenyewe mfalme juu ya Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Siku ndiyo hii! Nini? Naam, hata sasa hivi. Naye BWANA ataipiga Israeli, hata iwe kama unyasi unaosukwasukwa juu ya maji. Ataingʼoa Israeli kutoka nchi hii nzuri aliyowapa baba zao na kuwatawanya ngʼambo ya Mto Frati, kwa sababu wamemghadhibisha BWANA kwa kutengeneza nguzo za Ashera Naye atawaacha Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu aliyoyatenda na kusababisha Israeli kuyatenda.” Kisha mke wa Yeroboamu akainuka, akaondoka kwenda Tirsa. Mara alipokanyaga kizingiti cha mlango, kijana akafa. Wakamzika na Israeli yote ikamwombolezea, kama BWANA alivyokuwa amesema kupitia mtumishi wake, nabii Ahiya. Matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, vita vyake na jinsi alivyotawala, vimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. Yeroboamu akawatawala kwa miaka ishirini na miwili, kisha akalala na baba zake. Naye Nadabu mwanawe akawa mfalme baada yake. Rehoboamu mwana wa Solomoni alikuwa mfalme wa Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji ambao BWANA alikuwa ameuchagua kutoka makabila yote ya Israeli ili apate kuliweka humo Jina lake. Mama yake aliitwa Naama, ambaye alikuwa Mwamoni. Yuda wakatenda maovu machoni pa BWANA. Kwa dhambi walizotenda wakachochea hasira yake yenye wivu zaidi kuliko baba zao walivyofanya. Pia wakajijengea mahali pa juu pa kuabudia miungu, mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kilichoinuka na kila mti uliotanda. Walikuwepo hata wanaume mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu katika nchi; watu wakajiingiza katika kutenda machukizo ya mataifa ambayo BWANA aliyafukuza mbele ya Waisraeli. Katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu. Akachukua hazina za Hekalu la BWANA na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao zote za dhahabu ambazo Solomoni alikuwa amezitengeneza. Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme. Kila wakati mfalme alipokwenda katika Hekalu la BWANA, walinzi walizichukua hizo ngao, na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi. Kwa matukio mengine ya utawala wa Rehoboamu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita vinavyoendelea kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. Naye Rehoboamu akalala na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama, ambaye alikuwa Mwamoni. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.