1 Wafalme 14:1-31
1 Wafalme 14:1-31 BHN
Wakati huo, Abiya mwana wa mfalme Yeroboamu, akawa mgonjwa. Yeroboamu akamwambia mkewe, “Jisingizie kuwa mwingine, uende mjini Shilo anakokaa nabii Ahiya aliyesema kwamba mimi nitakuwa mfalme wa Israeli. Mpelekee mikate kumi, maandazi kadha, na asali chupa moja. Yeye atakuambia yatakayompata mtoto wetu.” Basi, mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda Shilo nyumbani kwa Ahiya. Wakati huo, Ahiya alikuwa hawezi tena kuona sawasawa kwa sababu ya uzee. Mwenyezi-Mungu alikuwa amekwisha mwambia Ahiya kwamba mke wa Yeroboamu alikuwa njiani, anakuja kumwuliza yatakayompata mwanawe mgonjwa, na jinsi atakavyomjibu. Mkewe Yeroboamu alipofika, alijisingizia kuwa mtu mwingine. Lakini Ahiya alipomsikia anaingia mlangoni, alisema, “Karibu ndani mke wa Yeroboamu. Lakini mbona unajisingizia kuwa mtu mwingine? Ninao ujumbe usio mzuri kwako! Nenda ukamwambie Yeroboamu kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Nilikuteua miongoni mwa watu, nikakufanya kuwa kiongozi wa watu wangu, Israeli; nikaurarua ufalme utoke kwa wazawa wa Daudi, nikakupa wewe. Lakini wewe ni kinyume kabisa cha mtumishi wangu Daudi ambaye alizishika amri zangu, akafuata matakwa yangu kwa moyo wake wote na kutenda tu yaliyo sawa mbele ya macho yangu. Wewe umetenda uovu mbaya zaidi kuliko waliotenda wale waliokutangulia; wewe umenikasirisha kwa kujitengenezea miungu mingine na sanamu za kufua, kisha umeniacha. Haya basi, sasa nitailetea balaa jamaa hii yake, Yeroboamu, nitawaua wanaume wote wa jamaa zake katika Israeli, awe mtumwa au huru. Jamaa wake wote nitawateketeza kama mtu ateketezavyo mavi, mpaka yatoweke. Yeyote aliye wa jamaa ya Yeroboamu atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.’” Ahiya akamwambia mkewe Yeroboamu, “Haya inuka, uende zako nyumbani. Mara tu utakapoingia mjini, mwanao atakufa. Watu wote wa Israeli watafanya matanga na kumzika. Walakini, ni huyo tu wa jamaa ya Yeroboamu atakayezikwa, kwani ni yeye tu wa jamaa ya Yeroboamu aliyepata kumpendeza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Tena leo hii, Mwenyezi-Mungu ataweka mfalme mwingine katika Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Naam, tangu sasa, Mwenyezi-Mungu atawapiga watu wa Israeli, nao watatikisika kama unyasi unavyotikiswa mtoni. Atawangoa kutoka nchi hii nzuri aliyowapa babu zao, na kuwatawanya mbali, ngambo ya mto Eufrate, kwa sababu wamemkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa kujitengenezea sanamu za Ashera, mungu wa kike. Mwenyezi-Mungu ataitupa Israeli kwa sababu ya dhambi alizotenda Yeroboamu, na kuwafanya watu wa Israeli pia watende dhambi.” Hapo, mkewe Yeroboamu akaondoka, akashika safari mpaka Tirza. Mara tu alipofika mlangoni, mtoto akafa. Watu wote wa Israeli wakamzika na kufanya matanga kama alivyosema Mwenyezi-Mungu, kwa njia ya nabii Ahiya, mtumishi wake. Matendo mengine ya mfalme Yeroboamu, jinsi alivyopigana vita na alivyotawala, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Yeroboamu alitawala kwa muda wa miaka ishirini na miwili, halafu akafariki, na Nadabu, mwanawe, akatawala mahali pake. Rehoboamu, mwanawe Solomoni, alikuwa na umri wa miaka arubaini na mmoja alipoanza kutawala Yuda. Naye alitawala kwa muda wa miaka kumi na saba katika Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi-Mungu aliuchagua miongoni mwa miji ya makabila yote ya Israeli aabudiwe humo. Mama yake Rehoboamu alikuwa Naama kutoka Amoni. Watu wa Yuda walitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha kwa dhambi zao walizotenda, nyingi kuliko za babu zao. Walijitengenezea pia mahali pa ibada, minara ya kutambikia, na sanamu za Ashera, juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Tena, kukawa na ibada za ukahaba nchini; watu walitenda matendo ya kuchukiza ya mataifa ambayo Mungu aliyafukuza Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini Kanaani. Katika mwaka wa tano wa utawala wa Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri, aliushambulia mji wa Yerusalemu, akaichukua hazina yote ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya ikulu; alichukua kila kitu; pia alichukua ngao zote za dhahabu alizozitengeneza Solomoni. Badala ya ngao hizo, mfalme Rehoboamu alitengeneza ngao za shaba na kuziweka chini ya ulinzi wa wangojamlango wa ikulu. Kila wakati mfalme alipokwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walinzi walizibeba ngao hizo, na baadaye wakazirudisha katika chumba cha ulinzi. Matendo mengine ya mfalme Rehoboamu, na yote aliyoyafanya, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Daima kulikuwako vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. Hatimaye, Rehoboamu alifariki na kuzikwa kwenye makaburi ya wazee wake, katika mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama kutoka Amoni, na Abiyamu mwanawe akatawala mahali pake.