1 Wakorintho 10:1-13
1 Wakorintho 10:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, nataka mjue kwamba babu zetu wote walikuwa chini ya ulinzi wa lile wingu, na kwamba wote walivuka salama ile bahari. Wote walibatizwa katika umoja na Mose katika lile wingu na katika ile bahari. Wote walikula chakula kilekile cha kiroho, wakanywa pia kinywaji kilekile cha kiroho, maana walikunywa kutoka ule mwamba wa kiroho uliowafuata; mwamba huo ulikuwa Kristo mwenyewe. Hata hivyo, wengi wao hawakumpendeza Mungu, na maiti zao zilisambazwa jangwani. Sasa, mambo hayo yote ni mfano tu kwetu; yanatuonya sisi tusitamani ubaya kama wao walivyotamani. Msiwe waabudu sanamu kama baadhi yao walivyokuwa; kama yasemavyo Maandiko: “Watu waliketi kula na kunywa, wakasimama kucheza.” Wala tusizini kama baadhi yao walivyozini, wakaangamia siku moja watu 23,000. Tusimjaribu Bwana kama baadhi yao walivyomjaribu, wakauawa na nyoka. Wala msinungunike kama baadhi yao walivyonungunika, wakaangamizwa na Mwangamizi! Basi, mambo hayo yaliyowapata wao ni kielelezo kwa wengine, na yaliandikwa ili kutuonya sisi ambao mwisho wa nyakati unatukabili. Anayedhani amesimama imara ajihadhari asianguke. Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.
1 Wakorintho 10:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze. Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu elfu ishirini na tatu. Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakauawa na nyoka. Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakauawa na mharibifu. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiwa na miisho ya nyakati. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke. Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita muwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili muweze kustahimili.
1 Wakorintho 10:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze. Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu. Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka. Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke. Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.
1 Wakorintho 10:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndugu zangu, sitaki mkose kufahamu ukweli huu kwamba baba zetu walikuwa wote chini ya wingu na kwamba wote walipita katikati ya bahari. Wote wakabatizwa kuwa wa Mose ndani ya lile wingu na ndani ya ile bahari. Wote walikula chakula kile kile cha roho, na wote wakanywa kile kile kinywaji cha roho, kwa maana walikunywa kutoka ule mwamba wa roho uliofuatana nao, nao ule mwamba ulikuwa Kristo. Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, kwa hiyo miili yao ilitapakaa jangwani. Basi mambo haya yalitokea kama mifano ili kutuzuia tusiweke mioyo yetu katika mambo maovu kama wao walivyofanya. Msiwe waabudu sanamu, kama baadhi yao walivyokuwa, kama ilivyoandikwa, “Watu waliketi chini kula na kunywa, kisha wakainuka kucheza na kufanya sherehe za kipagani.” Wala tusifanye uzinzi kama baadhi yao walivyofanya, wakafa watu 23,000 kwa siku moja. Wala tusimjaribu Kristo, kama baadhi yao walivyofanya, wakafa kwa kuumwa na nyoka. Msinungʼunike kama baadhi yao walivyofanya, wakaangamizwa na mharabu. Mambo haya yote yaliwapata wao ili yawe mifano kwa wengine, nayo yaliandikwa ili yatuonye sisi ambao mwisho wa nyakati umetufikia. Hivyo, yeye ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke. Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.