1 Wakorintho 10:1-13
1 Wakorintho 10:1-13 BHN
Ndugu, nataka mjue kwamba babu zetu wote walikuwa chini ya ulinzi wa lile wingu, na kwamba wote walivuka salama ile bahari. Wote walibatizwa katika umoja na Mose katika lile wingu na katika ile bahari. Wote walikula chakula kilekile cha kiroho, wakanywa pia kinywaji kilekile cha kiroho, maana walikunywa kutoka ule mwamba wa kiroho uliowafuata; mwamba huo ulikuwa Kristo mwenyewe. Hata hivyo, wengi wao hawakumpendeza Mungu, na maiti zao zilisambazwa jangwani. Sasa, mambo hayo yote ni mfano tu kwetu; yanatuonya sisi tusitamani ubaya kama wao walivyotamani. Msiwe waabudu sanamu kama baadhi yao walivyokuwa; kama yasemavyo Maandiko: “Watu waliketi kula na kunywa, wakasimama kucheza.” Wala tusizini kama baadhi yao walivyozini, wakaangamia siku moja watu 23,000. Tusimjaribu Bwana kama baadhi yao walivyomjaribu, wakauawa na nyoka. Wala msinungunike kama baadhi yao walivyonungunika, wakaangamizwa na Mwangamizi! Basi, mambo hayo yaliyowapata wao ni kielelezo kwa wengine, na yaliandikwa ili kutuonya sisi ambao mwisho wa nyakati unatukabili. Anayedhani amesimama imara ajihadhari asianguke. Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.