Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 16:8-43

1 Mambo ya Nyakati 16:8-43 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; Wajulisheni watu matendo yake. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi; Zitafakarini ajabu zake zote. Jisifuni kwa jina lake takatifu; Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA. Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote. Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya; Miujiza yake na hukumu za kinywa chake; Enyi wazao wa Israeli, mtumishi wake, Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake. Likumbukeni agano lake milele, Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. Agano alilofanya na Ibrahimu, Na uapo wake kwa Isaka; Alilomthibitishia Yakobo kuwa amri, Na Israeli liwe agano la milele. Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Iwe urithi wenu mliopimiwa; Mlipokuwa watu wawezao kuhesabiwa; Naam, watu wachache na wageni ndani yake. Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa, Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine. Hakumwacha mtu awaonee; Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao; Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu. Mwimbieni BWANA, nchi yote; Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake. Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kusifiwa sana; Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote. Maana miungu yote ya watu si kitu; Lakini BWANA ndiye aliyezifanya mbingu. Heshima na adhama ziko mbele zake; Nguvu na furaha zipo mahali pake. Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Leteni sadaka, mje mbele zake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu; Tetemekeni mbele zake, nchi yote. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike; Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie; Na waseme katika mataifa, BWANA ametamalaki; Bahari na ivume na vyote viijazavyo; Mashamba na yashangilie na vyote vilivyomo; Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha, Mbele za BWANA, Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Nanyi mkaseme, Ee Mungu wa wokovu wetu, utuokoe, Utukusanye kwa kututoa katika mataifa, Tulishukuru jina lako takatifu, Tuzifanyie shangwe sifa zako. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, tangu milele hata milele. Na watu wote wakasema, Amina; wakamhimidi BWANA. Basi akawaacha huko, mbele ya sanduku la agano la BWANA, Asafu na nduguze, ili watumike mbele ya sanduku daima, kila siku kama ilivyokuwa kazi yake. Naye Obed-edomu, pamoja na ndugu zao, sitini na wanane; Obed-edomu na mwana wa Yeduthuni, na Hosa, wawe mabawabu; na Sadoki kuhani, na nduguze makuhani, mbele ya maskani ya BWANA katika mahali pa juu palipokuwa huko Gibeoni, ili kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa daima asubuhi na jioni, naam, sawasawa na yote yaliyoandikwa katika torati ya BWANA, aliyowaamuru Israeli; na pamoja nao Hemani na Yeduthuni, na wale wengine waliochaguliwa, waliotajwa majina yao, ili kumshukuru BWANA, kwa kuwa fadhili zake ni za milele; na pamoja nao Hemani na Yeduthuni wenye baragumu na matoazi, kwa hao watakaovumisha sauti, na vinanda kwa ajili ya hizo nyimbo za Mungu; na hao wana wa Yeduthuni wawepo mlangoni. Kisha watu wote wakaenda zao kila mtu nyumbani kwake; naye Daudi akarudi ili awabariki watu wa nyumbani mwake.

1 Mambo ya Nyakati 16:8-43 Biblia Habari Njema (BHN)

Mpeni shukrani Mwenyezi-Mungu, tangazeni ukuu wake, yajulisheni mataifa mambo aliyoyatenda! Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa; simulieni matendo yake ya ajabu! Jisifieni jina lake takatifu; wenye kumcha Mwenyezi-Mungu na wafurahi. Mwendeeni Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu; mwendeeni Mwenyezi-Mungu daima. Kumbukeni matendo ya ajabu aliyotenda, maajabu yake na hukumu alizotoa, enyi wazawa wa Abrahamu, mtumishi wake, enyi wazawa wa Yakobo, wateule wake. Yeye Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu; hukumu zake zina nguvu duniani kote. Yeye hulishika agano lake milele, hutimiza ahadi zake kwa vizazi elfu. Hushika agano alilofanya na Abrahamu, na ahadi aliyomwapia Isaka. Alimthibitishia Yakobo ahadi yake, akamhakikishia agano hilo la milele. Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani, nayo itakuwa mali yenu wenyewe.” Idadi yenu ilikuwa ndogo, mlikuwa wachache na wageni katika nchi ya Kanaani, mkitangatanga toka taifa hadi taifa, kutoka nchi moja hadi nchi nyingine, Mungu hakumruhusu mtu yeyote awadhulumu; kwa ajili yao aliwaonya wafalme: “Msiwaguse wateule wangu; msiwadhuru manabii wangu!” Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote. Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu. Yatangazieni mataifa utukufu wake, waambieni watu wote matendo yake ya ajabu. Maana Mwenyezi-Mungu ni mkuu, anasifika sana anastahili kuheshimiwa kuliko miungu yote. Miungu yote ya mataifa mengine si kitu; lakini Mwenyezi-Mungu aliziumba mbingu. Utukufu na fahari vyamzunguka, nguvu na furaha vyajaza hekalu lake. Mpeni Mwenyezi-Mungu, heshima enyi jamii zote za watu, naam, kirini utukufu na nguvu yake. Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima ya utukufu wa jina lake; leteni tambiko na kuingia nyumbani mwake. Mwabuduni Mwenyezi-Mungu patakatifuni pake. Ee dunia yote; tetemeka mbele yake! Ameuweka ulimwengu imara, hautatikisika. Furahini enyi mbingu na dunia! Yaambieni mataifa, “Mwenyezi-Mungu anatawala!” Bahari na ivume, pamoja na vyote vilivyomo! Furahini enyi mashamba na vyote vilivyomo! Ndipo miti yote msituni itaimba kwa furaha mbele ya Mwenyezi-Mungu anayekuja naam, anayekuja kuihukumu dunia. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele! Mwambieni Mwenyezi-Mungu: Utuokoe, ee Mungu wa wokovu wetu, utukusanye pamoja na kutuokoa kutoka kwa mataifa, tupate kulisifu jina lako takatifu, kuona fahari juu ya sifa zako. Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele! Kisha watu wote wakasema, “Amina!” Pia wakamsifu Mwenyezi-Mungu. Hivyo, mfalme Daudi akawaacha Asafu na nduguze Walawi mahali walipoliweka sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya huduma zinazotakiwa mbele ya sanduku kila siku. Obed-edomu, mwana wa Yeduthuni, pamoja na wenzake sitini na wanane waliwasaidia. Obed-edomu mwana wa Yeduthuni na Hosa walikuwa walinzi wa malango. Mfalme Daudi akawaweka kuhani Sadoki na makuhani wenzake kuwa wahudumu wa hema ya Mwenyezi-Mungu iliyokuwa mahali pa kuabudu huko Gibeoni ili kutolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka za kuteketezwa daima asubuhi na jioni, kulingana na yote yaliyoandikwa katika sheria ya Mwenyezi-Mungu aliyowaamuru Waisraeli. Pamoja nao walikuwa Hemani na Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa, waliotajwa majina yao, ili kumshukuru Mwenyezi-Mungu kwa kuwa fadhili zake ni za milele. Hemani na Yeduthuni walikuwa na tarumbeta na matoazi kwa ajili ya muziki na ala za muziki kwa ajili ya nyimbo takatifu. Wana wa Yeduthuni walichaguliwa kuyalinda malango. Kisha, kila mtu aliondoka kwenda nyumbani kwake; naye Daudi akaenda nyumbani kwake kuibariki jamaa yake.

1 Mambo ya Nyakati 16:8-43 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; Wajulisheni watu matendo yake. Mwimbieni, mwimbieni nyimbo za kumsifu; Yatangazeni matendo yake yote ya ajabu. Jisifuni kwa jina lake takatifu; Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA. Mtafuteni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote. Yakumbukeni matendo yake yote ya ajabu aliyoyafanya; Miujiza yake na hukumu za kinywa chake; Enyi wazao wa Israeli, mtumishi wake, Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu; Duniani kote kuna hukumu zake. Likumbukeni agano lake milele, Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. Agano alilofanya na Abrahamu, Na kiapo chake kwa Isaka; Aliyomthibitishia Yakobo kuwa amri, Na kwa Israeli kuwa agano la milele. Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Iwe urithi wenu mliopimiwa; Mlipokuwa watu wawezao kuhesabiwa; Naam, watu wachache na wageni ndani yake. Mkitangatanga toka taifa hadi taifa, Toka ufalme mmoja hadi kwa watu wengine. Hakumwacha mtu awaonee; Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao; Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu. Mwimbieni BWANA, nchi yote; Tangazeni wokovu wake siku baada ya siku. Watangazieni mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake. Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kusifiwa sana; Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote. Maana miungu yote ya watu si kitu; Lakini BWANA ndiye aliyezifanya mbingu. Heshima na adhama ziko mbele zake; Nguvu na furaha zipo mahali pake. Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Leteni sadaka, na mje mbele zake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu; Tetemekeni mbele zake, nchi yote. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike; Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie; Na waseme katika mataifa, BWANA ametamalaki; Bahari na ivume na vyote viijazavyo; Mashamba na yashangilie na vyote vilivyomo; Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha, Mbele za BWANA, Kwa maana anakuja kuihukumu nchi. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Nanyi semeni, Ee Mungu wa wokovu wetu, utuokoe, Utukusanye kwa kututoa katika mataifa, Tulishukuru jina lako takatifu, Tuzifanyie shangwe sifa zako. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, tangu milele hata milele. Na watu wote wakasema, Amina; wakamhimidi BWANA. Basi akawaacha huko, mbele ya sanduku la Agano la BWANA, Asafu na nduguze, ili watumike mbele ya sanduku daima, kila siku kama ilivyokuwa kazi yake. Naye Obed-edomu, pamoja na ndugu zao, sitini na wanane; Obed-edomu na mwana wa Yeduthuni, na Hosa, wawe mabawabu; na Sadoki kuhani, na nduguze makuhani, mbele ya maskani ya BWANA katika mahali pa juu palipokuwa huko Gibeoni, ili kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa daima asubuhi na jioni, naam, kulingana na yote yaliyoandikwa katika Torati ya BWANA, aliyowaamuru Israeli; na pamoja nao Hemani na Yeduthuni, na wale wengine waliochaguliwa, waliotajwa majina yao, ili kumshukuru BWANA, kwa kuwa fadhili zake ni za milele; na pamoja nao Hemani na Yeduthuni wenye baragumu na matoazi, kwa hao watakaovumisha sauti, na vinanda kwa ajili ya hizo nyimbo za Mungu; na hao wana wa Yeduthuni wawepo mlangoni. Kisha watu wote wakaenda zao kila mtu nyumbani kwake; naye Daudi akarudi ili awabariki watu wa nyumbani mwake.

1 Mambo ya Nyakati 16:8-43 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda. Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa; waambieni matendo yake yote ya ajabu. Lishangilieni jina lake takatifu; mioyo ya wale wamtafutao BWANA na ifurahi. Mtafuteni BWANA na nguvu zake; utafuteni uso wake siku zote. Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya, miujiza yake na hukumu alizozitamka, enyi wazao wa Israeli mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye ndiye BWANA Mungu wetu; hukumu zake zimo duniani pote. Hulikumbuka agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu, agano alilolifanya na Abrahamu, kiapo alichomwapia Isaki. Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri, kwa Israeli liwe agano la milele: “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani kuwa sehemu utakayoirithi.” Walipokuwa wachache kwa idadi, wachache sana na wageni ndani yake, walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine, kutoka ufalme mmoja hadi mwingine. Hakuruhusu mtu yeyote awaonee; kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema: “Msiwaguse niliowatia mafuta; msiwadhuru manabii wangu.” Mwimbieni BWANA dunia yote; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku. Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa, matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote. Kwa kuwa BWANA ni mkuu, mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote. Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini BWANA aliziumba mbingu. Fahari na enzi viko mbele yake; nguvu na utukufu vimo patakatifu pake. Mpeni BWANA, enyi jamaa za mataifa, mpeni BWANA utukufu na nguvu, mpeni BWANA utukufu unaostahili jina lake. Leteni sadaka na mje katika nyua zake; mwabuduni BWANA katika uzuri wa utakatifu wake. Dunia yote na itetemeke mbele zake! Ulimwengu ameuweka imara; hauwezi kusogezwa. Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; semeni katikati ya mataifa, “BWANA anatawala!” Bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake; mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo ndani yake. Kisha miti ya msituni itaimba, itaimba kwa furaha mbele za BWANA, kwa maana anakuja kuihukumu dunia. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele. Mlilieni, “Ee Mungu Mwokozi wetu, tuokoe. Tukusanye tena na utukomboe kutoka kwa mataifa, ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu, na kushangilia katika sifa zako.” Atukuzwe BWANA, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Nao watu wote wakasema, “Amen,” na “Msifuni BWANA.” Daudi akamwacha Asafu na wenzake mbele ya Sanduku la Agano la BWANA ili wahudumu humo mara kwa mara, kulingana na mahitaji ya kila siku. Pia akamwacha Obed-Edomu pamoja na wenzake sitini na wanane wahudumu pamoja nao. Obed-Edomu mwana wa Yeduthuni na pia Hosa walikuwa mabawabu wa lango. Daudi akamwacha kuhani Sadoki pamoja na makuhani wenzake mbele ya hema ya ibada ya BWANA katika mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni ili kutoa sadaka za kuteketezwa kwa BWANA kwenye madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mara kwa mara, asubuhi na jioni, sawasawa na kila kitu kilichoandikwa katika sheria ya BWANA ambayo alikuwa amempa Israeli. Waliohudumu pamoja nao walikuwa Hemani, Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa na kutajwa kwa jina kumpa BWANA shukrani, “Kwa maana fadhili zake zadumu milele.” Hemani na Yeduthuni walikuwa na wajibu wa kupiga tarumbeta, matoazi na kutumia vyombo vingine kwa ajili ya nyimbo za sifa kwa Mungu. Wana wa Yeduthuni waliwekwa langoni. Kisha watu wote wakaondoka, kila mmoja akarudi nyumbani kwake, naye Daudi akarudi nyumbani kuibariki jamaa yake.