1 Mambo ya Nyakati 16:37-43
1 Mambo ya Nyakati 16:37-43 Biblia Habari Njema (BHN)
Hivyo, mfalme Daudi akawaacha Asafu na nduguze Walawi mahali walipoliweka sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya huduma zinazotakiwa mbele ya sanduku kila siku. Obed-edomu, mwana wa Yeduthuni, pamoja na wenzake sitini na wanane waliwasaidia. Obed-edomu mwana wa Yeduthuni na Hosa walikuwa walinzi wa malango. Mfalme Daudi akawaweka kuhani Sadoki na makuhani wenzake kuwa wahudumu wa hema ya Mwenyezi-Mungu iliyokuwa mahali pa kuabudu huko Gibeoni ili kutolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka za kuteketezwa daima asubuhi na jioni, kulingana na yote yaliyoandikwa katika sheria ya Mwenyezi-Mungu aliyowaamuru Waisraeli. Pamoja nao walikuwa Hemani na Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa, waliotajwa majina yao, ili kumshukuru Mwenyezi-Mungu kwa kuwa fadhili zake ni za milele. Hemani na Yeduthuni walikuwa na tarumbeta na matoazi kwa ajili ya muziki na ala za muziki kwa ajili ya nyimbo takatifu. Wana wa Yeduthuni walichaguliwa kuyalinda malango. Kisha, kila mtu aliondoka kwenda nyumbani kwake; naye Daudi akaenda nyumbani kwake kuibariki jamaa yake.
1 Mambo ya Nyakati 16:37-43 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi akawaacha huko, mbele ya sanduku la Agano la BWANA, Asafu na nduguze, ili watumike mbele ya sanduku daima, kila siku kama ilivyokuwa kazi yake. Naye Obed-edomu, pamoja na ndugu zao, sitini na wanane; Obed-edomu na mwana wa Yeduthuni, na Hosa, wawe mabawabu; na Sadoki kuhani, na nduguze makuhani, mbele ya maskani ya BWANA katika mahali pa juu palipokuwa huko Gibeoni, ili kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa daima asubuhi na jioni, naam, kulingana na yote yaliyoandikwa katika Torati ya BWANA, aliyowaamuru Israeli; na pamoja nao Hemani na Yeduthuni, na wale wengine waliochaguliwa, waliotajwa majina yao, ili kumshukuru BWANA, kwa kuwa fadhili zake ni za milele; na pamoja nao Hemani na Yeduthuni wenye baragumu na matoazi, kwa hao watakaovumisha sauti, na vinanda kwa ajili ya hizo nyimbo za Mungu; na hao wana wa Yeduthuni wawepo mlangoni. Kisha watu wote wakaenda zao kila mtu nyumbani kwake; naye Daudi akarudi ili awabariki watu wa nyumbani mwake.
1 Mambo ya Nyakati 16:37-43 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi akawaacha huko, mbele ya sanduku la agano la BWANA, Asafu na nduguze, ili watumike mbele ya sanduku daima, kila siku kama ilivyokuwa kazi yake. Naye Obed-edomu, pamoja na ndugu zao, sitini na wanane; Obed-edomu na mwana wa Yeduthuni, na Hosa, wawe mabawabu; na Sadoki kuhani, na nduguze makuhani, mbele ya maskani ya BWANA katika mahali pa juu palipokuwa huko Gibeoni, ili kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa daima asubuhi na jioni, naam, sawasawa na yote yaliyoandikwa katika torati ya BWANA, aliyowaamuru Israeli; na pamoja nao Hemani na Yeduthuni, na wale wengine waliochaguliwa, waliotajwa majina yao, ili kumshukuru BWANA, kwa kuwa fadhili zake ni za milele; na pamoja nao Hemani na Yeduthuni wenye baragumu na matoazi, kwa hao watakaovumisha sauti, na vinanda kwa ajili ya hizo nyimbo za Mungu; na hao wana wa Yeduthuni wawepo mlangoni. Kisha watu wote wakaenda zao kila mtu nyumbani kwake; naye Daudi akarudi ili awabariki watu wa nyumbani mwake.
1 Mambo ya Nyakati 16:37-43 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Daudi akamwacha Asafu na wenzake mbele ya Sanduku la Agano la BWANA ili wahudumu humo mara kwa mara, kulingana na mahitaji ya kila siku. Pia akamwacha Obed-Edomu pamoja na wenzake sitini na wanane wahudumu pamoja nao. Obed-Edomu mwana wa Yeduthuni na pia Hosa walikuwa mabawabu wa lango. Daudi akamwacha kuhani Sadoki pamoja na makuhani wenzake mbele ya hema ya ibada ya BWANA katika mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni ili kutoa sadaka za kuteketezwa kwa BWANA kwenye madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mara kwa mara, asubuhi na jioni, sawasawa na kila kitu kilichoandikwa katika sheria ya BWANA ambayo alikuwa amempa Israeli. Waliohudumu pamoja nao walikuwa Hemani, Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa na kutajwa kwa jina kumpa BWANA shukrani, “Kwa maana fadhili zake zadumu milele.” Hemani na Yeduthuni walikuwa na wajibu wa kupiga tarumbeta, matoazi na kutumia vyombo vingine kwa ajili ya nyimbo za sifa kwa Mungu. Wana wa Yeduthuni waliwekwa langoni. Kisha watu wote wakaondoka, kila mmoja akarudi nyumbani kwake, naye Daudi akarudi nyumbani kuibariki jamaa yake.