Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 10

10
Mungu anaahidi ukombozi
1Mwombeni Mwenyezi-Mungu awape mvua za masika.
Mwenyezi-Mungu ndiye aletaye mawingu ya mvua;
ndiye awapaye watu mvua za rasharasha,
na kustawisha mimea shambani kwa ajili ya wote.
2Vinyago vyao vya kupigia ramli ni upuuzi mtupu,
na waaguzi wao wanaagua uongo;
watabiri wao wanatabiri ndoto za danganyifu,
na kuwapa watu faraja tupu.
Ndio maana watu wa Yuda wanatangatanga kama kondoo;
wanataabika kwa kuwa wamekosa mchungaji.
3Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nimewaka hasira dhidi ya hao wachungaji,
nami nitawaadhibu hao viongozi.#10:3 viongozi: Kiebrania: Beberu.
Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
nitalitunza kundi langu, ukoo wa Yuda.
Nitawafanya kuwa farasi wangu hodari wa vita.
4Kwa ukoo wa Yuda kutatokea:
Watawala wa kila namna,
viongozi imara kama jiwe kuu la msingi,
walio thabiti kama kigingi cha hema,
wenye nguvu kama upinde wa vita.
5Watu wa Yuda watakuwa kama mashujaa vitani
watawakanyaga maadui zao katika tope njiani.
Watapigana kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nipo pamoja nao;
nao watawaaibisha hata wapandafarasi.
6“Watu wa Yuda nitawaimarisha;
nitawaokoa wazawa wa Yosefu.
Nitawarejesha makwao kwa maana nawaonea huruma,
nao watakuwa kana kwamba sikuwa nimewakataa.
Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wao,
nami nitayasikiliza maombi yao.
7Watu wa Efraimu watakuwa kama mashujaa vitani;
watajaa furaha kama waliokunywa divai.
Watoto wao wataona hayo na kufurahi,
watajaa furaha mioyoni kwa sababu yangu Mwenyezi-Mungu.
8“Nitawaita watu wangu
na kuwakusanya pamoja;
nimekusudia kuwakomboa,
nao watakuwa wengi kama hapo awali.
9Japo niliwatawanya kati ya mataifa,
hata hivyo, watanikumbuka wakiwa humo.
Nao pamoja na watoto wao wataishi
na kurudi majumbani mwao.
10Nitawarudisha kutoka nchini Misri,
nitawakusanya kutoka Ashuru;
nitawaleta nchini Gileadi na Lebanoni,
nao watajaa kila mahali nchini.
11Watapitia katika bahari ya mateso,#10:11 mateso: Au Misri.
nami nitayapiga mawimbi yake,
na vilindi vya maji ya mto Nili vitakauka.
Kiburi cha Ashuru kitavunjwa
na nguvu za Misri zitatoweka.
12Mimi nitawaimarisha watu wangu,
nao watanitii na kuishi kwa kunipendeza.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Iliyochaguliwa sasa

Zekaria 10: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha