Tito 2
2
Mafundisho ya kweli
1Lakini wewe unapaswa kuhubiri mafundisho sahihi. 2Waambie wanaume wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu.
3Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema, 4ili wawazoezeshe kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto, 5wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa.
6Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi. 7Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako. 8Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili maadui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu.
9Watumwa wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao, 10au kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonesha kwamba wao ni wema na waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu ya Mungu, Mwokozi wetu.
11Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote. 12Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa, 13tukiwa tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo. 14#Taz Zab 130:8 Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema.
15Basi, sema mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau.
Iliyochaguliwa sasa
Tito 2: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.