Waroma 8:5-11
Waroma 8:5-11 BHN
Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho. Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uhai na amani. Maana, mwenye kutawaliwa na fikira za mwili ni adui wa Mungu; haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii. Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini nyinyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo. Lakini kama Kristo yumo ndani yenu, ingawa miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai kwa sababu mmefanywa kuwa waadilifu. Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu ataipa uhai miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.