Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waroma 13

13
Utii kwa viongozi wa nchi
1Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali; maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu. 2Anayepinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu; nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe. 3Maana, watawala hawasababishi hofu kwa watu wema, ila kwa watu wabaya. Basi, wataka usimwogope mtu mwenye mamlaka? Fanya mema naye atakusifu; 4maana yeye ni mtumishi wa Mungu anayefanya kazi kwa faida yako. Lakini ukifanya mabaya, basi, huna budi kumwogopa, maana anao kweli uwezo wa kuadhibu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, kuwaonesha ghadhabu yake wale watendao maovu. 5Kwa hiyo ni lazima kuwatii wenye mamlaka, si tu kwa sababu ya kuogopa ghadhabu ya Mungu, bali pia kwa sababu dhamiri inadai hivyo.
6Kwa sababu hiyohiyo nyinyi hulipa kodi; maana viongozi hao humtumikia Mungu ikiwa wanatimiza wajibu wao. 7Mpeni kila mtu haki yake; mtu wa ushuru, ushuru; wa kodi, kodi; na astahiliye heshima, heshima.
Kupendana kindugu
8Msiwe na deni kwa mtu yeyote, isipokuwa tu deni la kupendana. Ampendaye jirani yake ameitekeleza sheria. 9Maana, amri hizi: “Usizini; Usiue; Usitamani;” na nyingine zote, zimo katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” 10Ampendaye jirani yake hamtendei vibaya. Basi, upendo ni utimilifu wa sheria.
11Zaidi ya hayo, nyinyi mnajua tumo katika wakati gani: Sasa ndio wakati wa kuamka usingizini; naam, wokovu wetu uko karibu zaidi sasa kuliko wakati ule tulipoanza kuamini. 12Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga. 13Na tuishi kwa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana, na wala sio kwa ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugomvi na wivu. 14Bwana Yesu Kristo awe vazi lenu; msishughulikie tena tamaa zenu za maumbile na kuziridhisha.

Iliyochaguliwa sasa

Waroma 13: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia