Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waroma 10:1-15

Waroma 10:1-15 BHN

Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima. Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli. Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe na hivyo hawakuikubali njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu. Maana kwa kuja kwake Kristo, sheria imefikia kikomo chake, ili wote wanaoamini wafanywe waadilifu. Kuhusu kuwa mwadilifu kwa kuitii sheria, Mose aliandika hivi: “Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya sheria ataishi.” Lakini kuhusu kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: “Usiseme moyoni mwako: ‘Nani atapanda mpaka mbinguni?’ (yaani, kumleta Kristo chini); wala usiseme: ‘Nani atashuka mpaka kuzimu?’ (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu).” Maandiko Matakatifu yasema hivi: “Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako” nao ndio ile imani tunayoihubiri. Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Maana mtu huamini kwa moyo akafanywa mwadilifu; na hukiri kwa kinywa akaokolewa. Maandiko Matakatifu yasema: “Kila anayemwamini hataaibishwa.” Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.” Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!”

Video ya Waroma 10:1-15

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Waroma 10:1-15