Ufunuo 1:9-15
Ufunuo 1:9-15 BHN
Mimi ni Yohane, ndugu yenu, ambaye kwa kuungana na Yesu, nashiriki pamoja nanyi mateso na ufalme wake na uvumilivu thabiti. Mimi nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa sababu ya kuhubiri neno la Mungu na kumshuhudia Yesu. Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta. Nayo ilisema, “Andika katika kitabu yale unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamumu, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea.” Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu, na katikati yake kulikuwa na kitu kama Mwana wa Mtu, naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na mkanda wa dhahabu kifuani. Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba nyeupe, kama theluji; macho yake yalimetameta kama moto; miguu yake kama shaba iliyong'arishwa iliyosafishwa katika tanuri ya moto, na sauti yake ilikuwa kama sauti ya poromoko la maji.