Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 97:1-12

Zaburi 97:1-12 BHN

Mwenyezi-Mungu anatawala! Furahi, ee dunia! Furahini enyi visiwa vingi! Mawingu na giza nene vyamzunguka; uadilifu na haki ni msingi wa utawala wake. Moto watangulia mbele yake, na kuwateketeza maadui zake pande zote. Umeme wake wauangaza ulimwengu; dunia yauona na kutetemeka. Milima yayeyuka kama nta mbele ya Mwenyezi-Mungu; naam, mbele ya Bwana wa dunia yote. Mbingu zatangaza uadilifu wake; na mataifa yote yauona utukufu wake. Wote wanaoabudu sanamu wanaaibishwa, naam, wote wanaojisifia miungu duni; miungu yote husujudu mbele zake. Watu wa Siyoni wanafurahi; watu wa Yuda wanashangilia, kwa sababu ya hukumu zako, ee Mungu. Wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu juu ya dunia yote; wewe watukuka juu ya miungu yote. Mwenyezi-Mungu huwapenda wanaochukia uovu, huyalinda maisha ya watu wake; huwaokoa makuchani mwa waovu. Mwanga humwangazia mtu mwadilifu, na furaha kwa watu wanyofu wa moyo. Furahini kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu; mshukuruni kwa ajili ya jina lake takatifu.

Soma Zaburi 97