Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 69:1-36

Zaburi 69:1-36 BHN

Uniokoe, ee Mungu; maji yamenifika shingoni. Ninazama ndani ya matope makuu, hamna hata mahali pa kuweka miguu. Nimetumbukia kwenye kilindi cha maji, nachukuliwa na mawimbi. Niko hoi kwa kupiga yowe, na koo langu limekauka. Macho yangu yamefifia, nikikungojea ewe Mungu wangu. Watu wengi kuliko nywele zangu ndio wanichukiao bure. Wana nguvu sana hao wanaotaka kuniua, hao wanaonishambulia kwa mambo ya uongo. Je, nirudishe kitu ambacho sikuiba? Ee Mungu, waujua upumbavu wangu; makosa yangu hayakufichika kwako. Wanaokutumainia wasiaibishwe kwa sababu yangu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi; wanaokutafuta, wasione fedheha kwa sababu yangu ee Mungu wa Israeli. Kwa ajili yako nimefedheheshwa, aibu imefunika uso wangu. Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, kaka na dada zangu hawanitambui. Upendo wangu kwa nyumba yako unanimaliza. Kashfa zote wanazokutolea wewe zimenipata mimi. Nilipojinyenyekesha kwa kufunga, watu walinilaumu. Nilipovaa vazi la gunia kuomboleza, wao walinidharau. Watu wananisengenya mabarabarani; walevi wanatunga nyimbo juu yangu. Lakini mimi nakuomba wewe, ee Mwenyezi-Mungu; nikubalie ombi langu wakati unaopenda, ee Mungu. Kwa wingi wa fadhili zako unijibu. Wewe ni mkombozi wa kuaminika. Kwa msaada wako amini uniokoe nisizame katika matope; uniokoe na hao wanaonichukia, unisalimishe kutoka vilindi vya maji. Usiniache nikumbwe na mkondo wa maji, au nizame kwenye kilindi au nimezwe na kifo. Unijibu, ee Mwenyezi-Mungu, kwa wema na fadhili zako; unielekee kwa wingi wa huruma yako. Usimfiche mtumishi wako uso wako; unijibu haraka, maana niko hatarini. Unijie karibu na kunikomboa, uniokoe na maadui zangu wengi. Wewe wajua ninavyotukanwa, wajua aibu na kashfa ninazopata; na maadui zangu wote wewe wawajua. Kashfa zimeuvunja moyo wangu, nami nimekata tamaa. Nimetafuta kitulizo lakini sikupata, wa kunifariji lakini sikumpata. Walinipa sumu kuwa chakula, na nilipokuwa na kiu wakanipa siki. Karamu zao na ziwe mtego kwao, na sikukuu zao za sadaka ziwanase. Macho yao yatiwe giza wasiweze kuona, uitetemeshe daima migongo yao. Uwamwagie hasira yako, ghadhabu yako iwakumbe. Kambi zao ziachwe mahame, asiishi yeyote katika mahema yao. Maana wanawatesa wale uliowaadhibu, wanawaongezea majeraha wale uliowajeruhi. Uwaadhibu kwa kila uovu wao; uwakatalie kabisa msamaha wako. Uwafute katika kitabu cha walio hai, wasiwemo katika orodha ya waadilifu. Lakini mimi mnyonge na mgonjwa; uniinue juu, ee Mungu, uniokoe. Kwa wimbo nitalisifu jina la Mungu, nitamtukuza kwa shukrani. Jambo hili litampendeza Mwenyezi-Mungu zaidi, kuliko kumtolea tambiko ya ng'ombe, kuliko kumtolea fahali mzimamzima. Wanyonge wataona hayo na kufurahi; wanaomheshimu Mungu watapata moyo. Mwenyezi-Mungu huwasikiliza fukara; hatawasahau kamwe watu wake wafungwa. Enyi mbingu na dunia msifuni Mungu; bahari na vyote vilivyomo, msifuni. Maana Mungu atauokoa mji Siyoni, na kuijenga tena miji ya Yuda. Watu wake wataishi humo na kuimiliki; wazawa wa watumishi wake watairithi, wale wanaopenda jina lake wataishi humo.

Soma Zaburi 69

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 69:1-36