Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 44

44
Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
(Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Wakorahi)
1Ee Mungu, sisi tumesikia kwa masikio yetu,
wazee wetu wametusimulia
mambo uliyotenda nyakati zao,
naam, mambo uliyotenda hapo kale:
2Kwa mkono wako mwenyewe uliyafukuza mataifa mengine,
na mahali pao ukawakalisha watu wako;
uliyaadhibu mataifa mengine,
na kuwafanikisha watu wako.
3Watu wako hawakuitwaa nchi kwa silaha zao,
wala hawakupata ushindi kwa nguvu zao;
ila uliwasalimisha kwa mkono wako mwenyewe,
kwa kuwaangazia uso wako,
kwani wewe uliwapenda.
4Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu!
Wawajalia ushindi wazawa wa Yakobo.
5Kwa nguvu yako twawashinda maadui zetu,
kwa jina lako twawakanyaga wanaotushambulia.
6Mimi siutegemei upinde wangu,
wala upanga wangu hauwezi kuniokoa.
7Wewe ndiwe uliyetuokoa na maadui zetu;
uliwavuruga wale waliotuchukia.
8Daima tutaona fahari juu yako, ee Mungu;
tutakutolea shukrani milele.
9Lakini sasa umetuacha na kutufedhehesha;
huandamani tena na majeshi yetu.
10Umetufanya tuwakimbie maadui zetu,
nao wakaziteka nyara mali zetu.
11Umetufanya kama kondoo wanaopelekwa kuchinjwa;
umetutawanya kati ya mataifa mengine.
12Umewauza watu wako kwa bei ya chini;
wala hukupata faida yoyote.
13Umetufanya kuwa kioja kwa jirani zetu,
nao wanatudhihaki na kutucheka.
14Umetufanya tudharauliwe na watu wa mataifa;
wanatutikisia vichwa vyao kwa kutupuuza.
15Mchana kutwa fedheha yaniandama,
na uso wangu umejaa aibu tele
16kwa maneno na madharau ya wenye kunitukana,
kwa kukabiliwa na maadui zangu na walipiza kisasi.
17Hayo yote yametupata sisi
ijapokuwa hatujakusahau,
wala hatujavunja agano lako.
18Hatujakuasi wewe,
wala hatujaziacha njia zako.
19Hata hivyo umetuacha hoi kati ya wanyama wakali;
umetuacha katika giza kuu.
20Tungalikuwa tumekusahau wewe Mungu wetu,
tukamkimbilia mungu wa uongo,
21ee Mungu, ungalikwisha jua jambo hilo,
kwa maana wewe wazijua siri za moyoni.
22 # Taz Rom 8:36 Lakini kwa ajili yako twakikabili kifo kila siku;
tunatendewa kama kondoo wanaopelekwa kuchinjwa.
23Amka, ee Bwana! Mbona umelala?
Inuka! Tafadhali usitutupe milele!
24Mbona wajificha mbali nasi,
na kusahau dhiki na mateso yetu?
25Tumedidimia hata mavumbini,
tumegandamana na ardhi.
26Uinuke, uje kutusaidia!
Utukomboe kwa sababu ya fadhili zako.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 44: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia