Zaburi 4:1-8
Zaburi 4:1-8 BHN
Ee Mungu mtetezi wa haki yangu, unijibu niombapo. Nilipokuwa katika shida, wewe ulinisaidia; unionee huruma na kusikia sala yangu. Jamani, mtaniharibia jina langu mpaka lini? Mpaka lini mtapenda upuuzi na kusema uongo? Jueni kuwa Mwenyezi-Mungu amejiteulia mwaminifu wake. Mwenyezi-Mungu husikia kila ninapomwomba. Tetemekeni kwa hofu na msitende dhambi; tafakarini vitandani mwenu na kunyamaza. Toeni tambiko zilizo sawa, na kumtumainia Mwenyezi-Mungu. Wengi husema: “Laiti tungepata tena fanaka! Utuangalie kwa wema, ee Mwenyezi-Mungu!” Lakini mimi umenijalia furaha kubwa moyoni, kuliko ya hao walio na divai na ngano kwa wingi. Nalala na kupata usingizi kwa amani; ee Mwenyezi-Mungu, wewe peke yako waniweka salama.