Zaburi 4:1-8
Zaburi 4:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Ee Mungu mtetezi wa haki yangu, unijibu niombapo. Nilipokuwa katika shida, wewe ulinisaidia; unionee huruma na kusikia sala yangu. Jamani, mtaniharibia jina langu mpaka lini? Mpaka lini mtapenda upuuzi na kusema uongo? Jueni kuwa Mwenyezi-Mungu amejiteulia mwaminifu wake. Mwenyezi-Mungu husikia kila ninapomwomba. Tetemekeni kwa hofu na msitende dhambi; tafakarini vitandani mwenu na kunyamaza. Toeni tambiko zilizo sawa, na kumtumainia Mwenyezi-Mungu. Wengi husema: “Laiti tungepata tena fanaka! Utuangalie kwa wema, ee Mwenyezi-Mungu!” Lakini mimi umenijalia furaha kubwa moyoni, kuliko ya hao walio na divai na ngano kwa wingi. Nalala na kupata usingizi kwa amani; ee Mwenyezi-Mungu, wewe peke yako waniweka salama.
Zaburi 4:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo; Uliniokoa nilipokuwa katika shida; Unifadhili na kuisikia sala yangu. Enyi wanadamu, hadi lini utukufu wangu utafedheheka? Je! Mtapenda ubatili na kutafuta uongo hadi lini? Bali jueni ya kuwa BWANA amejiteulia mtauwa; BWANA husikia nimwitapo. Muwe na hofu wala msitende dhambi, Tafakarini vitandani mwenu na kutulia. Toeni dhabihu za haki, Na kumtumaini BWANA. Wengi husema, Nani atakayetuonesha mema? BWANA, utuinulie nuru ya uso wako. Umenitia furaha moyoni mwangu, Kupita yao wanapozidishiwa nafaka na divai. Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, Maana Wewe, BWANA, peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama.
Zaburi 4:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo; Umenifanyizia nafasi wakati wa shida; Unifadhili na kuisikia sala yangu. Enyi wanadamu, hata lini utukufu wangu utafedheheka? Je! Mtapenda ubatili na kutafuta uongo? Bali jueni ya kuwa BWANA amejiteulia mtauwa; BWANA atasikia nimwitapo. Mwe na hofu wala msitende dhambi, Tafakarini vitandani mwenu na kutulia. Toeni dhabihu za haki, Na kumtumaini BWANA. Wengi husema, Nani atakayetuonyesha mema? BWANA, utuinulie nuru ya uso wako. Umenitia furaha moyoni mwangu, Kupita yao wanapozidishiwa nafaka na divai. Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, Maana Wewe, BWANA, peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama.
Zaburi 4:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nijibu nikuitapo, Ee Mungu wangu mwenye haki! Nipumzishe katika shida zangu; nirehemu, usikie ombi langu. Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu kuwa aibu hadi lini? Mtapenda udanganyifu na kufuata miungu ya uongo hadi lini? Fahamuni hakika kwamba BWANA amewatenga wale wamchao kwa ajili yake; BWANA atanisikia nimwitapo. Katika hasira yako, usitende dhambi. Tulieni kimya mkiwa vitandani mwenu, mkiichunguza mioyo yenu. Toeni dhabihu zilizo haki; mtegemeeni BWANA. Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye kutuonesha jema lolote?” Ee BWANA, tuangazie nuru ya uso wako. Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi. Nitajilaza chini na kulala kwa amani, kwa kuwa wewe peke yako, Ee BWANA, waniwezesha kukaa kwa salama.