Zaburi 37:1-15
Zaburi 37:1-15 BHN
Usihangaike kwa sababu ya waovu; usiwaonee wivu watendao mabaya. Maana hao watatoweka mara kama nyasi; watanyauka kama mimea mibichi. Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kutenda mema, upate kuishi katika nchi na kuwa salama. Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu, naye atakujalia unayotamani moyoni. Mkabidhi Mwenyezi-Mungu maisha yako; mtumainie yeye naye atafanya kitu. Ataufanya wema wako ungae kama mwanga, na uadilifu wako kama jua la adhuhuri. Tulia mbele ya Mwenyezi-Mungu, mngojee kwa saburi; usihangaike juu ya wale wanaofanikiwa, watu wanaofaulu katika mipango yao mibaya. Epuka hasira wala usiwe na ghadhabu; usihangaike maana hiyo huzidisha ubaya. Watu watendao mabaya wataangamizwa, bali wanaomtumaini Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi. Bado kitambo kidogo, naye mwovu atatoweka; utamtafuta pale alipokuwa, wala hutamwona. Lakini wapole wataimiliki nchi, hao watafurahia wingi wa fanaka. Mwovu hula njama dhidi ya mwadilifu, na kumsagia meno kwa chuki. Lakini Mwenyezi-Mungu humcheka mwovu, kwani ajua mwisho wake u karibu. Waovu huchomoa panga na kuvuta pinde zao, wapate kuwaua maskini na fukara; wawachinje watu waishio kwa unyofu. Lakini panga zao zitawapenya wao wenyewe, na pinde zao zitavunjwavunjwa.