Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 37:1-15

Zaburi 37:1-15 NEN

Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu, wala usiwaonee wivu watendao mabaya, kwa maana kama majani watanyauka mara, kama mimea ya kijani watakufa mara. Mtumaini BWANA na utende yaliyo mema; Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama. Jifurahishe katika BWANA naye atakupa haja za moyo wako. Mkabidhi BWANA njia yako, mtumaini yeye, naye atatenda hili: Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko, na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri. Tulia mbele za BWANA na umngojee kwa uvumilivu; usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao, wanapotekeleza mipango yao miovu. Epuka hasira na uache ghadhabu, usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu. Kwa maana waovu watakatiliwa mbali, bali wale wanaomtumaini BWANA watairithi nchi. Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana, ingawa utawatafuta, hawataonekana. Bali wanyenyekevu watairithi nchi na wafurahie amani tele. Waovu hula njama dhidi ya wenye haki na kuwasagia meno, bali Bwana huwacheka waovu, kwa sababu anajua siku yao inakuja. Waovu huchomoa upanga na kupinda upinde, ili wawaangushe maskini na wahitaji, kuwachinja wale ambao njia zao ni nyofu. Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe, na pinde zao zitavunjwa.