Zaburi 22:19-31
Zaburi 22:19-31 BHN
Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu, usikae mbali nami; ewe msaada wangu, uje haraka kunisaidia. Iokoe nafsi yangu mbali na upanga, yaokoe maisha yangu makuchani mwa mbwa hao! Uniokoe kinywani mwa simba; iokoe nafsi yangu dhaifu toka pembe za nyati hao. Nitawasimulia ndugu zangu matendo yako; nitakusifu kati ya kusanyiko lao: Enyi mnaomcha Mwenyezi-Mungu, msifuni! Mtukuzeni enyi wazawa wote wa Yakobo! Mcheni Mungu enyi wazawa wote wa Israeli! Maana yeye hapuuzi au kudharau unyonge wa mnyonge; wala hajifichi mbali naye, ila humsikia anapomwomba msaada. Kwa sababu yako ninakusifu katika kusanyiko kubwa la watu; nitatimiza ahadi zangu mbele yao wakuchao. Maskini watakula na kushiba; wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu watamsifu. Mungu awajalie kuishi milele! Ulimwengu wote utakumbuka na kumrudia Mwenyezi-Mungu; jamaa zote za mataifa zitamwabudu. Maana Mwenyezi-Mungu ni mfalme; yeye anayatawala mataifa. Wenye kiburi wote duniani watasujudu mbele yake; wote ambao hufa watainama mbele yake, wote ambao hawawezi kudumisha uhai wao. Vizazi vijavyo vitamtumikia; watu watavisimulia habari za Mwenyezi-Mungu, watatangaza matendo yake ya wokovu. Watu wasiozaliwa bado wataambiwa: “Mwenyezi-Mungu ndiye aliyefanya hayo!”