Zaburi 104
104
Kumsifu Muumba
1 # Taz Ebr 1:7 Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu!
Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, wewe ni mkuu mno!
Umejivika utukufu na fahari.
2Umejizungushia mwanga kama vazi,
umezitandaza mbingu kama hema;
3umejenga makao yako juu ya maji ya mbingu.
Umeyafanya mawingu kuwa gari lako;
waruka juu ya mabawa ya upepo,
4waufanya upepo kuwa mjumbe wako,
moto na miali yake kuwa watumishi wako.
5Dunia umeiweka imara juu ya misingi yake,
ili isitikisike milele.
6Uliifunika dunia kwa bahari kama vazi,
na maji yakaimeza milima mirefu.
7Ulipoyakaripia, maji yalikimbia,
yaliposikia ngurumo yako yalitimka mbio.
8Yaliporomoka toka milimani hadi mabondeni,
mpaka pale mahali ulipoyatengenezea.
9Uliyawekea hayo maji mipaka,
yasije yakaifunika tena dunia.
10Umetokeza chemchemi mabondeni,
na mikondo yake ipite kati ya vilima.
11Hizo zawapatia maji wanyama wote porini.
Humo pundamwitu huzima kiu zao.
12Ndege hujenga viota vyao katika miti ya hapo,
hutua katika matawi yake na kuimba.
13Toka juu angani wainyeshea milima mvua,
nayo dunia waitosheleza kwa baraka yako.
14Waotesha nyasi kwa ajili ya mifugo,
na mimea kwa matumizi ya binadamu
ili naye ajipatie chakula chake ardhini:
15Divai ya kumchangamsha,
mafuta ya zeituni ya kumfurahisha,
na mkate wa kumpa nguvu.
16Miti mikubwa ya Mwenyezi-Mungu yapata maji ya kutosha;
naam, mierezi ya Lebanoni aliyoiotesha.
17Humo, ndege hujenga viota vyao;
korongo hufanya maskani yao katika misonobari.
18Milima mirefu ni makao ya mbuzimwitu;
na pelele hupata maficho yao miambani.
19Umeuumba mwezi utupimie majira;
jua nalo lajua wakati wa kutua.
20Waleta giza, usiku waingia;
nao wanyama wote wa porini wanatoka:
21Wanasimba hunguruma wapate mawindo,
humngojea Mungu awape chakula chao.
22Jua lichomozapo hurudi makwao,
na kujipumzisha mapangoni mwao.
23Hapo naye binadamu huenda kwenye shughuli zake;
na kufanya kazi zake mpaka jioni.
24Ee Mwenyezi-Mungu, umetenda mambo mengi mno!
Yote umeyafanya kwa hekima!
Dunia imejaa viumbe vyako!
25Mbali kule iko bahari - kubwa na pana,
ambamo kumejaa viumbe visivyohesabika,
viumbe hai, vikubwa na vidogo.
26 # Taz Zab 74:14 Ndimo zinamosafiri meli,
na lile dude Lewiyathani uliloliumba licheze humo.
27Wote wanakungojea wewe,
uwapatie chakula chao kwa wakati wake.
28Wanaokota chochote kile unachowapa;
ukifumbua mkono wako wanashiba vinono.
29Ukiwapa kisogo, wanaogopa;
ukiondoa pumzi yao, wanakufa,
na kurudi mavumbini walimotoka.
30Ukiwapulizia pumzi yako, wanaishi tena;
wewe waipa dunia sura mpya.
31Utukufu wa Mwenyezi-Mungu udumu milele;
Mwenyezi-Mungu apendezwe na matendo yake mwenyewe.
32Huitazama dunia nayo hutetemeka,
huigusa milima nayo hutoa moshi!
33Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote;
nitamsifu Mungu wangu muda wote niishipo.
34Upendezwe, ee Mwenyezi-Mungu, na mawazo yangu haya;
maana furaha yangu naipata kwako.
35Wenye dhambi waondolewe duniani,
pasiwe na waovu wowote tena!
Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu!
Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 104: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.