Methali UTANGULIZI
UTANGULIZI
Kitabu cha Methali ni Kimojawapo cha vitabu vya Agano la Kale vya maandishi ya hekima (vitabu vingine vya namna hii ni kama vile Yobu, Mhubiri, n.k.)
Kitabu chenyewe kina mkusanyo wa methali mbalimbali ambazo kwa jumla lengo lake ni kuwafunza watu maisha bora.
Kama inavyodhihirika, methali nyingine nyingi zilitungwa na washairi wa nyakati mbalimbali na nyingi zinatokana bila shaka na utamaduni wa kidini wa watu wa Israeli. Nyingine zinatajwa kuwa za mfalme Solomoni ambaye alijulikana kama mwenye hekima mkuu kabisa.
Methali hizi zinadokezea ni nini hasa maana ya kuwa na hekima kama watu wa kale wa Israeli walivyoona na kuelewa au kueleweshwa na wenye hekima wao katika nyakati hizo za kale. Aghalabu hekima kuu kupita zote ni ile itokanayo na kuwa na uhusiano mwema na Mungu. Jambo la kushika amri zake Mungu ndilo pekee lenye kufaa miongoni mwa wanadamu wote. Kutindikiwa na hekima hakutamfaa mtu kitu chochote; tena kuishi kipumbavu ni dhambi na chanzo cha upotovu. Hekima ya watu wa Israeli ilitilia mkazo kuwajibika kwa kila mtu binafsi, jambo ambalo kama likikosekana kati ya watu, ulinzi wa Mungu kwa watu wake hutoweka.
Kuwa na hekima si jambo geni kwa watu. Hekima hufunzwa hata watoto wadogo kwa vitendawili na misemo ambayo hupatikana katika makabila mbalimbali ulimwenguni.
Mambo yaliyomo katika kitabu hiki yanaweza kugawanywa kwa namna mbalimbali:
Katika sura 1–9 kuna utangulizi juu ya hekima. Katika sehemu hii tunaelezwa kinaganaga kazi ya hekima. Hekima hapa inazungumziwa kana kwamba ni “mwanamke” ambaye anawaalika wote waishi kulingana na busara na akili timamu.
Katika sura 10–29 kuna mkusanyo wa methali zinazojulikana kama za mfalme Solomoni (10:1–22:16; 25:1–29:27), pamoja na nyingine ambazo zatoka kwa wenye hekima wengine (22:17–24:34).
Katika sura 30–31 kuna visehemu vinne tofauti, viwili vikitupa habari juu ya fikira na mawaidha ya wenye hekima ambao huenda hawakuwa Wayahudi (30:11-14 na 31:1-9).
Iliyochaguliwa sasa
Methali UTANGULIZI: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.