Methali 20:1-15
Methali 20:1-15 BHN
Divai huleta dhihaka na kileo huleta ugomvi; yeyote anayevutiwa navyo hana hekima. Ghadhabu kali ya mfalme ni kama simba angurumaye; anayemkasirisha anayahatarisha maisha yake. Ni jambo la heshima kuepa ugomvi; wapumbavu ndio wanaogombana. Mvivu halimi wakati wa kulima; wakati wa mavuno atatafuta asipate chochote. Fikira za mtu zimefichika kama kilindi cha maji; lakini mtu mwenye busara ajua kuzichota humo. Watu wengi hujivunia kuwa wema, lakini mwaminifu wa kweli apatikana wapi? Mtu mwadilifu akiishi kwa unyofu; watoto wake atakaowaacha watabarikiwa. Mfalme mwema aketipo kutoa hukumu, huupepeta uovu wote kwa macho yake. Nani athubutuye kusema: “Nimeutakasa moyo wangu; mimi nimetakasika dhambi yangu?” Mizani ya udanganyifu na vipimo vya udanganyifu, vyote ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu. Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni njema na aminifu. Sikio lisikialo na jicho lionalo, yote mawili kayafanya Mwenyezi-Mungu. Usipende kulala tu usije ukawa maskini; uwe macho nawe utakuwa na chakula kingi. “Hakifai, hakifai”, mnunuzi hulalamika, lakini akiondoka hujisifu amepunguziwa bei. Kuna dhahabu na wingi wa mawe ya thamani kubwa; lakini cha thamani kubwa zaidi ni maneno ya busara!