Wafilipi 2:1-17
Wafilipi 2:1-17 BHN
Je, maisha yenu katika Kristo yanawapeni nguvu? Je, upendo wake unawafarijini? Je, mnao umoja na Roho Mtakatifu na kuoneana huruma na kusikitikiana nyinyi kwa nyinyi? Basi, ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na fikira moja, upendo mmoja, moyo mmoja na nia moja. Msifanye chochote kwa moyo wa fitina au kwa majivuno ya bure; muwe na unyenyekevu nyinyi kwa nyinyi, na kila mmoja amwone mwenzake kuwa bora kuliko yeye mwenyewe. Pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu bali faida ya mwenzake. Muwe na msimamo uleule aliokuwa nao Kristo Yesu: Yeye, kwa asili alikuwa daima Mungu; lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kungangania kwa nguvu. Bali, kwa hiari yake mwenyewe, aliachilia hayo yote, akajitwalia hali ya mtumishi, akawa sawa na wanadamu, akaonekana kama wanadamu. Alijinyenyekesha na kutii mpaka kufa, hata kufa msalabani. Kwa sababu hiyo Mungu alimkweza juu kabisa, akampa jina lililo kuu kuliko majina yote. Ili kwa heshima ya jina la Yesu, viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu, vipige magoti mbele yake, na kila mtu akiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba. Wapenzi wangu, nilipokuwa nanyi mlinitii daima, na hata sasa niwapo mbali nanyi endeleeni kutii. Fanyeni kazi kwa hofu na tetemeko kwa ajili ya ukombozi wenu, kwani Mungu ndiye afanyaye kazi daima ndani yenu, na kuwapeni uwezo wa kutaka na kutekeleza mambo yanayopatana na mpango wake mwenyewe. Fanyeni kila kitu bila kunungunika na bila ubishi, ili mpate kuwa watu safi, wasio na lawama, kama watoto wanyofu wa Mungu wanaoishi katika ulimwengu mbaya na uliopotoka. Mtangara kati yao kama nyota zinavyoliangaza anga, mkishika imara ujumbe wa uhai. Na hapo ndipo nami nitakapokuwa na sababu ya kujivunia katika siku ile ya Kristo, kwani itaonekana dhahiri kwamba bidii yangu na kazi yangu havikupotea bure. Hata ikiwa nitatolewa mhanga pamoja na imani yenu iliyo tambiko kwa Mungu, basi, nafurahi sana na kuwashirikisha nyinyi nyote furaha hiyo.